1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Ujerumani Weizsäcker afariki dunia

31 Januari 2015

Rais wa zamani wa Ujerumani Richard Wizseäcker ambaye alikuwa akiheshimiwa kimataifa kama kiunganishi cha kuungana upya kwa Ujerumani amefariki dunia Berlin Jumamosi (31.01.2015) akiwa na umri wa miaka 94.

https://p.dw.com/p/1ETuI
Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker.Picha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Weizsäcker alikuwa rais wa kwanza wa Ujerumani iliyoungana upya na alitimiza dhima muhimu katika kuisaidia nchi kukabiliana na na kipindi chake cha kale cha utawala wa Manazi.

Wakati wa kipindi chake madarakani cha miaka 10 kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1994 alikuwa hakwepi kujihusisha katika mijadala nyeti ya kisiasa kama vile suala la kujumuishwa wageni katika jamii na kadhalika na alikuja kuheshimika ndani na nje ya nchi.

Juu ya kwamba wadhifa huo wa rais kwa kiasi kikubwa ni wa heshima tu alikuja kutambulika kama "rais wa kisiasa" kutokana na weledi wake wa kutowa hotuba za kusisimuwa ambazo mara nyingi zilikuwa kielelezo cha historia yake mwenyewe.

Kumbukumbu kuu

Katika hotuba yake inayokumbukwa sana kuadhimisha miaka 40 ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia aliwaambia wabunge kwamba tarehe nane mwezi wa Mei mwaka 1945 ilikuwa ni siku ya ukombozi kutoka mfumo wa kinyama wa ukatili wa Usoshalisti wa Kizalendo.

Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker akihutubia bunge la Ujerumani. (08.05.1985)
Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker akihutubia bunge la Ujerumani. (08.05.1985)Picha: dpa

Alianza kulitumikia jeshi hapo mwaka 1938 na aliwahi kujeruhiwa mara kadhaa na alikuwa karibu na kaka zake wawili wakati walipouwawa mapema wakati wa vita hivyo vya dunia.Aliliambia gazeti la kila wiki la Spiegel katika toleo lake la mtandao hapo mwaka 2009 kwamba alimzika mwenyewe kaka yake na kwamba alikuwa hana haja ya kueleza mtu anakuwa na hisia gani wakati huo.

Baada ya kumalizika kwa vita alijifunza sheria na historia na ingali akiwa bado ni mwanafunzi alimsaidia mwanasheria kumtetea baba yake Ernst von Weizsäcker ambaye alikuwa afisa mwandamizi wa waziri wa mambo ya nje wa Hitler, Joachim von Ribbentrop katika kesi za Nuremberg zilizokuwa zikiendeshwa na Marekani.

Baba yake alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani na baadae kupunguzwa kuwa cha miaka mitano.

Historia yake

Weizsäcker amezaliwa katika mji wa kusini magharibi wa Stuttgart hapo tarehe 15 mwezi wa Aprili mwaka 1929 ni mtoto wa nne kaika familia ya wasomi.Kutokana na kwamba baba yake alikuwa mwanadiplomasia aliishi maisha yake ya utotoni katika miji tafauti ya Ulaya kabla ya kuanza kusoma katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza na Grenoble kusini mashariki kwa Ufaransa.

Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker.
Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker.Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Baada ya kumalizika kwa vita alikuja kwa haraka kuwa mkuu wa kitengo cha sera za kiuchumi cha kampuni ya viwanda ya Mannesmann kabla ya kujiunga na Benki ya Waldthausen & Co na hapo mwaka 1962 alijiunga na kampuni ya madawa ya Boehringer.

Kutokana na kwamba alikuwa tayari amejiunga na chama cha Christian Demokrat (CDU) hapo mwaka 1954 alikuwa akijishughulisha katika harakati za kisiasa halikadhalika katika masuala ya Kanisa la Kiprotestanti sanjari na maisha yake ya kikazi.Alichaguliwa kujiunga na buge la Ujerumani Bundestag hapo mwaka 1969.

Alikutana na Honecker

Akiwa meya wa Berlin kuanzia mwaka 1981 hadi mwaka 1984 alikuwa meya wa kwanza akiwa madarakani kuitembelea Ujerumani Mashariki ambapo alikutana na kiongozi wake Erick Honecker.

Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker wakati huo akiwa Meya wa Berlin akikutana na kiongozi wa Ujerumani Mashariki Erich Honecker Berlin ya mashariki(15.09.1983)
Rais wa zamani wa Ujerumani Richard von Weizsäcker wakati huo akiwa Meya wa Berlin akikutana na kiongozi wa Ujerumani Mashariki Erich Honecker Berlin ya mashariki(15.09.1983)Picha: picture alliance/dpa

Wizsäcker aligombea urais bila ya mafanikio hapo mwaka 1974 lakini muongo mmoja baadae hapo mwezi wa Mei mwaka 1984 akiwa na uungaji mkono mkubwa alikuja kuwa rais wa sita wa Ujerumani kwa kipindi cha miaka mitano ambapo alishuhudiwa akiikosoa enzi ya kale ya Ujerumani bila ya kificho, kutetea maadili ya kidemokrasia, Ukristo pamoja na kupigania maafikiano.

Hususan alizingatia matatizo ya nchi zinazoendelea, ukosefu wa ajira duniani na utunzaji wa mazingira.

Akiwa nyumbani alitowa wito wa upatanishi na Ujerumani Mashariki na kushajiisha mazungumzo na utawala huo wa Kikomunisti pamoja na kuhimiza mageuzi yaliokuja kuzingatiwa kwa makini chini ya kiongozi wa mwisho wa Muungano wa Kisovieti Mikhali Gorbachov.

Miezi michache kabla ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin alipewa mamlaka ya kipindi cha pili cha urais hapo mwezi wa Mei mwaka 1989 safari hii akiwa na uungaji mkono mkubwa zaidi kuliko hata ilivyokuwa mwaka 1984 na kuja kushuhudia kuungana upya kwa Ujerumani mwishoni mwa Vita Baridi.

Kuungana upya kwa Ujerumani

Hapo tarehe tatu mwezi wa Oktoba mwaka 1990 siku ambayo Ujerumani iliungana tena baada ya zaidi ya miaka 40 alisisitiza umuhimu wa kuwa na msimamo wa pamoja kwa changamoto zinazowakabili na kuonya kwamba mikopo mikubwa pekee haiwezi kugharamia umoja.

Mojawapo ya shamra shamra za kuungana upya kwa Ujerumani mwaka 1990.
Mojawapo ya shamra shamra za kuungana upya kwa Ujerumani mwaka 1990.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema kuungana tena kunamaanisha kujifunza kushirikiana kile kiliopo.

Weizsäcker ambaye ameacha mjane Marianne na watoto watatu aliendelea kuitumikia jamii katika shughuli mbali mbali za kisiasa na za hisani baada ya kuacha wadhifa huo wa rais.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Amina Abubakar