1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Suluhisho la Kiafrika kwa matatizo ya Afrika" lawezekana?

24 Mei 2013

Umoja wa Afrika leo unaadhimisha miaka 50 ya kuanzishwa kwake ukihimiza kauli mbiu yake ya "Suluhisho la Afrika kwa matatizo ya Afrika", lakini ni wazi kuwa Umoja huo unakabiliwa na changamoto kadhaa kutimiza azma hiyo.

https://p.dw.com/p/18dVr
An African Union cease-fire monitor patrols among displaced Sudanese in the Abu Shouk camp near al Fasher in north Darfur province Wednesday Nov. 3, 2004. About 3,000 AU soldiers are being deployed in the Darfur region in an attempt to end the humanitarian crisis. (AP Photo/Jose Cendon)
Bildergalerie 50-jähriges Jubiläum der Afrikanischen Union AUPicha: picture-alliance/AP

Umoja wa Afrika umechukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU, ulioundwa tarehe 25 Mei 1963, kwa dhamira ya kuhakikisha kuwa bara la Afrika linatoka kwenye mikono ya wakoloni na kuhimiza maendeleo na umoja kati ya nchi wanachama wa Umoja huo.

Sera kuu ya sasa ya Umoja wa Afrika kuelekea mataifa wanachama ni kuingilia mambo yanayohusu nchi hizo. Sera hii ilianza kupata msukumo baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka1994, pale jamii ya kimataifa ilipoukosoa Umoja huo kwa kushindwa kuingilia haraka na kuzuia mauaji hayo.

Kufatia hali hiyo, mwaka 2002 Umoja huo ulitunga sera za kutafuta suluhisho la ndani la matatizo ya nchi wanachama na kujipa mamlaka ya kuingilia matatizo ya kivita, mauaji ya kimbari na uovu dhidi haki za binadamu katika nchi hizo.

Kamisheni ya Ulinzi na Amani ya Umoja inayoshughulikia matatizo ya nchi wanachama wa umoja huo, kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya fedha, na kukosa usimamizi kamili kwa vikosi vya wanajeshi kutoka mataifa ya kigeni wanaotumwa na Umoja wa Mataifa katika nchi za Afrika kusaidia Umoja wa Afrika kumaliza mapigano.

Uwezo mdogo wa Umoja wa Afrika

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema uwezo mdogo wa Umoja wa Afrika katika kusimamia majeshi yanayotoka katika nchi za Magharibi kinapunguza uwezo wake wa kutatua mizozo na mapigano ya kisiasa katika nchi wanachama.

Wanajeshi wa Burundi katika AMISOM wakilinda mitaa ya Mogadishu, Somalia.
Wanajeshi wa Burundi katika AMISOM wakiwazika wenzao.Picha: ALEXANDER JOE/AFP/Getty Images

Hivi karibuni Umoja wa Afrika ulikosolewa kwa kutoitikia haraka tatizo la kisiasa la nchini Mali, wakati waasi wa nchi hiyo walipopindua serikali mwezi Machi mwaka jana, hadi baadaye Januari mwaka huu, mkoloni wa zamani, Ufaransa, alipoamua kuingiza majeshi yake katika nchi hiyo ya magharibi ya Afrika.

"Ilikuwa wapi Kamisheni ya Ulinzi na Amani ya Umoja wa Afrika hadi majeshi ya Ufaransa kuingia nchini Mali?" Anauliza Liesl Louw-Vaudran, wa Taasisi ya Masomo ya Ulinzi ya Afrika ya Kusini, ISS.

Anasema kutokuwa na msimamo kwa viongozi AU kumedhihirika katika ghasia za Libya mwaka 2011, kwani kuna viongozi waliokuwa wanataka kuwatambua waasi waliokuwa wanapigana dhidi ya Gaddafi na wale waliokuwa wanamuunga mkono kiongozi huyo, ambaye mwenyewe ndiye muasisi na mfadhili mkubwa wa wazo la Umoja wa sasa Afrika.

Mafanikio licha ya changamoto

Kwa upande wake, Waziri Mambo ya Nje wa Ethiopia, ambaye ni mwenyekiti wa AU kwa sasa, Teodros Gebreyesus, amesema pamoja na changamoto hizo, Afrika imepiga hatua ya maendeleo katika miongo kadhaa iliyopita kutokana na kuhimza amani na utulivu katika bara hilo.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema mafanikio hayo makubwa yamefikiwa pale Umoja wa Afrika ulipoingiza wanajeshi wake 17,700 nchini Somalia kutoka katika mataifa matano ya Afrika ili kupambana na waasi wa al-Shabaab ambao wana mafungamano na kundi la al-Qaida.

Mmoja wa maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hadi sasa inakadiriwa askari 3,000 walinda amani wa Umoja wa Afrika wameshauawa toka mwaka 2007, ikiwa ni sawa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliouawa tangu mwaka 1948

Licha ya kuwa misaada mingi ya kuyahudumia majeshi ya kulinda amani inatoka katika nchi za Magharibi, lakini vikosi vya Umoja wa Afrika vimeonesha mchango mkubwa katika kulinda amani nchini Somalia.

Mafanikio mengine ya Umoja wa Afrika ni katika mapambano yake dhidi ya uasi wa kundi la Lord's Resistance Army, LRA, la Joseph Kony wa Uganda, ndani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwandishi: Hashim Gulana/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef