1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras: Tunataka muafaka unaozingatia hali halisi

31 Machi 2015

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ameliambia bunge la nchi yake kwamba serikali yake inataka muafaka wenye kujali ukweli wa mambo, katika juhudi za kuufufua uchumi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1Ezuq
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/Y. Kolesidis

Tsipras aliyasema hayo katika hotuba yake mbele ya bunge jana jioni, wakati wakopeshaji wakuu wa nchi yake, yaani Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF na Umoja wa Ulaya wakiichunguza orodha ya mageuzi yanayopendekezwa na serikali ya Ugiriki. Tsipras alisema ingawa wanataka makubaliano yenye kuzingatia hali halisi, hawatatia saini kile alichokilinganisha na kusalimu amri bila masharti yoyote.

Waziri Mkuu huyo wa Ugiriki alisema nchi yake inakabiliwa na shinikizo lisiloambatana na huruma yoyote, na kudai kwamba hiyo ndio sababu serikali yake inaungwa mkono na umma wa nchi hiyo. Aliwaambia aliwatupia mpira wabunge, akisema uamuzi wa kusaini mkataba na wakopeshaji ni wao.

''Wakopeshaji wamekubali malengo yetu ya kupata ziada katika bajeti mwaka 2015, kwa mashariti kwamba mazungumzo juu ya deni letu yaanze mwezi Juni. Kwa hiyo, ili kuweza kuufunga ukurasa huu milele, hakuna makubaliano mapya yaliyosainiwa. Chaguo la kusaini makubaliano hayo ni lenu, sio letu.'' Amesema Tsipras.

Bila ukweli deni halilipiki

Kiongozi huyo wa serikali mpya ya Ugiriki alikariri mahitaji ya kulijadili upya deni la nchi hiyo, ambalo kwa wakati huu ni sawa na asilimia 177 ya pato la ndani la taifa, akisema bila hali hiyo, haitawezekana kulipa deni hilo. Tsipras amesema mazungumzo na IMF na Umoja wa Ulaya yataanza mara tu makubaliano ya sasa yatakapomaliza muda wake mwezi Juni, na kuongeza kuwa majadiliano juu ya makubaliano mengine yatahusu mpango wa maendeleo ya uchumi wa Ugiriki.

Uchumi wa Ugiriki umeporomoka na unahitaji mkopo ili kufufuliwa
Uchumi wa Ugiriki umeporomoka na unahitaji mkopo ili kufufuliwaPicha: Reuters/Y. Behrakis

Upande wa upinzani nchini humo umeishutumu serikali ya bwana Tsipras kutoheshimu ahadi ilizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi, ukisema waziri mkuu huyo amekubali kisirisiri kuridhia sera za kubana matumizi zinazotakiwa na wakopeshaji, ili kupata awamu nyingine ya mkopo kabla ya mwisho wa mwezi Aprili.

Upinzani unatilia shaka

Mbunge wa upinzani Effie Christofilopoulou ambaye alihudhiria kikao kilichohutubiwa na Tsipras, alisema hawana uhakika kama makubaliano yako njiani.

''Tunayo matumaini kuwa makubaliano yatafikiwa, lakini sidhani yatapatikana. Tusubiri tuone, hilo ndilo sisi kama upinzani tunaloweza kulifanya. Tutaunga mkono makubaliano, lakini ni kazi yao kuyafikia.''

Hata hivyo, chanzo kutoka ndani ya Umoja wa Ulaya kiliiambia tovuti moja ya habari nchini Ugiriki, kwamba mapendekezo ya Ugiriki bado yanafanyiwa kazi, na kwamba ukosefu wa utalaamu kwa upande wa Ugiriki unakwamisha mambo.

Mnamo mwezi Aprili, Ugiriki inahitaji mkopo mpya wa euro bilioni 2.4 na wakati huo huo kulipa deni la kiasi cha euro milioni 820, zikiwemo milioni 460 inazodaiwa na IMF.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape/DW website

Mhariri: Iddi Ssessanga