1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yakutana na ujumbe wa kimataifa

Mohammed Khelef29 Januari 2015

Serikali mpya ya Ugiriki inakutakana kwa mara ya kwanza na mkuu wa bunge la Umoja wa Ulaya, ikiwa ni siku moja tu baada ya kutangaza hatua za kujiondoa kwenye mpango wa kubana matumizi.

https://p.dw.com/p/1ESWD
Serikali mpya ya Ugiriki baada ya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri.
Serikali mpya ya Ugiriki baada ya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Spika wa Bunge la Ulaya, Martin Shulz, atakuwa wa kwanza kukutana Alhamisi (tarehe 29 Januari) na viongozi hao wapya wa Ugiriki na baadaye atafuatia rais wa kile kiitwacho Eurogroup, ambayo ni klabu ya mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Kabla ya mikutano hiyo, tayari Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, alisharejelea msimamo wa Umoja huo kwamba kulifuta deni kubwa la Ugiriki haikuwa njia ya kufuatwa na badala yake kuitaka serikali mpya ya Ugiriki "kuwaheshimu wenzao wa Ulaya."

"Hata kama mipango mipya inawezekana, lakini kamwe hatutaondosha msingi uliopo. Tspiras anaahidi kwamba Ugiriki haitakubaliana tena na hatua za kubana matumizi. Nchi za euro zinajibu kwamba hakutakuwa tena na mkopo ikiwa Ugiriki itakhalifu ahadi zake," alisema Juncker kwenye mahojiano yaliyochapishwa na gazeti la La Figaro la Ufaransa siku ya Alhamisi (tarehe 29 Januari).

Katika kile kinachoonekana kutekeleza ahadi zake za kampeni siku mbili tu baada ya kuapishwa, hapo jana Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, alitangaza kuziondoa hatua za kubana matumizi ambazo zinaambatana na mkopo wa euro bilioni 240 iliopewa nchi hiyo na wafadhili wa kimataifa.

Serikali yake inasema inazuia mipango yote ya kuuza hisa kwenye bandari za Piraeus na Thessaloniki, na kwamba ingelisimamisha ubinafishaji wa kampuni kubwa za umeme na mafuta.

China, Ujerumani zaonya

China, ambayo kampuni yake ya COSCO imeingia ubia kwenye bandari ya Piraeus, imeionya serikali mpya ya Ugiriki juu ya hatua yoyote itakayoathiri uwekezaji huo. Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China, Shen Danyang, amewaambia waandishi wa habari hili leo mjini Beijing, kwamba serikali haitakaa kimya.

Serikali mpya ya Ugiriki baada ya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri.
Serikali mpya ya Ugiriki baada ya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

"Wizara ya Biashara itaendelea kufuatilia kwa karibu muelekeo wa sera za serikali mpya ya Ugiriki, itakuwa na mawasiliano na serikali hiyo, na inaitolea wito kwamba ilinde haki za kisheria za kampuni za China, ikiwemo Cosco," alisema Shen.

Mjini Berlin, Waziri wa Uchumi ambaye pia ni Naibu Kansela, Sigmar Gabriel, amesema serikali hiyo ya Ugiriki haiwezi kufanya mageuzi makubwa ya ghafla kwenye sera zake za uchumi na kisha ikatarajia kuwa mataifa mengine ya Ulaya yatalipia gharama zake.

Akizungumza bungeni asubuhi ya leo, Gabriel ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha SPD, amesema Ugiriki haipaswi kuwa mzigo kwa mataifa mengine ya Ulaya kwa ajili ya siasa zake za ndani, akiongeza kwamba ni hali ya ukosefu wa usawa ndani ya jamii ya Ugiriki yenyewe ndio chanzo na matatizo yanayolikumba taifa hilo, ambalo serikali yake mpya inajaribu kutupia lawama viongozi wa nje.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf