1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yashutumiwa kushindwa kulinda haki za wafanyakazi

23 Aprili 2014

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeishutumu Qatar kwa kushindwa kuwalinda wafanyakazi wa nyumbani kutoka mataifa ya kigeni

https://p.dw.com/p/1BmTC
Picha: AP

Ripoti iliyochapishwa leo na shirika la Amnesty International iliyopewa jina usingizi wangu ndiyo mapumziko yangu inaonyesha kuwa wafanyakazi wa nyumbani kutoka mataifa ya kigeni wanakabiliwa na unyanyasaji ukiwemo kutumikishwa,kufanya kazi kwa saa nyingi bila mapumziko,kutukanwa kupigwa na hata kudhalilishwa kingono.

Wengi wa wafanyakazi hao huhadaiwa kwenda nchini Qatar kwa ahadi za kupata mishahara mikubwa na mazingira mazuri ya kazi lakini wachunguzi wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu wanasema wengi wa wafanyakazi hao wa nyumbani wanafanyishwa kazi hadi saa 100 kwa wiki, siku saba mfululizo, bila siku za mapumziko na hawaruhisiwi kuondoka kutoka nyumba wanazofanyia kazi.

Wafanyakazi wa kike wateswa

Mtafiti wa Amnesty International Regina Spöttl amesema utafiti wao nchini humo umegundua visa vya kuogofya ambapo wafanyakazi hao wanapitia masaibu ya kusikitisha na haki zao haziheshimiwi.

Mtaalamu wa Amnesty International Qatar Regine Spöttl
Mtaalamu wa Amnesty International Qatar Regine SpöttlPicha: privat

Mwanamke mmoja aliyezungumza na wachunguzi hao aliwaonyesha kovu kifuani mwake lililotakana na kuchomwa na muajiri wake kwa kutumia pasi baada ya kujaribu kutoroka.Mwanamke huyo alikamatwa na polisi na anazuiwa katika kituo cha kuwazuia wahamiaji haramu.

Qatar kama nchi nyingine katika kanda hiyo zina mfumo ambao waajiri wana mamlaka makubwa juu ya wafanyakazi wao wa kigeni ambao wana mikataba nao, ambayo imakuwa vigumu kuacha kazi na kwenda kwingine au hata kurejea makwao kwani wanadhibiti hati zao za usafiri na vibali vya kuishi nchini humo.

Kulingana na shirika la Amnesty International kuna kiasi ya wafanyakazi 84,000 wa nyumbani kutoka nchi za kigeni nchini Qatar wengi wao kutoka nchi za kusini mashariki mwa Asia na barani Afrika.

Qatar yatakiwa kuchukua hatua

Amnesyt International inasema Qatar haionekani kuwachukulia hatua raia wake wanaoshutumiwa kuwatesa wafanyakazi wa nyumbani wengi wao wanawake ambao wakati mwingine wanabakwa kutokana na kile maafisa nchini humo wanasema ni ukosefu wa ushahidi.

Nembo ya shirika la Amnesty International
Nembo ya shirika la Amnesty International

Wanawake wanaojaribu kushitaki visa vya ubakaji hujikuta katika hatari ya kufunguliwa mashitaka ya uzinzi.

Hii inakuja baada ya mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kuishutumu Qatar pia kwa kuwatesa wafanyakazi wanaohusika katika sekta ya ujenzi hasa wanaoshughulika na ujenzi wa viwanja vya michezo huku nchi hiyo ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia la kandanda mwaka 2022.

Ahadi za kipindi cha nyuma kutoka Qatar za kuboresha sheria za kuwalinda wafanyakazi hazijatimizwa na shirika la Amanesty International linaitaka nchi hiyo kuacha kujikokota kutekeleza sera za kuimarisha maisha ya wafanyakazi na kuwahakikishia wafanyakazi hao wa kigeni usalama na kuzingatiwa kwa haki zao za kimsingi ili kukomesha kile ilichokiita utumwa mambo leo.

Mwandishi.Caro Robi/dpa/ap/afp

Mhariri: Gakuba Daniel