1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu ngeni yateka uongozi katika Bundesliga

22 Septemba 2014

Vigogo vya soka katika bundesliga vinahangaika msimu huu kupata pointi, wakati timu zilizopanda daraja zikipata mafanikio.Viongozi wa Bundesliga Paderbonn inaikabili Bayern Munich katika duru ya tano Jumanne(23.09.2014)

https://p.dw.com/p/1DH2N
Fußball Bundesliga 4. Spieltag SC Paderborn - Hannover 96
Wachezaji wa FC Paderborn inayoongoza ligi ya Ujerumani BundesligaPicha: Getty Images/Christof Koepsel

Mpangilio katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga unaonekana chini juu wakati timu iliyopanda daraja msimu huu Paderborn ikiongoza kundi la timu 18 katika ligi hiyo, ikifuatiwa na Manz 05 na Hoffenheim wakati timu vigogo katika ligi hiyo zikisuasua mwanzoni mwa msimu huu baada ya michezo minne.

Kwa mashabiki nchini Ujerumani, ambao wamekuwa wakitarajia Bayern Munich kutikisa kila timu katika njia yake kuelekea ubingwa tena kama ilivyofanya msimu uliopita, hali ya sasa ni mshangao wenye kufurahisha.

Fußball Bundesliga 4. Spieltag SC Paderborn - Hannover 96 Moritz Stoppelkamp
Mchezaji Moritz Stoppelkamp wa PaderbornPicha: picture-alliance/dpa/Oliver Krato

Paderborn ambao ni wageni katika ligi hii, wakiwa na bajeti ya euro milioni 5 tu, ndogo hata kwa baadhi ya timu za daraja la pili , imechupa na kuteka nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi kwa kujikusanyia points 8 ikiwa imeshinda michezo miwili na kutoka sare miwili.

Hata hivyo kila moja ya pointi hizo ilizojikusanyia ni muhimu iwapo itafika wakati ambapo italazimika kupambana kujizuwia kushuka daraja.

Baderborn yapeta

Kocha wa Paderborn Andre Breitenreiter amesema amefarijika sana na hali ya timu yake.

Tumefurahi sana, kwamba tumeweza leo kushinda , na tumeweza kupata pointi tatu zaidi , pointi tatu zaidi, ili kuweza kubakia katika daraja la kwanza. Hii ndio tunataka. Hata kama tunakwenda vizuri hivi sasa, na kwamba tuko juu na mashabiki wanafurahia.

Fußball Bundesliga 4. Spieltag 1. FSV Mainz - Borussia Dortmund Adrian Ramos
Mchezaji wa Borussia Dortmund Adrian Ramos akionyesha fadhaa yake baada ya kipigo dhidi ya Mainz 05Picha: picture-alliance/dpa/F, von Erichsen

Mwishowe huenda tusiweze kuendeleza hali hii. Tutaendelea kujituma na kujaribu, kufanya vizuri na kukusanya pointi nyingi zaidi iwezekanavyo.

Paderborn inatambua wazi kwamba mafanikio inayoyapata hivi sasa huenda yakawa ni kwa muda ambapo mabingwa watetezi Bayern Munich wanawasubiri nyumbani Allianz Arena kesho Jumanne.

Hata hivyo kocha wa Paderborn Andre Breitenreiter amesema anataka kikosi chake kufanya vizuri nyumbani kwa Bayern ambapo ligi hiyo inaingia katika duru yake ya tano kesho Jumanne na Jumatano.

Bayern ambayo nayo ina points 8 lakini inashika nafasi ya nne kutokana na tofauti ya magoli, imekuwa ikigharamika kutokana na kikosi kilichosheheni nyota kadhaa ambao zaidi ya nusu bado hawajakuwa katika kiwango cha juu baada ya michuano ya kombe la dunia , wakati wengine wako nje ya uwanja kwa kuwa ni majeruhi.

Bayern Munich haijaweza kurudia kile ilichokifanya msimu uliopita ambapo walinyakua ubingwa wa ligi muda mrefu kabla ligi hiyo kumalizika.

Fußball Bundesliga - Borussia Dortmund - FC Schalke
Julian Draxler wa Schalke 04Picha: Getty Images

Sare ya bila kufungana na Hamburg SV imethibitisha kwamba timu hiyo bado inahaingaika kufikia kiwango ilichokuwa nacho msimu uliopita huku kocha Pep Guardiola akisema kikosi hicho kitachukua muda mrefu kurejea katika hali yake ya kawaida.

Borussia Dortmund yadorora

Dortmund , ikiwa na points sita iko katika nafasi ya 10 , imepoteza michezo miwili na bundi bado yuko juu ya paa lake kwa kuandwamwa na lundo la wachezaji majeruhi , kama mchezaji wa kati Marco Reus , Nuri Sahin , Jakub Kuba Blaszczykowski na ILkay Gundorgan. Na wiki hii orodha hiyo imeongezeka na kumjumuisha Henrikh Mkhtaryan pia.

Mlinzi wa Borussia Dortmund Matthias Ginter alijifunga mwenyewe wakati Borusia ilipolazwa siku ya Jumamosi kwa mabao 2-0 nyumbani kwa Mainz 05 na anasema kikosi hicho kilikuwa na nafasi za kupata mabao lakini kwa bahati mbaya haikuweza kuziona nyavu.

"Tulipata nafasi hapa na pale , lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kupata bao. Mainz lakini ilipata mabao yake katika wakati muafaka . Tulipata penalti ambayo tulishindwa kufunga, halafu mpira uligonga nguzo, bahati mbaya leo kila kitu hakikuwezekana."

Kwa Schalke 04 , ambayo pamoja na Bayern , Dortmund na Bayer Leverkusen , inacheza katika Champions League, imeanza kwa kusuasua kabisa ikiwa haijashinda hadi sasa.

Schalke bado hoi

Schalke imeonekana kuwa katika hali nzuri wakati walipokuwa nyuma , lakini wakatoka suluhu ya mabao 2-2 dhidi ya Eintracht Frankfurt siku ya Jumamosi lakini wachezaji wake wa kati Kevin-Prince Boateng na Julian Draxler walitolewa nje kwa kadi nyekundu, na kupunguza uwezo wa kocha Jens Keller katika upangaji wa kikosi chake dhidi ya Werder Bremen siku ya Jumatano. Julian Draxler atakosa michezo miwili na atakosa mpambano wa watani wa jadi dhidi ya Borussia Dortmund siku ya Jumamosi.

Hannover 96 - FC Schalke 04
Eric-Maxim Choupo MotingPicha: picture-alliance/dpa

Mchezaji wa kati wa Schalke 04 Eric-Maxim Choupo-Moting amesema kutolewa kwa wachezaji hao kumeidhoofisha Schalke.

"Nafikiri , tungepata ushindi , iwapo tungebakia wachezaji kumi na moja uwanjani. Tuliweza kurejea katika mchezo huo , ambapo ni jambo muhimu. Upande ambao sio mzuri ni kwamba tumekuwa wajinga mno kuruhusu kufungwa mabao, ambayo hatukupaswa kufungwa. Iwapo umefungwa mabao , inakuwa vigumu sana kurejesha. Kwa bahati mbaya , ilitulazimu kucheza tukiwa pungufu. Hata hivyo tunayakubali matokeo na tunaweza kufurahi, kwasababu tumecheza tukiwa pungufu na hatukushindwa."

Ligi ya Ujerumani inaendelea kesho Jumanne na Jumatano ambapo Bayern Munich inaisubiri Paderborn, Hoffenheim inaikaribisha Freiburg, Werder Bremen iko nyumbani ikiisubiri Schalke 04 na Eintracht Frankfurt inamiadi na Mainz 05.

Jumatano Bayer Leverkusen inaikaribisha Augsburg, Borussia Dortmund iko nyumbani ikiisubiri VFB Stuttgart, Borussia Moenchengladbach ina miadi na Hamburg SV , FC Kolon inasafiri kuelekea Hannover na Hertha BSC Berlin itapimana nguvu na VFL Wolfsburg.

Real Madrid yatunisha misuli

Na katika ligi ya Uhispania La Liga Real Madrid inaendelea na mbio zake kuzifukuzia mabingwa Atletico Madrid na viongozi wa ligi hiyo kwa sasa FC Barcelona wakati watakapoikaribisha Elche katika Santiago Bernabeu kesho Jumanne. Kikosi cha kocha Carlo Ancelotti kimerejea kutoka vipigo mfululizo dhidi ya Real Sociedad na Atletico Madrid kwa kupachika mabao 13 katika michezo na Basel katika champions League na Depotivo la Coruna katika wiki iliyopita. Real Madrid iliisambaratisha Depotivo la Coruna kwa mabao 8-2 siku ya Jumamosi.

Kesho(23.09.2014) mbali ya pambano hilo kati ya Real Madrid na Elche, pia Celta Vifo itaumana na Depotivo la Coruna, na Malaga inakibarua dhidi ya Barcelona.

Cristiano Ronaldo UEFA Super Cup Madrid vs Sevilla
Wachezaji wa Real Madrid ya UhispaniaPicha: Getty Images

Huko Italia mambo ni tofauti, baada ya michezo mitatu, ligi ya Serie A inaonekana kufuata mkondo wa msimu uliopita, wakati Roma na mabingwa Juventus wakiwa juu ya msimamo wa ligi.

Roma itaingia uwanjani Jumatano kupambana na Parma , wakati Juventus inakwaana na Cesena.

Michezo mingine ni kati ya Inter Milan ikikwaana na Atalanta, Cagliari inakabana koo na Torino, Fiorentina inaisubiri Sassuolo na sampdoria ina miadi na Chievo Verona.

Qatar itapoteza nafasi ya kuwa mwenyeji wa kombe la dunia

Mjumbe wa kamati kuu ya shirikisho la kandanda duniani FIFA kutoka Ujerumani Theo Zwanziger anaamini kuwa Qatar itapoteza haki ya kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2022 kutokana na wasi wasi kuhusu hali ya hewa. Zwanziger ameliambia gazeti la michezo la Bild la Ujerumani leo, kuwa shirikisho hilo la kandanda haliwezi kujiingiza katika hatari ya kuhusika katika masuala ambayo yanahusiana na hali ya joto katika wakati michezo hiyo itakapofanyika katika majira ya joto.

Zwanziger amesema ni imani yake kuwa fainali za kombe la dunia mwaka 2022 hazitfanyika nchini Qatar.

Nigeria kuchagua viongozi

Huko katika bara la Afrika shirikisho la kandanda la Nigeria limesema litawachagua viongozi wake wapya hapo Septemba 30.

Uchaguzi utafanyika chini ya usimamizi wa rais anayeondoka madarakani wa Shirikisho la kandanda la Nigeria NFF Aminu Maigari, ambaye alilazimishwa mara mbili kuondoka madarakani katika miezi ya hivi karibuni na kurejeshwa na shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Nigeria ambayo ni bingwa wa bara la Afrika , ilipigwa marufuku kushiriki katika michezo ya kimataifa kwa siku tisa Julai mwaka huu kutokana na serikali kuingilia kati shughuli za michezo baada ya waziri wa michezo kuunga mkono kuondolewa madarakani kwa Maigari.

Albert Ebosse
Marehemu Albert Ebosse kutoka Cameroon aliyefariki dunia nchini AlgeriaPicha: -/AFP/Getty Images

Na klabu ya soka la JS Kabylie ya Algeria imezuiwa kucheza katika mashindano ya bara la Afrika kwa miaka miwili kutokana na kifo cha mchezaji kutoka Cameroon Albert Ebosse. Uamuzi huo umechukuliwa na shirikisho la kandanda barani Afrika CAF katika mkutano wake uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Kabylie imemaliza ikiwa ya pili katika ligi ya Algeria msimu uliopita na kuipa nafasi ya kushiriki katika Champions League msimu wa 2015.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman