1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Uhuru Kenyatta atimiza mwaka mmoja madarakani

Abdu Said Mtullya9 Aprili 2014

Leo unatimia mwaka mmoja tokea Rais Uhuru Kenyatta aanze kuiongoza Kenya.Katika hotuba yake ya kuingia madaraka Kenyatta alitoa ahadi nyingi. Jee amezitekeleza kwa kiasi gani.

https://p.dw.com/p/1BeIj
Rais Uhuru kenyatta wa Kenya
Rais Uhuru Kenyatta wa KenyaPicha: picture-alliance/AA

Ni mwaka mmoja, tokea Rais Kenyatta aapishwe kuanza kulitumikia taifa la Kenya .

Alitoa ahadi nyingi; ikiwa pamoja na kuuendeleza uchumi, kuuimarisha umoja wa taifa na kuweka utaratibu wa huduma za afya zinazoweza kulipiwa na kila mwananchi .Rais Kenyatta pia aliahidi kuleta uhakika wa chakula, kutenga nafasi za ajira kwa vijana na kugawa "Laptop" kwa watoto wote wa shule za msingi.Lakini aliyoweza kuyafanya ili kuzitekeleza ahadi hizo ni machache hadi sasa.

Bei za vyakula zimezidi kupanda, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana bado ni wa kiwango cha juu na hasa katika sehemu za mashambani .Aidha mpango wa kugawa "Laptop" kwa watoto wa shule umesahauliwa ndani ya mtoto wa meza kufuatia kashfa.

Mwandishi habari mmoja Inchikirwa Ndelejai amesema serikali ya Kenyatta haijafanya mengi. Amesema serika ya mfungamano wa Jubilee haijafanya ya kutosha. Ameeleza kwamba serikali haikufanya kama ilivyoahidi.

Mwandishsi habari huyo amesema ,ikiwa mtu atawapima wanasiasaa katika msingi wa ahadi walizozitoa, basi kilichofanyika hadi sasa ni cha kusikitisha.

Hatua fulani zapigwa

Hata hivyo hatua kadhaa zimepigwa na serikali ya Kenyatta katika kuzitekeleza baadhi ya ahadi.

Mara tu baada ya kuchaguliwa Kenyatta alianza kuutekeleza utaratibu wa kutoa huduma kwa ajili ya wajawazito bila ya malipo.Akina mama hawalipii gharama za kupimwa wanapokuwa wajawazito na pia hawalipii gharama za kujifungua.Katika hotuba yake Rais Kenyatta ,alisifu mafanikio yaliyopatikana katika uchumi na hatua zilizochukuliwa katika kupambana na ufisadi.

Watoto wa shule Kenya waliahidiwa ''Laptop''
Watoto wa shule Kenya waliahidiwa ''Laptop''Picha: dapd

Hatua fupi katika kupambana na ufisadi

Hata hivyo kuhusu ufisadi ndani ya polisi,mwakilishi wa Wakfu Ujerumani wa " Heinrich Böll" nchini Kenya Katrin Seidel amesema kwamba maafisa wengi wa polisi waliohusika na vitendo vya ufisadi vilivyoweza kuthibitishwa bado wanaendelea na kazi na bado wamo katika ngazi za uongozi pia katika idara ya usalama. Mwakilishi huyo wa Wakfu wa Ujerumani ,bibi Seidel amesema watu wengi nchini Kenya wanahisi kwamba hawahudumiwi kwa kiwango cha kutosha katika suala la usalama.

Kutokana na shambulio la magaidi kwenye jengo la maduka,Westgate mjini Nairobi mwezi Septemba mwaka uliopita Wakenya wengi wamepoteza imani juu ya idara za usalama. Lakini juu ya suala la usalama Rais Uhuru Kenyatta amesema " usalama wa watu wetu na ulinzi wa mipaka ya nchi ni miongomi mwa wajibu wangu mkuu." Rais Kenyatta amesema vitisho vyovyote dhidi ya mipaka ya Kenya vitakabiliwa kwa uwezo na nguvu zote za watu wa Kenya.

Shambulizi kwenye majengo ya Westgate mjini Nairobi liliwashtua wakenya wengi
Shambulizi kwenye majengo ya Westgate mjini Nairobi liliwashtua wakenya wengiPicha: DW/J. Shimanyula

Umaarufu wa Kenyatta katika utaifa

Katika upande mwingine Rais Kenyatta anatumia turufu ya utaifa ili kuhakikisha umaarufu wake. Hata kesi inayomkabili kwenye Mahakama Kuu ya Kimataifa ya ICC inapalilia umaarufu wake.

Rais Kenyatta anakabiliwa mashkata ya uhalifu dhidi ya binadamu. Katika ghasia zilizotokea nchini Kenya kufuatia uchaguzi wa Rais mnamo mwaka wa 2007 inadaiwa kuwa Kenyatta ambae wakati huo alikuwa kiongozi wa chama ndiye aliehamamisha makundi yaliyowatimua watu wa makabila mengine,yaliyofanya ubakaji na kuwaandama watu wa jamii nyingine.

Mwandishi:Fischer ,Hilke,

Tafisiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Yusuf Saumu