1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Ujerumani yaridhia kubakisha wanajeshi Afghanistan

Saumu Ramadhani Yusuf19 Novemba 2014

Baraza la mawaziri la Ujerumani limeidhinisha mipango ya kupeleka wanajeshi hadi 850 nchini Afghanistan watakaoshirikiana na kikosi cha NATO kutowa mafunzo na ushauri kuanzia Januari mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/1DpqR
Baraza la Mawaziri la Ujerumani
Baraza la Mawaziri la UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Ujerumani ni nchi iliyopeleka wanajeshi wengi nchini Afghanistan katika eneo ambalo lina utulivu kiasi kaskazini mwa taifa hilo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita na itaendelea kubeba dhamana ya jimbo hilo katika ujumbe huu mpya utakaoanza Januari ya mwaka 2015. Kikosi hicho maalum kitabakia nchini Afghanistan kwa kipindi cha mwaka mmoja kama ilivyoidhinishwa hii leo na serikali ya Kansela Angela Merkel.

Hata hivyo hatua ya baraza la mawaziri la kansela Merkel inabidi kwanza iidhinishwe na bunge la Ujerumani ambako muungano wa Merkel unawingi mkubwa.Kufikia hivi sasa Ujerumani ina wanajeshi 1520 nchini Afghanistan kama sehemu ya ujumbe wa kiusalama ambao utamaliza majukumu yake mwezi ujao wa Desemba kama ilivyo kwa kikosi cha Jumuiya ya kujihami ya NATO kitakachoondoka tarehe 31 ya Desemba.

Wanajeshi wa Ujerumani watakaopelekwa nchini Afghanistan katika mpango huu mpya watahitajika kubeba jukumu la kutoa mafunzo,ushauri na msaada na asilani hawatoruhisiwa kuingia kwenye uwanja wa mapambano amesisitiza msemaji wa serikali kuu mjini Berlin Steffen Seibert.

Aidha kikosi jumla cha Kimataifa kitakachobakia Afghanistan mwaka 2015 kitakuwa na wanajeshi kiasi 12,000.Marekani ambayo imekuwa ikiongoza kikosi cha NATO nchini Afghanistan kitapeleka wanajeshi 9800 sambamba na wanajeshi maalum katika ujumbe huo utakaohusika na ujenzi mpya wa Afghanistan baada ya kuondoka kikosi cha Nato mwishoni mwa mwaka huu.Ujerumani itakuwa katika nafasi ya pili kwa kutowa wanajeshi nchini humo.

Wanajeshi wa Ujerumani kusinimagharibi mwa Afghanistan,wakikabidhi ulinzi kwa waafghanistan
Wanajeshi wa Ujerumani kusinimagharibi mwa Afghanistan,wakikabidhi ulinzi kwa waafghanistanPicha: picture-alliance/dpa/MOD/Sergeant Obi Igbo

Kikosi cha kimataifa cha kutoa msaada ISAF ambacho kinaongozwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kiliingia Afghanistan mwaka 2001 baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani ya Septemba 11 mjini NewYork.

Kadhalika baraza hilo la mawaziri limeidhinisha ripoti ya awali ya mjumbe maalum wa serikali kuu juu ya Afghanistan Michael Koch ambapo kwa mujibu wa Steffen Seibert ripoti hiyo imeonyesha wazi kwamba mafanikio makubwa yamepatikana nchini Afghanistan ingawa bado kuna mengi hayajafikiwa.Kwa mujibu wa ripoti ya mjumbe maalum wa Ujerumani kuhusu Afghanistan imetajwa kwamba alau kuna hali ya demokrasia inayoshuhudia Afghanistan ingawa anakiri pia kwamba katika mzozo wa miezi kadhaa wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi wa rais nchini humo ilionesha wazi kwamba umma ulikosa imani na uchaguzi huo.Halikadhalika ripoti hiyo imetilia mkazo juu ya mapungufu yaliyopo kwenye suala la maendeleo ya kiuchumi wakati pia suala la usalama likitajwa kubakia tete.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:AbdulRahman Mohammed.