1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio lainyemelea Syria

2 Septemba 2013

Rais Barack Obama wa Marekani Jumatatu (02.09.2013)anatazamiwa kuimarisha kampeni yake kuwashawishi wabunge wenye mashaka kuunga mkono hatua ya kijeshi dhidi ya Syria wakati nchi ikitaka kuzuiliwa kwa shambuolio hilo.

https://p.dw.com/p/19a5X
Jumuiya ya Waarabu ikiwa Cairo Septemba Mosi 2013.
Jumuiya ya Waarabu ikiwa Cairo Septemba Mosi 2013.Picha: Reuters

Mkakati uliofafanuliwa na afisa wa Ikulu ya Marekani umekuja baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani kusema kwamba serikali ya nchi hiyo ina ushahidi kwamba serikali ya Syria imetumia gesi ya sumu ya sarin katika shambulio lililosababisha maafa hapo tarehe 11 mwezi wa Augusti.

Lakini Urusi imesema haiamini kabisa ushahidi uliowasilishwa na Marekani na washirika wake kuhusu shambulio hilo la sumu ambalo mataifa ya magharibi yanadai kwa limefanywa na serikali ya nchi hiyo.Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kile walichooneshwa hivi karibuni na washirika wao wa Marekani,Uingereza na Ufaransa hawakisadiki kabisa na kuongeza kwamba kuna mashaka mengi ya taswira za shambulio hilo zilizowekwa kwenye mtandao.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Kiarabu wameutaka Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kimataifa kuchukuwa hatua ya kuizuwiya nchi hiyo kuwadhuru wananchi wake na imeilamumu serikali ya nchi hiyo kwa shambulio hilo la silaha za sumu.Taarifa yao imetaka wahusika wa shambulio hilo wafunguliwe mashtaka katika Mhakama ya Uhalifu kama ilivyo kwa wahalifu wengine wote wa kivita.

Macho yaelekezwa Washington

Wakati zingatio lote likielekezwa Washington, Obama halikadhalika makamo wake wa rais John Biden na Katibu Kiongozi wa Ikulu ya Marekani Denis McDonough wametowa wito wa kibinafsi kwa wabunge hapo jana na wito zaidi unatazamiwa kutolewa leo hii kuwataka waunge mkono hatua ya Marekani kuishambuli kijeshi Syria.

Seneta John McCain.
Seneta John McCain.Picha: imago/UPI Photo

Kufuatia tangazo la kushangaza la Obama Ikulu ya Marekani imeliomba rasmi bunge hapo Jumamosi kibali cha kufanya mashambulizi katika rasimu yenye kuelezea operesheni hizo za kiwango kidogo.Lakini inasubiriwa kuona iwapo wabunge wenye mashaka watapitisha shinikizo la Obama la kufanya mashambulio hayo au kumkatalia na hiyo kumpa idhara kubwa.Wabunge wengi wakiwemo seneta mwenye ushawishi wa chama cha Republikan John McCain bado hawana uhakika iwapo wataunga mkono uamuzi huo wa Ikulu ya Marekani.

Hata hivyo mshirika muhimu wa Marekani imedokeza kwamba mashambulizi kidogo sio njia muafaka ya kuiadhibu Syria. Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye anapendelea kuchukuliwa kwa hatua kubwa ya kijeshi ya kimataifa nchini Syria amesisitiza kwamba mashambulizi yenye kikomo yatazidi kuifanya hali kuwa mbaya.

Ameuambia mkutano mjini Istanbul kwamba mashambulizi yatakayolenga maeneo mahsusi sio tu yatashindwa kuwaelekeza kwenye suluhisho lakini yatafanya hali kuzidi kuwa ngumu nchini Syria. Ametowa wito Assad kun'gatuka haraka na kukimbilia kwenye nchi itakayokuwa tayari kumpokea.Uturuki inashirikiana mpaka na Syria.

Umoja wa Mataifa watakiwa kuwajibika

Kwa upande mwengine Syria imeutaka Umoja wa Mataifa kuzuwiya uchokozi wowote ule dhidi ya nchi hiyo kufuatia wito wa Obama wa kutaka jeshi la Syria liadhibiwe kutokana na kushambulia raia kwa silaha za sumu mwezi uliopita ambapo zaidi ya watu 1,400 waliuwawa wakiwemo watoto.

Mkaguzi wa silaha za sumu wa Umoja Mataifa katika vitongoji vya Damascus.
Mkaguzi wa silaha za sumu wa Umoja Mataifa katika vitongoji vya Damascus.Picha: Reuters/Mohammad Abdullah

Katika baruwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Maria Cristina Percecal ,balozi wa Syria kwa Umoja wa Mataifa Bashar Ja'aafari amemtaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwajibika kwa kuzuwiya uchokozi wowote kwa Syria na kushinkiza ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo wa Syria.

Syria imekanusha matumizi yoyote yale ya silaha za sumu na imewalaumu waasi wanaopambana kumpinduwa Rais Bashar al Assad kwa kuhusika na mashambulizi ya silaha hizo.

Mwandishi: Mohammed Dahman

Mhariri: Josephat Charo