1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu zajiandaa kwa kibarua cha ulaya

20 Oktoba 2014

Ligi ya mabingwa barani Ulaya , Champions League inarejea uwanjani tena Jumanne na Jumatano wakati kukiwa na mechi kadhaa za kukata na shoka katika viwanja mbalimbali

https://p.dw.com/p/1DYtW
Deutschland Fußball Champions League Bayern München
Picha: C. Strache/AFP/Getty Images

Kocha wa klabu ya Roma ya Italia ameahidi kuipatia Bayern Munich ya Ujerumani makaribisho ambayo hawatayasahau, wakati mafahali hao wa Bundesliga wakiwasili katika mji huo mkuu wa Italia kuvuruga mwanzo mzuri wa timu hiyo , "Giallorossi" katika kampeni ya Champions League msimu huu.

Roma ilijipasha moto kwa ajili ya pambano hilo la kesho katika kundi E kwa kuiadhibu Chievo kwa mabao 3-0 siku ya jumamosi na licha ya ushindi wa kishindo wa Bayern dhidi ya Werder Bremen katika Bundesliga , kocha Garcia wa Roma anataka uwanja wao wa "Stadio Olimpico" kuwapa wenyeji kitu cha ziada.

Italien Fußball Champions League AS Roma
AS Roma wa Italia wanawakaribisha miamba wa Ujerumani Bayern MunichPicha: F. Monteforte/AFP/Getty Images

Bayern inasafiri kwenda Roma ikiwa inaongoza kundi hilo baada ya kupata ushindi mara mbili dhidi ya Manchester City na CSKA Moscow, na Roma ilipata ushindi mnono dhidi ya CSKA na kutoka sare na Manchester City, ikiwa inashikilia nafasi ya pili. Manchester City iko nyumbani kwa CSKA Moscow, ambapo itacheza bila mashabiki uwanjani kutokana na adhabu inayoikabili CSKA. Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini amesema kucheza bila mashabiki hakutaisaidia timu yake katika mchezo huo muhimu wa Champions League kesho.

Roberto di Matteo alikwisha nyanyua juu taji hilo la Champions League mwaka 2012 akiwa kocha mlezi wa Chelsea lakini kibarua kiliota majani katikati ya msimu wake kamili akiwa kocha wa timu hiyo. Hivi sasa amerejea katika dimba hilo la mabingwa akiwa kocha kamili wa Schalke 04.

Di Matteo anakabiliwa na changamoto dhidi ya Sporting Lisbon kesho nyumbani Gelsenkirchen, kabla ya kukabiliana na mwajiri wake wa zamani Chelsea hapo Novemba 25.

Fußballer Cristiano Ronaldo
Nyota wa Madrid Cristiano Ronaldo anaendelea kuzitembelea nyavu za wapinzani kama anavyotakaPicha: picture-alliance/dpa/J. Martin

Chelsea inakwaana na Maribor kesho uwanjani Stanford Bridge na inapaswa kuwa macho na kujihadhari isije kukutwa katika usingizi, licha ya kuwa inaoongoza katika Premier League.

Barcelona inahitaji kuepuka kuvutwa fikira zao kuelekea katika mchezo wa watani wa jadi nchini Uhispania , El Clasico , dhidi ya Real Madrid Jumamosi ijayo wakati watakapokutana na Ajax Amsterdam katika pambano la Champions League kesho.

Macho yote nchini Uhispania yako katika mpambano wa vigogo vya soka la nchi hiyo Barca ikipambana na Real Madrid , mashabiki wakitaraji kurejea dimbani kwa mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez baada ya marufuku ya kucheza kwa muda wa miezi minne kwa kumng'ata mlinzi wa Italia Giorgio Chiellini katika mchezo wa kombe la dunia.

Lakini Real Madrid pia ina miadi na Liverpool wakati vigogo hivyo vya soka barani Ulaya vikifufua uhasama wao siku ya Jumatano watakapokutana uwanjani Anfield wakati Liverpool ikijaribu kuweka rekodi yao ya asilimia 100 dhidi ya Real Madrid.

Kazi katika uwanja wa Luzhniki ambao utafanyika fainali ya kombe la dunia mwaka 2018 inaendelea vizuri kama ilivyopangwa, amesema mkaguzi mkuu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Chris Unger. Hii ni tofauti kabisa ikilinganishwa na uchelewesho ulioikumba Brazil katika ujenzi wa viwanja kwa ajili ya fainali za kombe la dunia mwaka huu.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Josephat Charo