1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yajipanga kulipiza mauaji ya Haines

Mohammed Khelef14 Septemba 2014

Baada ya kundi linalojiita 'Dola la Kiislamu' kusambaza vidio ya kukatwa kichwa kwa raia wa Uingereza, Waziri Mkuu David Cameron ameitisha mkutano wa dharura kujadiliana hatua za kuchukuwa.

https://p.dw.com/p/1DC2P
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Haines.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Haines.Picha: Reuters/James Glossop

Kikao cha Cameron na kamati maalum ya dharura kinachofahamika kama Cobra kinafanyika baada ya vidio hiyo kuonesha David Haines akikatwa kichwa, huku ikitishia kumuua mwengine. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza inasema haina sababu ya kutilia shaka uhakika wa vidio hiyo.

Bado haijafahamika kile kitakachoamuliwa na kikao hicho, lakini wachambuzi wa mambo wanasema ni wazi uamuzi utakuwa ni kulipeleka jeshi la Uingereza moja kwa moja kwenye vita dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu.

Cobra ni kikao cha juu kabisa cha masuala ya usalama na washiriki wake ni pamoja na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka jeshini na idara ya ujasusi, ofisi ya mambo ya nchi za nje na wizara ya mambo ya ndani. Awali Cameron alikilaani kitendo cha kukata kichwa kwa Haines, akikielezea kuwa "uovu mkubwa".

ACTED yalaani mauaji ya mfanyakazi wake

Shirika la misaada ambalo lilikuwa limemuajiri Haines, Agency for Technical Cooperation and Development (ACTED) lenye makao yake makuu Paris, Ufaransa, limetoa tamko la kusikitishwa na mauaji hayo na kulilaani vikali kundi la Dola ya Kiislamu.

David Haines katika uhai wake.
David Haines katika uhai wake.Picha: DW

"Mauaji ya kutisha dhidi ya David, mfanyakazi wa misaada ya kibinaadamu, ni dhidi ya kila msingi wa ubinaadamu, na yanaiathiri jamii nzima ya misaada ya kiutu," ilisema taarifa hiyo huku ikiapa kuendelea kwa huduma za shirika hilo kwa wale wenye matatizo.

Haines anakuwa raia wa tatu kutoka mataifa ya Magharibi kukatwa kichwa ndani ya wiki chache na kundi hilo, ambalo limechukuwa udhibiti wa eneo kubwa la Syria na Iraq, wengine wakiwa ni waandishi wa habari wa Kimarekani, James Foley na Steven Sotloff.

Australia yatuma wanajeshi

Katika hatua nyengine, Australia imekuwa nchi ya kwanza kuelezea idadi ya wanajeshi na ndege inazotuma kwenye muungano wa kupambana na wanamgambo wa 'Dola la Kiislamu' unaoongozwa na Marekani. Waziri Mkuu Tony Abbott alisema siku ya Jumapili (14 Septemba) kwamba wanajeshi 600, ndani yake wakiwamo 400 wa angani na 200 wa kikosi maalum watapelekwa kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.
Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.Picha: Reuters

Abbott alisema pamoja na wanajeshi hao, Australia itatuma ndege nane za kivita, moja ya kutoa tahadhari na udhibiti na moja ya kujazia mafuta ndege zikiwa angani. Kwa mujibu wa waziri mkuu huyo, yote hayo yatafanyika ndani ya siku chache zijazo.

Hata hivyo, Abbott alisema kwamba bado hajafanya maamuzi juu kutuma wanajeshi wa moja kwa moja wa ardhini kukabiliana na wanamgambo wa Dola ya Kiislamu, lakini haondoi uwezekano huo. Tayari timu maalumu ya washauri wa kijeshi imeundwa kushauriana na vikosi vya Iraq na vyombo vyengine vya usalama kwenye mapambano hayo.

Tangazo hilo linakuja siku mbili baada ya Australia kupandisha kiwango cha kitisho cha ugaidi katika ardhi yake, huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kwa wapiganaji wa jihadi wa Australia wanaorejea nyumbani baada ya kupigana Syria na Iraq.

Kerry aendelea na ziara yake Mashariki ya Kati

Tangu Rais Barack Obama wa Marekani kutangaza mkakati wake wa kukabiliana na kundi la "Dola la Kiislamu" katikati ya wiki iliyopita, Waziri wake wa Mambo ya Nje, John Kerry, amekuwa kwenye ziara ya mataifa ya Kiarabu, akisaka uungwaji mkono wa mataifa hayo kwenye operesheni hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) na mwenzake wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu.Picha: Reuters/U. Bektas

Tayari mataifa 10 ya Kiarabu - zikiwemo Misri, Iraq, Jordan, Lebanon, Oman, Bahrain, Saudi Arabia na Qatar - yamekubali kujiunga na kile kilichopewa jina la "Muungano wa Wenye Dhamira" ya kulishinda kundi hilo la kigaidi.

Saudi Arabia kwa upande wake imetangaza kuwa tayari kuwa mwenyeji wa kambi za mafunzo kwa waasi wa Syria wenye msimamo wa wastani wanaopambana na kundi hilo na pia serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Hata hivyo, kikwazo hadi sasa kimekuwa ni Uturuki ambayo licha ya kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na jirani wa Iraq na Syria liliko kundi la Dola la Kiislamu, imekataa kujiunga na kampeni ya kijeshi ikihofia usalama wa raia wake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Amina Abubakar