1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wakaribisha usitishwaji mapigano Gaza

27 Agosti 2014

Anga ya Ukanda wa Gaza imesalia tulivu hii leo wakati mpango wa kusitisha mapigano kwa muda mrefu baina ya Israel na Wapalestina ukianza kutekelezwa baada ya siku 50 za machafuko na umwagaji damu

https://p.dw.com/p/1D1i6
Palästinenser feiern Waffenstillstand
Picha: Reuters

Hatua hiyo ya kuweka chini silaha iliyoongozwa na Misri imepongezwa na viongozi wa ulimwengu. Mamilioni ndani na nje ya Ukanda wa Gaza wamefurahia usiku wa kwanza wa amani na utulivu ambapo hakuna mashambulizi yoyote yaliyofanywa katika ardhi ya Gaza, wala maroketi ya Wapalestina yaliyovurumishwa kuelekea Israel.

Mjini Gaza, sherehe ziliandaliwa punde baada ya kuanza kutekelezwa mpango huo wa kusitisha mapigano jana jioni, na kuendelea hadi usiku wa manane huku wakaazi milioni 1.8 wakishangilia mitaani kumalizika kwa wiki saba za mgogoro huo uliosababisha umwagaji damu.

Bildergalerie Gaza Israel Beerdigung Israelischer Soldat
Jamaa na marafiki wakihudhuria mazishi ya mwnajeshi wa Israel aliyeuawa katika eneo la EshkalonPicha: Reuters

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amesema baada ya makubaliano hayo kufaynwa kuwa msaada wa kiutu unapelekwa katika eneo hilo. Naye msemaji wa serikali ya Israel Mark Regev amesema anataraji kuwa mpango huo utaheshimiwa

Marekani imeuunga mkono kikamilifu mpango huo ulioongozwa na Misri, huku Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni John Kerry akizitaka pande zote mbili “kuyaheshimu kikamilifu masharti yote ya makubaliano hayo”.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliupongeza akisema anataraji kuwa utatoa nafasi ya mchakato wa kisiasa ambao hatimaye utaleta amani ya kudumu kati ya Israel na Wapalestina.

Uingereza pia imepongeza juhudi za Misri kuongoza mazungumzo ya upatanishi ili kumaliza umwagaji zaidi wa damu.

Israel kuondoa vizuizi katika Ukanda wa Gaza

Chini ya mpango huo, Israel itaondoa vizuizi ilivyoweka katika Ukanda wa Gaza kwa kipindi cha miaka minane. Hatua ya kuondoa mzingiro wa Ukanda huo imekuwa ni moja ya masharti muhimu yaliyokuwa mwiba katika mazungumzo ya Misri, huku Hamas ikiyasifu makubaliano hayo kuwa ni “ushindi kwa upinzani” kutoka upande Israel.

Bildergalerie Gaza Israel Beerdigung Hassan Ashour West Bank Ashour
Waombolezaji wakiubeba mwili wa kijana wa Kipalestina aliyeuawa katika mji wa NablusPicha: Reuters

Kiongozi wa ujumbe wa Wapalestina katika mazungumzo hayo Azzam al-Ahmed amesema miongoni mwa masuala yaliyokubaliwa ni kufungua tena vivuko ili kuruhusu bidhaa na msaada wa kiutu na chakula kuingia Gaza, pamoja na bidhaa za matibabu na vifaa vya kukarabati huduma za maji, umeme na mitandao ya simu za mkononi.

Aidha, vikwazo kuhusu shughuli za uvuvi vitaondolewa “maramoja” huku mashua zikiruhusiwa kuvua samaki kwa umbali wa hadi kilomita 10 mbali na pwani katika bahari ya mediterenia.

Na kisha baadaye, mnamo tarehe ambayo haijatangazwa, pande hizo mbili zitarejea mjini Cairo kujadili “ubadilishanaji wa wafungwa wa Kipalestina na wa miili ya wanajeshi wa Israel waliouawa” wakati wa mgogoro huo.

Takribani Wapalestina 2,143 na Waisrael 70 wameuawa tangu mzozo huo ulipozuka Julai 8 wakati Israel ilipoanzisha operesheni ya kusitisha mashambulizi yanayovurumishwa nchini mwake kutokea Gaza.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa karibu asilimia 70 ya wahanga wa Palestina walikuwa raia, wakati 64 kati ya Waisrael waliouawa walikuwa wanajeshi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo