1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier atangaza sera nje ya Ujerumani

Mohammed Khelef26 Februari 2015

Ugaidi wa Dola la Kiislamu, Ebola na mzozo wa Ukraine ni miononi mwa mambo ambayo yanaonekana kutokuwa na mwisho na ambayo sasa siasa ya nje ya Ujerumani inajaribu kuyatafutia majibu.

https://p.dw.com/p/1Ei30
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akijadili kile kiitwacho "Mapitio ya 2014 - Kufikiria zaidi siasa za nje" jijini Berlin.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, akijadili kile kiitwacho "Mapitio ya 2014 - Kufikiria zaidi siasa za nje" jijini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/G. Charisius

Ujerumani imetangaza kufanya marekebisho makubwa kwenye sera yake ya nje ili kuakisi matakwa ya dunia inayobadilika kwa kasi na hivyo kugundua nafasi mpya kwenye siasa za kilimwengu.

"Dunia inabadilika na hivyo lazima Wizara ya Mambo ya Nje nayo ibadilike," anasema Steinmeier, ambaye ndiyo kwanza amerejea kutoka ziara yake ya mashariki mwa Afrika alikotangaza kwamba sasa Ujerumani inapaswa kubadili muelekeo wake kuhusu bara hilo, akitoa wito wa uwekezaji mkubwa na kile alichokiita "kufunguka milango" ya Afrika.

Katika hafla ya kutimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (DGAP) mjini Berlin hapo jana, Waziri Steinmeier aliwaambia waalikwa kwamba siasa ya nje ya Ujerumani lazima irekebishwe na ijengewe nyenzo za kukabiliana na mizozo ya sasa ya kilimwengu.

Katika kuyapa sura mageuzi hayo anayoyasimamia, tayari Waziri Steinmeier ametangaza kuifumua wizara yake kwa kuzipanga upya idara zilizopo pamoja na kuanzisha nyengine mpya, huku akiwatolea wito maafisa wa wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii kubwa zaidi wakati huo, kuliko ilivyowahi kutokea wakati wowote kwenye historia ya wizara hiyo.

Mwanzo mpya kuelekea ulimwengu mpya

"Tunapaswa kufikiria ikiwa kila jambo tunalofanya liko sawa", alisema Steinmeier kuwaambia wafanyakazi wa wizara yake, huku mwenyewe akitajwa na wanaomjua kuwa ni kigezo chema kwa ufanyaji kazi usio kikomo. Mwanasiasa huyo wa SPD alichukuwa nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje kutoka kwa Guido Westerwelle wa FDP tarehe 17 Disemba 2013.

Mageuzi ya kwanza ya kimsingi kwa Steinmeier yalikuwa ni kuiondosha Wizara ya Mambo ya Nje kutoka taswira ya kijiwizara kidogo kinachotetea sera za ndani za Ujerumani nje ya mipaka yake, na kuwa ofisi kamili yenye wasta na wasifu wake yenyewe.

Waziri Steinmeier (kushoto) akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika ziara yake ya hivi karibuni mashariki mwa Afrika.
Waziri Steinmeier (kushoto) akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika ziara yake ya hivi karibuni mashariki mwa Afrika.Picha: picture-alliance/dpa/Michael Kappeler

Kutoka kile kilichopewa jina la "mapitio ya 2014 - kufikiria zaidi siasa za nje", tangu mwaka jana kumekuwa sasa na kile kiitwacho "ugunduzi wa siasa za nje", utaratibu wa kila mwezi ambao Steinmeier ameuanzisha wa kuwa na vikao vya wizara juu ya mwenendo wa siasa za Ujerumani kuelekea mataifa na taasisi za nje.

Chini ya mpango huo, kunakuwa na mijadala na wataalamu wa siasa za nje na ndani na wafanyakazi wa wizara ya mambo ya nje, lengo likiwa ni kujenga uwazi mkubwa kwenye siasa za nje. Zaidi ya asasi kubwa 60 kwenye miji yote mikubwa ya Ujerumani, zinashiriki mijadala ya wazi na ya mtandaoni juu sera ya nje, ambapo katika baadhi ya matukio, mwenyewe Steinmeier huongoza semina za mafunzo.

Ndani yake, ndimo munamojengwa muelekeo mpya wa Ujerumani kuelekea masuala kama yale ya Ukraine, Umoja wa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika, kaulimbiu ikiwa "dunia inabadilika, hivyo siasa ya nje ya Ujerumani nayo inapaswa kubadilika."

Mwandishi: Bettina Marx
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba