1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Platini ajiondoa katika uchaguzi wa FIFA

29 Agosti 2014

Rais wa Shirikisho la Soka Ulaya - UEFA Michel Platini amesema hatosimama na Sepp Blatter katika uchaguzi wa urais wa Shirikisho la Soka Duniani – FIFA, ijapokuwa anataraji kuwa kuna yule atakayejitokeza.

https://p.dw.com/p/1D3qp
UEFA Präsident Michel Platini
Picha: Fabrice Coffrini/Getty Images

Platini amesema hatogombea katika uchaguzi huo wa mwezi Mei dhidi ya Blatter, akisisitiza kuwa haikuwa hatua ya kukwepa kinyang'anyiro dhidi ya mtu ambaye alimfunza kazi.

Uamuzi wa Platini,uliokuwa umetarajiwa, unamwacha Blatter mwenye umri wa miaka 78 na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo na kuongoza kwa muhula wake wa tano na kuna uwezekano wa yeye kuchaguliwa bila kupingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

Platini mwenye umri wa miaka 59 amesema ataangazia badala yake katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka ujao wa kuendelea kuongoza UEFA, na pia kujaribu kuwania katika uchaguzi wa rais wa FIFA mwaka wa 2019.

FIFA imeweka mwishoni mwa Januari kama muda wa mwisho kwa wagombea wote kutangaza nia yao ya kusimama katika uchaguzi huo wa Mei 29 mjini Zurich. Aliyekuwa Mkurugenzi wa mahusiano ya kimataifa wa FIFA Jerome Champagne amesema atagombea, ijapokuwa anakiri kuwa itakuwa vigumu kumpiku bosi wake huyo wa zamani na ambaye ni mshirika wake wa muda mrefu.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu