1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waomba msaada kwa ajili ya Syria

19 Desemba 2014

Umoja wa Mataifa umeomba kiasi cha Dola bilioni 8.4 kwa ajili ya kutoa msaada wa dharura wa kibinaadamu kwa takribani watu milioni 18 wa Syria na kuzunguka ukanda huo unaokumbwa na mzozo.

https://p.dw.com/p/1E7ME
Antonio Gutteres akiwa na Valerie Amos
Antonio Gutteres akiwa na Valerie AmosPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Pedersen

Ombi hilo limetolewa jana na maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini Berlin, Ujerumani kwenye mkutano wa wafadhili na wamesema msaada huo unahitajika haraka nchini Syria, na katika nchi na jamii zinazopambana kuwahifadhi wakimbizi wa Syria.

Kwa mara ya kwanza ombi hilo la Umoja wa Mataifa, linahusisha msaada wa chakula cha kuwapa nguvu na kurudisha afya, malazi, msaada mwingine wa kibinaadamu pamoja na msaada wa maendeleo.

Maafisa wa umoja huo wamesema Dola bilioni 2.9 zinahitajika ili kuwasaidia watu milioni 12.2 walioko ndani ya Syria kwa mwaka 2015, na Dola bilioni 5.5 zinahitajika kwa ajili ya Wasyria walioomba hifadhi ya ukimbizi kwenye nchi jirani na zaidi ya watu milioni moja katika jamii zinazowahudumia.

Wakimbizi wa Syria wakiwa nchini Lebanon
Wakimbizi wa Syria wakiwa nchini LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/Mohammed Zaatari

Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa mjini Berlin, ni kikubwa zaidi ya kile kilichoombwa mjini Geneva, mwanzoni mwa mwezi huu, msaada ambao haukujumuisha fedha kwa ajili ya nchi jirani. Hata hivyo, umoja huo umeshapata nusu tu ya kiwango kilichoombwa mwaka huu 2014.

Mahitaji ya kibinaadamu yanaongezeka

Kamishna Mkuu wa Shirika linalowahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa-UNHCR, Antonio Gutteres ameonya kuwa wakimbizi na watu wasio na makaazi ndani ya Syria hawana akiba na nchi zinazowahifadhi ziko katika wakati mgumu, hivyo utaratibu mpya wa misaada unahitajika.

''Mahitaji ya kibinaadamu duniani yanaongezeka, na yanaongezeka kwa kasi. Na ni wazi kwamba fedha zilizopo kwa ajili ya kutimiza mahitaji hayo, haziongezeki kulingana na kukua kwa kasi ya mahitaji,'' alisema Gutteres.

Naye Mkuu wa shughuli za kibinadamu na misaada ya dharura ya Umoja wa Mataifa, Valerie Amos amesema Syria imetoka katika taifa la watu wenye kipato cha kati na kutumbukia kwenye nchi inayopambana na umaskini mkubwa. Amesema watu walioathirika na mzozo wanahitaji chakula, malazi, maji, dawa na ulinzi, lakini pia wanahitaji msaada wa kujenga upya maisha yao, kupata elimu na huduma za afya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amesema mzozo wa kibinaadamu nchini Syria na kwenye nchi jirani unatoa kitisho kwa utulivu wa ukanda wote. Amesema huo ni mwito wa mshikamano kwa mataifa yote na nchi yake iko tayari kutoa sehemu yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Institut für Auslandsbeziehungen / Dietmar Gust

Mwezi Oktoba, Ujerumani ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria, ambapo wajumbe waliahidi kuongeza msaada wa kifedha wa muda mrefu katika nchi kama vile Lebanon na Jordan, ambazo zinakabiliana na mamilioni ya wakimbizi wa Syria wanaoingia kwa kasi kwenye nchi hizo.

Kiasi watu 200,000 wamekufa na karibu nusu ya idadi ya wakaazi wa Syria hawana makaazi kutokana na mgogoro ulioanza kwa maandamano ya kuipinga serikali ya Rais Bashar al-Assad mwaka 2011 na kugeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu