1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Power asifu juhudi za kudhibiti Ebola Freetown

Josephat Nyiro Charo28 Oktoba 2014

Samantha Power amesema mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown, umeongeza mara tatu idadi ya mazishi salama ya wahanga wa Ebola katika wiki iliyopita na changamoto sasa ni kuutanua utaratibu huo nchi nzima.

https://p.dw.com/p/1Dd33
UN Botschafterin Samantha Power
Picha: Reuters

Akiendelea na ziara yake katika nchi tatu za Afrika Magharibi zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Ebola, zikiwemo Sierra Leone, Liberia na Guinea, Samantha Power ameyaeleza maziko yanayofanywa kwa njia iliyo salama ya watu wanaokufa kutokana na Ebola mjini Freetown kuwa hatua ya kutia moyo katika kuudhibiti ugonjwa huo. Amesema tangu rais wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, alipoamuru kila mtu anayefariki katika eneo la Freetown azikwe salama katika saa 24, timu zinazofanya maziko zimefaulu kwa zaidi ya asilimia 95 kuwazika watu katika muda wa masaa 24.

"Kwa hiyo huoni tu mfano jinsi Ebola inavyoweza kudhibitiwa, lakini pia njia ambazo pande zote zinatakiwa kushirikiana pamoja. Hapa Sierra Leone Marekani inashirikiana kwa karibu na serikali na washirika wetu wa kimataifa kukitafuta kirusi cha Ebola na kuzuia kuenea kwake."

Wakazi mjini Freetown hupiga simu kwa nambari maalumu kuripoti mtu yeyote ambaye huenda ameambukizwa Ebola au maiti iondolewe. Timu maalumu zinazoshughulika na mazishi zimetumwa kufanya kazi maeneo mbalimbali na lengo ni kuhakikisha maiti zinaondolewa katika kipindi cha masaa 24 baada ya simu kupokelewa.

Ernest Bai Koroma Wahlen in Sierra Leone
Rais wa Sierra Leone, Ernest Bai KoromaPicha: AFP/Getty Images

Power, ambaye ataizuru Liberia leo, amesema kuongeza mazishi yanayofanywa kwa usalama nchini kote Sierra Leone yumkini kukasaidia kubadili mkondo wa maambukizi, lakini ni muhimu pia kuhakikisha kuna vitanda vya kutosha vya matibabu. Power pia amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa afya wa kigeni na kutambua kujitolea kwao kwa dhati kusaidia juhudi za kudhibiti Ebola.

"Ni muhimu sana kwamba wafanyakazi wa afya wanaokuja hapa, wanaoacha familia zao, maisha mazuri na kutembelea hapa na wako tayari kujiweka karibu na ugonjwa wa Ebola, wajihisi wanakaribishwa tena Marekani. Wakati huo huo, nadhani kuna hofu ya kweli."

Balozi wa Uingereza nchini Sierra Leone, Peter West, amesema data zinaonyesha asilimia 80 ya maambukizi katika eneo la Afrika Magharibi yalisababishwa na kushika maiti za watu waliokufa kutokana na Ebola. Uingereza imekuwa msitari wa mbele kuisaidia serikali ya Sierra Leone kukabiliana na Ebola na hadi sasa imetenga mamilioni ya dola, baadhi ya fedha hizo zikitumika kujenga vitanda vipatavyo 600, vituo 200 vya jamii, kuwapa mafunzo wafanyakazi wa afya na timu za wanaofanya mazishi na kuongeza uwezo wa maabara.

Hatari ya hofu inayotokana na Ebola

Wakati haya yakiarifiwa katibu mkuu wa muungano wa kimataifa wa mashirika ya msalaba mwekundu na hilal nyekundu, Elhadj As Sy, alionya kwamba hofu inayosababishwa na Ebola huenda ikayafuta mafanikio yaliyopatikana katika mapambano ya kuudhibiti ugonjwa huo.

Elhadj As Sy IKRK Generalsekretär
Katibu mkuu Elhadj As SyPicha: picture alliance/AA/Murat Unlu

"Nina wasiwasi zaidi kuhusu taharuki na hofu na unyanyapaa na ubaguzi. Kwa sababu mambo hayo yanaweza kuuchochea mlipuko wa Ebola kuliko kirusi chenyewe kinachosababisha ugonjwa huo," aliongeza kusema katibu mkuu huyo.

Katibu mkuu huyo mpya alisema kuna haja ya kuwaelisha watu, kuwafahamisha kwa njia iliyo sahihi na kwa kina Ebola ni nini, jinsi unavyoambukizwa na vipi haumbukizwi, ili tuwe na uelewa ulio wazi kabisa wa matatizo, tuwe macho na tuwajibike kuchukua hatua zifaazo, badala ya kutaharuki na kusababisha tabia mbaya ambazo hazitasaidia.

Marekani yafanyia mageuzi utaratibu wake

Wakati huo huo, maafisa wa Marekani jana waliifanyia mabadiliko miongozo kwa madaktari na wauguzi wanaorejea nyumbani nchini humo wakitokea Afrika Magharibi walikokwenda kuwatibu wagonjwa wa Ebola, kufuatia wimbi la ukosoaji kuhusu taratibu za kuwaweka watu karantini, ukiwemo ukosoaji kutoka kwa karibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.

Hatua ya muuguzi wa Marekani kuwekwa karantini ya lazima mjini New York baada ya kuwatibu wagonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone iliibua utata na lawama kutoka kwa mwanamke huyo kwamba haki zake zimekiukwa. Muuguzi huyo aliachiwa jana, siku moja baada ya jimbo la New York kulegeza sheria zake kali za karantini kutokana na shinikizo la utawala wa rais Barack Obama.

Mkurugenzi wa Taasisi za kudhibiti na kuzuia magonjwa nchini Marekani, CDC, Dr Thomas Frieden, ametaka karantini ya kujitolea kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa Ebola, lakini akasema wafanyakazi wengi wa afya wanaorejea kutoka nchi tatu zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo Afrika Magharibi, watahitaji kufuatiliwa kwa karibu bila kuwekwa karantini. Taratibu hizo mpya za utawala wa rais Barack Obama si za lazima na majimbo yatakuwa na haki ya kuweka sera kali zaidi kukabiliana na Ebola.

Mwandishi:Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir