1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yagubika mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu

Admin.WagnerD25 Machi 2014

Mfalme Sabah al-Ahmed al- Sabah wa Kuwait ametoa wito kwa mataifa ya Kiarabu kuondoa tofauti zao kwa lengo la kuondosha hali ya mkwamo katika utekelezaji wa mipango ya pamoja ya matiafa hayo.

https://p.dw.com/p/1BVNf
Arabische Liga Gipfeltreffen 25.03.2014 Kuwait
Mkutano wa kilele wa mataifa yaliyo katika Jumuiya KiarabuPicha: Reuters

Kiongozi huyo aliyasema katika ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu unaofanyika Kuwait.

Akizungumza mbele ya viongozi wa mataifa ya kiarabu, Sheikh Sabah alisema hatari inayowazunguka katika mataifa hayo ni kubwa na kwamba hawawezi kusonga mbele pasipo kuwepo na umoja baina yao na kuondosha kabisa tofauti zao.

Kiongozi huyo hakutaja nchi kwa jina lakini alikuwa akitolea mifano machafuko katika baadhi ya mataifa ya Kiislamu na nafasi ya itikadi kali katika kanda hiyo na kile ambacho mataifa mengi ya Ghuba yanakiona kama ni Iran kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.

Kauli ya Nabil al Arab

Baadae katika taarifa yake kwa viongozi, katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Nabil al Arab amesema kuna umuhimu kwa mataifa ya kiarabu kumaliza kabisa tatizo la kubwa la Ugaidi katika mipaka ya mataifa hayo. Amezungumza madhira wanayokabiliana watu wa Syria na kuitaka jumuiya ya kimataifa kutupia jicho la huruma katika kutafuta namna ya kuwakwamua watu hao.

Arabische Liga Gipfeltreffen 25.03.2014 Kuwait
Wajumbe wa mkutano wa kilele wa mataifa ya Jumuiya ya KiarabuPicha: Reuters

Kiongozi wa muungano wa kitaifa wa upinzani nchini Syria Ahmad Jarba ametaka viongozi hao wawaunge mkono watu wa Syria katika kukabiliana na kile alichokiita udhalimu wa rais Bashar al-Assad na kuongeza kusema kitendo cha jumuiya hiyo kutoa kiti cha utawala wake kuhudhuria mkutano huo ni sawa na kutoa fursa ya kuendelea kwa vitendo vya kinyama vinavyofanyika nchini humo.

Wito kwa jumuiya ya Kimataifa

Katika mkutano huu pia Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kirabu katika mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi alizungumza mbele ya viongozi hao wa mataifa 22 akijikita hasa katika kutafuta suluhu ya kisaisa ya mgogo wa Syria baada ya kukwama kwa awamu mbili ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Syria na uasi mjini Geneva.

Mpatanishi hiyo aliyesitisha mazungumzo ya amani yaliopewa jina jina la Geneva mbili Februari 15 alisema mazungumzo mengine ya upatanishi baina ya pande hizo mbili yanasubiri muda muafaka tu. Amesema hivi sasa hali ya kisiasa katika Mashariki ya Kati imekuwa ngumu kuliko ilivyokuwa siku za nyuma akizinganzia hasa mgogoro wa Syria na watu wanavyopoteza maisha kila siku na ongezeko la idadi ya wakimbizi.

Mgogoro huo wa Syria ambao katikati ya Machi ulitimiza miaka mitatu, umesababisha vifo vya watu 140,000 na wengine mamilioni kuachwa bila ya makazi.

Katika mkutano wa maandalizi ya mkutano huu mkubwa, mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa hayo ya Jumuiya ya Kiarabu jumapili iliyopita walilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio namba 7 ambalo pamoja na mambo mengine linaamuru kusitishwa mapigano. Hata hivyo mgawanyiko miongoni mwa mataifa hayo ya kiarabu umeathiri viwango vya uwakilishi katika mkutano nchini Kuwait.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman