1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikwete apendekeza DRC izungumze na M23

16 Aprili 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amefanya mahojiano na mwandishi wetu wa DW aliyeko Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Saleh Mwanamilongo Jumanne (15.04.2014) nchini Tanzania

https://p.dw.com/p/1BjVH
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam. (15.04.2014)
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam. (15.04.2014)Picha: DW/S. Mwanamilongo

Katika mahojiano hayo yaliofanyika Ikulu ya Dar-es-Salaam yaliyodumu kwa takriban dakika arobaini Rais Kikwete ameelezea maoni yake juu ya shughuli za kulinda amani za kikosi cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambapo wanajeshi wa Tanzania wanashiriki,mjadala unaoendelea katika bunge la katiba nchini Tanzania kuhusu rasimu ya katiba,uhusiano wake na Rwanda na nafasi ya Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nini tathmini yako ikiwa ni mwaka mmoja baada ya majeshi ya Tanzania kupelekwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika Jimbo la Kivu kaskazini kushiriki katika shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa?

Mimi nadhani watakaoweza kufanya tathmini ni Wacongo wenyewe kama shughuli hiyo inafanikiwa.Utashi wangu kwanza ni kwamba wanajeshi wetu wako salama tumepoteza vijana watatu na tuna masikitiko makubwa kwa hilo lakini tunafurahi ile kazi wameifanya vizuri na lile tatizo kubwa lilioko pale la waasi wa kundi la M23 pengine limefika mwisho wake. Kilichobakia sasa ni mchakato wa kisiasa kuzungumza na waasi hao ili suala hilo limalizike kabisa. Hivi sasa wanajeshi wetu wanalisaidia jeshi la Congo kushughulikia suala la kupambana na waasi wa kundi la FDLR- NALU ambalo wanakwenda nalo vizuri.

Unadhani lilikuwa jambo la busara kwa viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADCC kutaka kikosi hicho kiwepo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa?

Ni jambo zuri kwani wakati tulipoanza katika Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu tulikubaliana tuanzishe jeshi hilo sisi wenyewe lakini zaidi liwe linajishughulisha katika kulinda mpaka kati ya Congo na Rwanda kwa sababu nchi hizo zilikuwa zinatiliana mashaka kila moja ikimshutumu mwenzake kwa kufanya mambo mabaya na kwa pamoja viongozi wakakubaliana waunde jeshi hilo litakalokaa mpakani kulinda amani na kuzipa uhakika nchi hizo mbili kwamba hakuna atakayejipenyeza kwenye nchi zao.Wakati tukikijadiliana juu ya suala hilo ndipo Umoja wa Mataifa ukapendekeza jeshi hilo tunalotaka kuunda liwe sehemu ya jeshi la Umoja wa Mataifa ambalo tayari liko Congo ili kusiwepo na majeshi mawili yanayofanya kazi hiyo hiyo. Baada ya kujadiliana kwenye nchi za maziwa makuu na jumuiya ya SADCC tukakubaliana kwa pamoja kwamba ni wazo zuri.

Hivi sasa mamlaka ya kikosi hicho yanaongezwa kwa mwaka mmoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unafikiri kikosi hicho cha kimataifa kinaweza kuyapokonya silaha au kuyatokomeza makundi ya waasi yaliyobakia likiwemo hilo FDLR-ADF-NALU?

Kitu kikubwa kitakachotokea ni ushirikiano kati ya makundi hayo ambapo wenyewe wakijitolea kuacha silaha itasaidia sana badala ya kwenda kuwasaka, lakini kama hawatafanya hivyo itabidi kuwasaka lakini sijuwi kama mwaka mmoja utatosha au hautoshi au pengine utachukuwa muda mfupi zaidi ya huo itategemea tu ukubwa wa kazi ambayo siwezi kuisemea kwa sababu sijuwi kwa hakika hali ikoje.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika mahojiano na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam.(15.04.2014)
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania katika mahojinano na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam.(15.04.2014)Picha: DW/S. Mwanamilongo

Wakati wa ziara yake nchini Tanzania Rais Barack Obama alizungumza na wewe kuhusu juhudi za pamoja za kutatuwa mzozo wa Congo na matatizo ya kanda ya maziwa makuu.Hizo hasa ni juhudi gani na hadi sasa zimefikia wapi?

Katika mazungumo yake alieleza maoni yao kuhusu amani na utulivu katika eneo hili na kuelezea utayari wa Marekani kusaidia pale nchi za kanda hiyo zitakapoona Marekani inaweza kutowa mchango wake.

Ni kweli kwamba Tanzania imetengwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ?

Nani ametutenga!Mimi sioni kama Tanzania imetengwa, imetengwa katika kitu gani? Sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki tunashiriki mambo yote ya jumuiya hiyo na mikutano yake yote na tunatimiza mambo yote yanayotuhusu kwa hiyo dhana kwamba tumetengwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki sio ya kweli.Mwezi huu mkutano wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika Arusha kwa hiyo jambo hilo wala halipo.

Kuna juhudi gani katika kurekebisha uhusiano wenu na Rwanda?

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwandishi Saleh Mwanamilongo Dar- es -Salaam.Picha: DW/S. Mwanamilongo

Mini nadhani wanayakuza zaidi mambo hayo kulikoni ukweli wenyewe kwani ukweli wenyewe ulivyo mimi sidhani kwamba uhusiano wetu sisi na Rwanda umefikia hali ya kuwasumbuwa watu,mimi silioni tatizo.

Je ni kweli kwamba Tanzania hivi sasa imeanza kufikiria kuwa na uhusiano zaidi wa kibiashara na kiuchumi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Burundi kuliko nchi nyengine za kanda hii?

Tanzania inapakana na Congo, Rwanda,Burundi,Uganda na Kenya na katika nchi zote hizo tuna mahusiano ya kiuchumi na biashara na kwamba sasa hivi tuna uhusiano na Congo badala ya nchi hizo nyengine sio kweli, suala hilo halipo na miaka yote tumekuwa na uhusiano na nchi hizo.

Wakati taifa la Tanzania likiwa katika mchakato wa kupata katiba mpya kumekuwa na mvutano mkubwa nchini.Una imani kuwepo kwa katiba hiyo mpya kutachangia kuimarisha muungano na sio kuuvunja kabisa muungano huo?

Muungano hautovunjika.Mimi napenda kuwepo kwa mjadala ule ili mambo haya yazungumzwe kwa uwazi, watu wenye mambo kifuani mwao wayatowe yatoke .....wapumuwe, kila mmoja anazungumza anavyoweza kuzungumza yeye na katika nchi ya kidemokrasia ni vizuri kuwaachia watu kuwa na uhuru.Jambo hilo la katiba limekuwa na maneno mengi wengine wanasema hata muungano wenyewe haukuwa halali kwa hiyo ni kipindi cha kusema yote lakini hatima ya yote uamuzi utafanyika.Mimi naamini wabunge watafanya uamuzi wa busara utakaoipatia nchi yetu katiba itakayolisogeza taifa letu miaka mia moja mbele nchi ikiwa salama na umoja,demokrasia, haki za binaadamu zinaheshimiwa ,utawala wa sheria upo na kubwa zaidi kuwepo na misingi mizuri zaidi ya uchumi kukua na watu maisha yao kuwa bora zaidi. Nafurahi kwamba tunao mchakato huo na nafurahi zaidi kwamba watu wanazungumza kwa uwazi kuhusu jinsi wanavyotaka katiba yao iwe, ni jambo jema na ndivyo ilivyo demokrasia kwa hiyo mjadala huo wala hausumbuwi akili yangu.

Mahojiano : Saleh Mwanamilongo

Imeandikwa na : Mohamed Dahman

Mhariri : Mohammed Abdul-rahman