1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania, Burundi zakubaliana juu ya mpaka

Prosper Kwigize29 Agosti 2014

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwenzake wa Burundi, Pierre Nkurunziza, wamekagua na kuidhinisha mpaka baina ya nchi zao kufuatia uhakiki uliofanywa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/1D3Hv
East African Community EAC Eriya Kategaya Ostafrikanische Gemeinschaft
Picha: AP

Katika shughuli hiyo ya pamoja iliyofanyika siku ya Jumatatu katika wilaya ya Ngara magharibi mwa Tanzania, marais hao walisema kuidhinisha mpaka sio kuwatenganisha wananchi wa nchi hizo, bali kuheshimu utaratibu wa kisheria.

Mkutano huo wa kwanza kufanyika katika eneo la mpakani, ulifanyika katika kijiji cha Mugikomero wilayani Ngara ambapo viongozi wengine wa nchi za Burundi na Tanzania pamoja na wananchi walihudhuria.

Akihutubia hafla hiyo, Rais Kikwete pamoja na kupongeza kuwepo kwa amani nchini Burundi alisifu pia mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Tanzania na Burundi.

Kikwete alitoa wito kwa wananchi pamoja na serikali za mitaa kuhakikisha mipaka yote ya nchi yanahifadhiwa na serikali itenge pesa kwa ajili ya kazi hiyo.

Kwa upande wake Rais wa Burundi Piere Nkurunziza licha ya kupongeza hatua hiyo ya uhakikii wa mipaka alikiri kuwa Tanzania na Burundi ni ndugu na kuishukuru Tanzania kwa kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi zaidi ya milioni moja kutoka Burundi.

Awali Waziri wa ardhi na maendeleo ya makazi wa Tanzania Bi. Anna Tibaijuka alisema kuwa tayari kazi kama hiyo imefanyika kwa maeneo ya mipaka iliyoko baharini.

Mwandishi: Prosper Kwigize
Mhariri: Mohammed Khelef