1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yasema tayari iko vitani na Urusi

Admin.WagnerD1 Septemba 2014

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Valeriy Geletey amesema tayari vita vikali vimeanza Kati ya nchi yake na Urusi, huku NATO ikijiimarisha katika nchi za Ulaya ya Mashariki kutuliza hofu ya wanachama wapya.

https://p.dw.com/p/1D4z0
Magari ya kivita ya Ukraine yakielekea msitari wa mbele
Magari ya kivita ya Ukraine yakielekea msitari wa mbelePicha: Reuters

Umoja wa kujihami wa NATO unaazimia kuongeza idadi ya wanajeshi na kiwango cha vifaa vya kijeshi katika nchi wanachama zilizoko mashariki mwa bara Ulaya, kuzihakikishia usalama nchi hizo mbele ya kitisho kinachotokana na hatua za mienendo ya Urusi nchini Ukraine.

Katibu mkuu wa umoja huo Anders Fogh Rasmussen amesema mkutano wa NATO utakaofanyika huko Wales nchini Uingereza, utaviweka vikosi vyao katika hali ya utayarifu wa kupigana vita katika muda wa siku chache sana.

Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amesema hatua hizo zitakazochukuliwa na umoja huo zitahakikisha kwamba vikosi vyao vinazo silaha za kutosha mahali vinakohitajika na kwa muda muafaka, na kuongeza kuwa vikosi hivyo vitabaki mashariki mwa Ulaya kwa muda wote vitakapohitajika.

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: picture-alliance/AP Photo

Hofu yatanda Ulaya Mashariki

Mzozo wa Ukraine umesababisha hofu miongoni mwa nchi wanachama wapya wa NATO kama vile Poland na mataifa ya ukanda wa Baltic, ambazo kwa miongo kadhaa zilitawaliwa chini ya ushawishi wa Urusi, wakiwa na wasiwasi kwamba mtutu wa nchi hiyo unawezwa kugeuzwa na kuziweka katika kilengeo.

Katika juhudi za kutuliza hofu hizo, NATO imekuwa ikitumia makundi madogo ya wanajeshi na ndege za kivita kufanya doria katika nchi hizo, na Marekani imetoa hakikisho kwamba umoja huo utatekeleza majukumu yake katika kuilinda nchi yoyote mwanachama itakayoshambuliwa.

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema Urusi haitaishambulia Ukraine.

''Hakutakuwepo uingiliaji kijeshi nchini Ukraine, wito wetu pekee ni kutaka suluhisho la amani katika mgogoro huu mkubwa, na kila hatua tunayoichukua huelekea kwenye mwafaka wa kisiasa.'' Amesema Lavrov.

Waasi wataka hadhi maalum

Wakati huo huo waasi wa mashariki mwa Ukraine wamesema wanataka hadhi maalum kwa eneo lao, ambayo itazingatia haki yao ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Urusi pamoja na eneo la kibiashara linaloongozwa na nchi hiyo.

Waasi wa mashariki mwa Ukraine wanataka hadhi maalum kwa eneo lao
Waasi wa mashariki mwa Ukraine wanataka hadhi maalum kwa eneo laoPicha: picture-alliance/AP Photo

Wachambuzi wanasema madai hayo ya waasi ni sawa na kuigawa Ukraine katika sehemu mbili, ikitiliwa maanani kwamba serikali mjini Kiev inanuia kufunganisha uchumi wake na ule wa Umoja wa Ulaya. Urusi imeonya kwamba ikiwa azma hiyo ya Ukraine itatekelezwa, uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hiyzo mbili utaathirika vibaya.

Akizungumzia mzozo huo wa Ukraine Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekariri kauli yake ya awali kwamba hakuna suluhisho la kijeshi katika mzozo huo, akitetea msimamo wa nchi za Ulaya kuiwekea vikwazo Urusi kuidhihirishia nchi hiyo kuwa vitendo vyake nchini Ukraine havitavumiliwa.

Lakini Muda mfupi uliopita waziri wa ulinzi wa Ukraine Valeriy Geletey ametangaza kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Facebook, kwamba tayari vita vikali vimeripuka kati ya nchi yake na Urusi, na kuonya kuwa hasara ya maisha itakayotokana na vita hivyo itakuwa katika kiwango cha maelfu, au hata makumi ya maelfu. Ametahadharisha kwamba vita hivyo vitaleta uharibifu ambao haujashuhudiwa barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape

Mhariri:Yusuf Saumu