1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yakaribisha vikwazo vipya dhidi ya Urusi

Admin.WagnerD30 Julai 2014

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Pavlo Klimkin, amekaribisha vikwazo vipya vilivyotangazwa na Marekani na Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, na kusema Kiev haitaishambulia miji inayodhibitiwa na waasi.

https://p.dw.com/p/1CmIb
Russland Sanktionen Waldimir Putin und Igor Setschin
Picha: picture-alliance/AP Images

Waziri Klimkin ambaye alikuwa na siku mbili za mazungumzo mjini Washinton, ukiwemo mkutano na makamu wa rais Joe Biden, alisema kuwa anarejea mjini Kiev akiwa na ujumbe wa wazi kwamba Marekani na Umoja wa Ulaya zinazungumza kwa sauti moja kuiunga mkono Ukraine.

Klimkin alisema anaunga mkono wazo la kuitisha mkutano wa kimataifa kukomesha miezi kadhaa ya machafuko, na kuongeza kuwa ni suluhu ya kisiasa tu itakayokomesha mgogoro huo.

"Kilicho muhimu ni kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ya pande zote kwa nia ya kurejesha uhuru wa mipaka ya Ukraine," alisema na kuongeza kuwa "tunahitaji kupiga hatua, tunahitaji kuwaachiwa kwa wafungwa haraka iwezekanvyo, na pia ni suala la heshima ya kiutu."

Waziri Pavlo Klimkin.
Waziri Pavlo Klimkin.Picha: picture-alliance/dpa

Vikwazo vikali zaidi

Marekani na Umoja wa Ulaya zilitangaza vikwazo vikali zaidi vinavyozilenga sekta muhimu za fedha, silaha na nishati, lakini benki kuu ya Urusi imeahidi kuzisaidia taasisi zilizolengwa na vikwazi hivyo.

Rais Barack Obama alionya kuwa vikwazo hivyo vipya vitauumiza sana uchumi wa Urusi, ambao tayari unashuka kuelekea sifuri, na kusema Washington ilikuwa na ushahidi kwama mizingia ya Urusi ilivishambulia vikosi vya Ukraine.

Alisema mataifa washirika sasa wamedhamiria kuchukuwa hatua za pamoja baada ya kuangushwa kwa ndege ya ndege ya Malaysia katika anga ya Ukraine mwezi huu, na waasi wanaoelemea upande wa Urusi.

Siyo vita baridi

Lakini alikanusha kuwa mataifa ya magharibi yalikuwa yanaanzisha vita vingine baridi dhidi ya Urusi. "Hii siyo vita baridi, hili ni suala makhsusu linalohusu kutokuwa tayari kwa Urusi kutambua kwamba Ukraine inaweza kujiongoza. Nadhani ukimsikiliza rais Petro Poroshenko, ukiwasikia raia wa Ukraine wanasisitizaa kuwa wanataka uhusiano mzuri na Urusi.

"Wasichokubali ni Urusi kuwapatia silaha wanaofanya uharibifu ndani ya Ukraine, na hivyo kudhoofisha uwezo wa Ukraine kujitawala kwa amani," alisema Obama.

Wakati vikwazo hivyo vimesanifiwa kizidhoofisha ipasavyo sekta muhimu za uchumi wa Urusi na watu wa karibu wa rais Putin, kulikuwa na onyo kuwa uchumi wa Ulaya pia utaathiriwa na vikwazo hivyo.

Benki kuu Urusi yaahidi kusaidia

Wizaraya fedha ya Marekani ilizitaja Benki ya VTB, benki yake tanzu ya Moscow, na benki ya kilimo ya Urusi kuwa taasis tatu zinazojumlishwa kwenye ordha ya vikwazo dhidi ya Urusi. Vikwazo hivyo pia vinailenga kampuni ya ujenzi wa Meli, ambayo inatengeneza nyambizi za mashambulizi na meli za kivita.

RAis Barack Obama.
RAis Barack Obama.Picha: Win McNamee/Getty Images

Lakini katika taarifa iliyowekwa mtandaoni, benki kuu ya Urusi imeahidi kuchukuwa hatua zinazostahiki kuzisaidia taasisi hizo, huku Benki ya Moscow ikisema bishara yake haijaathirwa na vikwazo hivyo.

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Australia Tonny Abbot, alisema siku ya Jumatano kuwa hafikirii kufuata nyayo za Marekani na Umoja wa Ulaya, kuiongezea vikwazo Urusi kwa wakati huu ambapo serikali yake imeelekeza nguvu kuipata miili ya wahanga wa ajali ya ndege ya Malaysia.

Waziri mkuu Abbot amekuwa na mazungumzo mara kadhaa kwa njia ya simu na rais Putin, na amemsifu jinsi alivyoshirikiana kuhakikisha upatikanaji wa miili ya wahanaga wa ajali hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,rtre,afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo