1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ziarani Asia

Elizabeth Shoo31 Oktoba 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, analitembelea bara la Asia. Huko amekutana na viongozi wa Korea Kusini kujadili uwezekano wa nchi hiyo kuungana tena na Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/1Detj
Frank-Walter Steinmeier na Yun Byung-se Seoul
Picha: picture-alliance/AP Photo/Ahn Young-joon

Steinmeier aliianza ziara hiyo ya siku mbili kwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini, Yun Byung-se. Viongozi hao watazungumzia hasa namna ya kuufanikisha mpango wa kuziunganisha tena Korea mbili.

Waziri Yun Byung-se alisema kuwa serikali yake inachukua mfano kwa Ujerumani, nchi ambayo ilikuwa imegawanyika lakini sasa imeungana na kuwa taifa moja. "Tumekubaliana kuendelea kuliunga mkono jopo linaloishauri serikali ili liweze kutunga mapendekezo yatakayouwezesha muungano wa Korea," alisema Yun. "Tutaichukua Ujerumani kama mfano wa namna ya kuendesha sera za mambo ya nje kwa ajili ya kuungana."

Mazungumzo ya nyuklia kuanza tena

Steinmeier na mwenzake wa Korea Kusini watakutana pia na jopo maalumu la kuuwezesha muungano. Jopo hilo liliundwa Septemba mwaka huu na linawajumuisha watu 14. Kazi yao itakuwa kutambua mambo ambayo Korea Kusini inaweza kuiga kutoka kwa muungano wa Ujerumani.

Korea Kaskazini na Kusini zinatenganishwa na mpaka wenye ulinzi mkali
Korea Kaskazini na Kusini zinatenganishwa na mpaka wenye ulinzi mkaliPicha: picture-alliance/AP

Mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini ni mada nyingine iliyojadiliwa. Steinmeier alikumbusha kwamba safari bado ni ndefu. "Kuna changamoto kadhaa katika mchakato huu wa kuleta muungano wa Korea. Utawala wa Korea Kaskazini na hata jamii haina uwazi na Korea Kaskazini haiko tayari kusitisha silaha zake za nyuklia." Aliogezea kwamba Korea Kaskazini haitaweza kupata maendeleo ya kiuchumi au kujenga urafiki na nchi nyingine wakati ikiwa na silaha za nyuklia.

Steinmeier amekiri kwamba kwa sasa hakuna dalili za kuonyesha kuwa Korea Kaskazini inaweka juhudi za kuleta muungano. Aidha, alisistiza kwamba Ujerumani ikiwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, inaunga mkono wazo la kuanzisha tena mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani, China, Japan, Urusi na Korea mbili. Mazungumzo hayo yamekwama tangu mwaka 2008, licha ya kwamba serikali ya Korea Kaskazini mwaka 2005 ililisaini makubaliano ya kusitisha mipango yake ya nyuklia ikiwa itapatiwa misaada ya kifedha kutoka jumuiya ya kimataifa.

Steinmeier atalitembelea pia eneo la mpaka kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini. Baada ya hapo, ataendelea na ziara yake nchini Indonesia.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/reuters

Mhariri: Josephat Charo