1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti ya mabadiliko ya tabia nchi yatowa onyo

3 Novemba 2014

Mabadiliko ya tabia nchi yanatokea na takriban moja kwa moja yanasababishwa na binaadamu,hayo yamebainishwa na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliozinduliwa Copenhagen ,Denmark Jumapili (02.11.2014).

https://p.dw.com/p/1Dg1L
Visiwa vidogo viko hatarini kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Visiwa vidogo viko hatarini kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.Picha: picture-alliance/DPPI Media

Tathmini ya nne na ya mwisho ya Jopo la Kiserikali kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi haishangazi na wala haikutegemewa kwa vile inachanganya utafiti wa repoti tatu zilizotolewa katika kipindi cha miezi 13 iliopita.

Lakini imetilia mkazo changamoto za mabadiliko ya tabia nchi kwa maelezo mazito. Utowaji wa gesi chafu unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya nishati visukuku yumkini kukahitajiwa kupunguza kufikia kiwango cha sifuri kufikia mwishoni mwa karne hii ili kuiwezesha dunia kuwa na fursa adhimu ya kudhibiti ongezeko la ujoto kuwa chini ya kiwango kinachohesabiwa kuwa cha hatari.

Jopo hilo la IPCC halikusema hasa dunia itakuwaje lakini yumkini kukahitajika mabadliko makubwa ya kuhamia kwenye nishati mbadala kwa matumizi ya majumbani, viwandani na kwa kuendesha magari na kutumia teknolojia mpya kunyonaya gesi ya hewa ukaa ilioko hewani.

Athari kwa binaadamu na mazingira

Ripoti hiyo inaonya kwamba kushindwa kupunguza utowaji wa gesi chafu kutakuwa na athari kwa watu na mazingira ambazo hazitoweza kufanyiwa marekebisho. Baadhi ya tathira tayari zimeanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kupanda kwa maji ya bahari,maji ya bahari kuwa na joto zaidi na yenye tindi kali, kuyeyuka kwa barafu na bahari ya barafu ya Aktiki na hivi karibuni kabisa kuongezeka sana kwa hali ya joto.

Mafuriko yaliosababishwa na mvua mkubwa Pakistan pia yanachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mafuriko yaliosababishwa na mvua mkubwa Pakistan pia yanachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.Picha: REUTERS/M. Raza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo amesema " Sayansi imebainisha.Hakuna ubabaifu katika ujumbe wao. Viongozi lazima wachukuwe hatua.Wakati hauko pamoja nasi."

Licha ya onyo kali ripoti hiyo inasema zana zipo za kuweika dunia katika mkondo wa kupunguza utowaji wa gesi hizo chafu na kuondokana na uraibu wa kutumia nishati visukuku za mafuta, makaa ya mawe na gesi ambazo huchafuwa hali ya anga.

Nia ya mabadiliko

Mwenyekiti wa jopo hilo la IPCC Rajendra Pachauri amesema kile kinachohitajiwa ni nia ya kufanya mabadiliko ambapo wanaamini itachochewa na maarifa na uwelewa wa sayansi ya mabadliko ya tabia nchi.

Rajendra K. Pachauri Mwenyekiti wa Jopo la Mabadiliko ya Tabia Nchi la Umoja wa Mataifa IPCC.
Rajendra K. Pachauri Mwenyekiti wa Jopo la Mabadiliko ya Tabia Nchi la Umoja wa Mataifa IPCC.Picha: picture-alliance/dpa

Jopo la IPCC limeanzishwa hapo mwaka 1988 kutathmini ongezeko la ujoto duniani na taathira zake.Repoti hiyo iliotolewa Jumapili inaaelezea tathimini ya hivi karibuni kabisa ikiwa ni uchambuzi mkubwa kabisa wa tafiti 30,000 za mabadiliko ya tabia nchi ambayo inathibitisha kwa uhakika wa asilimia 95 kwamba sehemu kubwa ya ongezeko hilo la joto dunia lililoshuhudiwa tokea miaka ya 1950 limesababishwa na binaadamu.

Ripoti hiyo inatakiwa iwe ramani kwa ajili ya mazungumzo ya tabia nchi ya Umoja wa Mataifa ambayo yanaendelea mwezi ujao mjini Lima,Peru katika mkutano mkuu wa mwisho kabla ya mkutano wa kilele mjini Paris mwaka ujao ambapo makubaliano ya dunia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yanatarajiwa kufikiwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman