1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama katika ziara Saudi Arabia

27 Januari 2015

Marekani yasema pana haja ya kulizungumzia suala la haki za binadamu ingawa rais Obama ameashiria kutokuwa tayari kulizungia suala hilo katika ziara hii inayokusudiwa kutoa pole kwa kifo cha mfalme Abdullah

https://p.dw.com/p/1ERDL
Rais Obama akipokelewa na mfalme Salman Abdul Aziz al Saud alipowasili wanja wa Kimataifa wa Mfalme Khaled
Rais Obama akipokelewa na mfalme Salman Abdul Aziz al Saud alipowasili wanja wa Kimataifa wa Mfalme KhaledPicha: Reuters/J. Bourg

►Rais Barack Obama wa Marekani ametetea nia ya Marekani ya kuwa na ushirikiano wa karibu na Saudi Arabia katika suala la usalama wa taifa licha ya kuwepo mashaka makubwa juu ya kukiukwa haki za binadamu katika taifa hilo la kifalme. Rais Obama aliyewasili mchana wa leo(27.01.2015) mjini Riyadh Saudi Arabia kutowa pole kufuatia kifo cha Mfalme Abdullah amesema ni muhimu kwake kutilia mkazo juu ya haki za Binadamu nchini Saudi Arabia.

Nafasi ya Saudi Arabia kama mojawapo ya washirika muhimu wa Marekani katika ulimwengu wa Kiarabu imeonekana baadhi ya wakati kuongeza wasiwasi wa Marekani juu ya nchi hiyo kufadhili magaidi pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu.

Obama akisalimiana na mfalme wa Saudia Salman
Obama akisalimiana na mfalme wa Saudia SalmanPicha: Reuters/J. Bourg

Katika ziara hii, Rais Obama amesema ameona pana haja na umuhimu mkubwa wa kuishinikiza nchi hiyo kuhusu suala la ukiukaji wa haki za binadamu hata ikiwa pana ushirikiano katika masuala mbali mbali. Obama amesema baadhi ya wakati wanahitaji kuweka uwiano kati ya kuzungumzia suala la haki za binadamu na nchi hiyo na wasiwasi uliopo katika mapambano dhidi ya ugaidi au suala zima la usalama wa kanda hiyo. Kauli hiyo ya rais wa Marekani imetokana na mahojiano aliyofanyiwa na kituo cha televisheni cha Marekani CNN yaliyorushwa hewani kabla ya Obama kuwasili mjini Riyadh.

Obama aliwasili Riyadh pamoja na mkewe Michelle na kupokelewa na Mfalme Salman bin Abdul Aziz al-Saud. Viongozi kadhaa wa Saudi Arabia walimkaribisha Obama baada ya nyimbo za mataifa yote mawili kupigwa na bendi ya jeshi katika uwanaj wa ndege wa Riyadh.

Rais Obama ambaye yuko Saudia kwa masaa manne amepangiwa kuwa na mazungumzo ya kwanza kiserikali na Mfalme Salman na baadaye kuhudhuria chakula cha jioni na viongozi wengine wa Kisaudi katika kasri la Erga.

Hata hivyo, tayari rais huyo wa Marekani ameshaashiria kwamba katika mazungumzo ya mfalme huyo wa Saudi Arabia hatoligusia suala la wasiwasi wa Marekani kuhusiana na hatua ya kupigwa viboko mwandishi wa blogu, Raif Badawi, aliyeshtakiwa kwa kuukashifu Uislamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na viboko 1,000. Mwandishi huyo wa blogu alianza awamu ya kwanza ya kupigwa viboko mapema mwezi huu wa Januari mbele ya mamia ya watu mjini Jeddah, ingawa awamu ya pili imeakhirishwa baada ya daktari kusema majeraha aliyoyapata kutokana na awamu ya kwanza ya kucharazwa viboko hayajapona.

Obama akisalimiana na mfalme wa Saudia Salman
Obama akisalimiana na mfalme wa Saudia SalmanPicha: Reuters/J. Bourg

Badala yake, Obama amesema ziara yake hii zaidi inalenga kutowa pole na heshima kwa kifo cha Mfalme Abdullah ambaye amemtaja kuwa mtu aliyeonekana kwa kuwakilisha baadhi ya mageuzi ya kwenda na wakati wa sasa ndani ya taifa hilo la kifalme.

Katika ziara hiyo Obama anafuatana na ujumbe mzito unaomjumuisha Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry, mawaziri wa zamani wa mambo ya nje, Condolezza Rice na James Baker, wote waliofanya kazi chini ya utawala wa marais wa upande wa chama cha Republican, miongoni mwa wengine.

Ikumbukwe kwamba tangu alipofariki Mfalme Abdullah Ijumaa iliyopita viongozi mbali mbali wa dunia wamekuwa wakifanya ziara Saudi Arabia kwa lengo la kutowa pole na kukutana na mfalme mpya Salman Abdul Aziz Al Saud.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef