1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya ya Burkina Faso yaanza kazi

24 Novemba 2014

Serikali mpya ya mpito ya Burkina Faso itaandaa mkutano wake wa kwanza leo, huku jeshi likisalia na nyadhifa kuu ikiwa ni wiki tatu baada ya jeshi kuchukua madaraka kufuatia maandamano makubwa ya umma

https://p.dw.com/p/1Ds34
Burkina Faso ÜbergangsPräsident Michel Kafando
Rais wa mpito wa Burkina Faso Michel KafandoPicha: picture-alliance/dpa

Katika serikali mpya iliyotangazwa jana jioni na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Alain Thierry Ouattara, Kiongozi wa jeshi Luteni Kanali Isaac Zida atasalia kuwa waziri mkuu na pia kuchukua wadhifa wa waziri wa ulinzi. Jeshi pia litakuwa na udhibiti wa wizara ya ndani.

Kwa jumla, maafisa wanne wa jeshi wamejumuishwa kwenye baraza hilo lenye mawaziri 26. Rais wa kiraia wa mpito Michel Kafando pia ataongoza wizara ya mambo ya nchi za kigeni.

Kafando, mwanadiplomasia wa zamani, aliapishwa Ijumaa iliyopita ili kuliongoza taifa hilo la Afrika katika kipindi cha mpito cha mwaka mmoja baada ya kiongozi wa muda mrefu Blaise Compaore kuangushwa kufuatia wimbi la maandamano ya umma mwezi uliopita. Jeshi limeahidi kusaidia kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia.

Muundo wa serikali mpya awali ulitarajiwa kuzinduliwa Alhamisi iliyopita, na kisha Jumamosi, lakini uliahirishwa kila mara kwa sababu za tofauti baina ya makundi pinzani. Duru zilisema kucheleweshwa huko kulisababishwa na upinzani wa jeshi dhidi ya wagombea wa wizara kadhaa waliopendekezwa na makundi ya kiraia.

Burkina Faso Isaac Zida in Ouagadougou
Luteni Kanali Isaac Zida ndiye waziri mkuu wa mpitoPicha: STR/AFP/Getty Images

Licha ya kuchukua mkondo wa kiraia, na Kafando kuwa rais, udhibiti wa jeshi wa nyadhifa za usalama una maana kuwa wanajeshi wanasalia kuwa nguvu kubwa ya kisiasa nchini humo.

Baadhi ya wawakilishi wa makundi ya kiraia yameelezea wasiwasi kuhusiana na uteuzi wa Zida, na baadhi ya wakaazi wa Ouagadougou wameiita hatua hiyo kuwa usaliti wa “mapinduzi” yao.

Hakuna viongozi wa upinzani walioteuliwa katika baraza jipya la mawaziri. Hii ni kutokana na uamuzi wao, kwa sababu hakuna yeyote katika serikali hii atakayeruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka ujao. Kafando na Zida wote wanazuiwa kugombea katika uchaguzi huo unaopangwa kuandaliwa Novemba mwaka ujao, chini ya mpango wa kipindi cha mpito.

Kafando ameapa kuwaadhibu waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za serikali wakati wa utawala wa Compaore wa miaka 27, ambaye alikuwa mshirika wa karibu na aliyekuwa rais wa ki imla wa Libya, marehemu Muamar Gaddafi na mbabe wa kivita wa Liberia aliyegeuka na kuwa rais Charles Taylor, ambaye kwa sasa yuko kizuizini kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita.

Compaore, yuko ziarani Morocco baada ya kusafiri Ijumaa iliyopita akitokea Cote d'ivoire, ambako alikimbilia baada ya utawala wake wa muda mrefu kukamilika Oktoba 31 kutokana na maandamano ya umma. Burkina Faso huuza pamba na dhahabu katika mataifa ya nje, lakini karibu nusu ya idadi ya watu inaishi chini ya dola moja kwa siku na wengi ni wakulima wadogowadogo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo