1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sepp Blatter ashinda tena kuiongoza FIFA

30 Mei 2015

Licha ya shinikizo na kashfa za rushwa ndani ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni, FIFA, rais wake kwa miaka 17 Sepp Blatter amechaguliwa tena kuliongoza shirikisho hilo kwa muhula wa tano mfululizo.

https://p.dw.com/p/1FZIP
Sepp Blatter akisherehekea ushindi wake
Sepp Blatter akisherehekea ushindi wakePicha: P. Schmidli/Getty Images

Sepp Blatter mwenye umri wa miaka 79 alitangazwa mshindi katika uchaguzi wenye mvutano mkubwa uliofanyika jana usiku mjini Zurich, Uswisi, baada ya mpinzani wake wa pekee, mwanamfalme Ali bin al-Hussein wa Jordan kujiondoa katika duru ya pili ya uchaguzi huo, baada ya duru ya kwanza kutombainisha mshindi wa moja kwa moja.

Matokeo ya duru ya kwanza yalimuonyesha rais aliyekuwepo Sepp Blatter akiongoza kwa kura 133 dhidi ya 73 alizozipata mwanamfalme Ali bin al-Hussein wa Jordan. Kwa matokeo hayo Blatter hakupata theluthi mbili ya kura ili kupita moja kwa moja, na ilitangazwa duru ya pili ambapo anayemzidi mwenzake wingi wa kura anatangazwa mshindi. Ali bin al-Hussein aliamua kujiondoa kabla ya duru hiyo ya pili, na hivyo kumuachia ushindi Blatter, na dhamana ya kuiongoza FIFA kwa muhula wa tano mfululizo.

Al-Hussein aepusha duru ya pili

Al-Hussein ambaye aliungwa mkono hasa na na nchi za Ulaya, aliwashukuru wote waliomuunga mkono.

Mwanamfalme Ali bin al-Hussein alikubali kushindwa na kuepusha duru ya pili ya uchaguzi
Mwanamfalme Ali bin al-Hussein alikubali kushindwa na kuepusha duru ya pili ya uchaguziPicha: AFP/Getty Images/F. Coffrini

''Imekuwa safari murua kuwafahamu na kufanya kazi nanyi, na kuziona changamoto zinazowakabili. Shukrani za kipekee ziwaendee nyiye mliokuwa na ujasiri wa kunichagua mimi, na kwa machache hayo najiondoa katika kinyang'anyiro hiki''. Alisema al-Hussein.

Sepp Blatter ambaye ametikiswa na uchunguzi ulioanzishwa na Marekani na Uswisi kuhusu madai ya rushwa ndani ya FIFA, alijitwisha jukumu la kilisafisha shirikisho hilo.

Alisema, ''Na sasa, kama nilivyosema awali, najitwisha jukumu la kuirejeshea heshima FIFA. Mimi ni mtu mwaminifu, na nimesema, naamini kwamba kwa msaada wa Mungu au Allah, tutaiweka FIFA mahali inapopaswa kuwa. Ninawaahidi kuwa nitakabidhi kwa mrithi wangu, FIFA ambayo iko katika hali nzuri.''

Kamata kamata ya FBI

Mkutano mkuu wa FIFA wa mwaka huu ulikumbwa na msukosuko pale maafisa wa uchunguzi wa Marekani walipowakamata maafisa waandamizi saba wa FIFA kwenye hotel yao katika mji wa Zurich walipokuwa wakijiandaa kuingia mkutanoni. Serikali ya Uswisi hali kadhalika ilitangaza kuanzisha uchunguzi katika madai ya ulaghai na rushwa, kuhusiana na nafasi ya kuandaa kombe la dunia la mwaka 2018 nchini Urusi, na 2022 nchini Qatar.

Mkutano mkuu wa FIFA ulikumbwa na msukosuko pale polisi walipowakamata maafisa waandamizi kwa shutuma za rushwa
Mkutano mkuu wa FIFA ulikumbwa na msukosuko pale polisi walipowakamata maafisa waandamizi kwa shutuma za rushwaPicha: Reuters/A. Wiegmann

Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA lilimuwekea shinikizo Sepp Blatter ajiuzulu kutokana na mashinikizo hayo, wito ambao Blatter aliupuuza. UEFA ambayo wanachama wake karibu wote wamempinga Blatter katika uchaguzi wa jana, inapanga kufanya mkutano wiki ijayo, kupanga mikakati mipya dhidi ya kiongozi huyo raia wa Uswisi, ambaye ameiongoza FIFA kwa miaka karibu 17.

Rais wa UEFA mfaransa Michel Platini alitishia kabla ya uchaguzi huo kuwa shirikisho lake linaweza kususia michezo ya kombe la dunia la mwaka 2018 iwapo Blatter angeshinda, hata hivyo, mkuu wa shirikisho la soka la bingwa sasa wa dunia, Ujrumani, Wolfgang Niersbach, amesema kususia kombe la dunia hakuwezi kuwa suluhisho.

Pamoja na upinzani wa Ulaya, Marekani pamoja na washirika wao, Blatter aliungwa mkono sana na Urusi, pamoja na mashirikisho ya soka ya Afrika, Asia, na Amerika Kusini.

Tukiwa bado katika masuala ya Soka leo ni leo kati ya timu mbili zilizotinga fainali za kombe la Ujerumani, Borussia Dortmund na Wolfsburg. Nchini Uingereza nako, Arsenal na Aston Villa zinacheza mechi ya fainali ya kombe la FA katika uwanja wa Wembley baadaye leo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/rtre

Mhariri: Caro Robi