1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pillay aikosoa vikali Israel

23 Julai 2014

Huku Marekani ikiendelea na jitihada zake za kupatikana kwa usitishaji wa mapigano kwenye Ukanda wa Gaza, Umoja wa Mataifa umesema kuna dalili Israel inafanya uhalifu wa kivita na mauaji yakiendelea.

https://p.dw.com/p/1Ch0f
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, akizungumza kwenye kikao maalum juu ya Gaza tarehe 23 Julai 2014, mjini Geneva.
Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, akizungumza kwenye kikao maalum juu ya Gaza tarehe 23 Julai 2014, mjini Geneva.Picha: Reuters

Katika kile kinachoonekana kuwa ni kauli kali kabisa kuwahi kutolewa na Umoja wa Mataifa tangu Israel ilipoanza kuishambulia Gaza wiki mbili zilizopita, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja huo, Navi Pillay, amekiambia kikao cha dharura cha kamisheni hiyo mjini Geneva hivi leo, kwamba Israel imekuwa ikitumia nguvu zilizopindukia.

Licha ya Pillay kulaani pia urushwaji wa makombora kutoka Gaza kuelekea Israel, bado amelaani vikali mashambulizi ya Israel yanayowalenga watoto, wanawake na watu wenye ulemavu katika kiwango ambacho amesema hakivumiliki.

"Siku mbili zilizopita, mnamo tarehe 21 Julai, makombora ya Israel yalipiga Hospitali ya Al-Aqsa katika eneo la Djier al-Barra, yakiripotiwa kuuwa kwa uchache watu watatu na kuwajeruhi wengine kadhaa wakiwemo madaktari. Hii ni mifano michache tu ambapo kunaonekana kuwepo uwezekano mkubwa kwamba sheria za kimataifa za kibinaadamu zimekiukwa katika kiwango ambacho kinaweza kuwa uhalifu wa kivita. Kila moja kati ya visa hivi lazima kichunguzwe kwa ukamilifu na kwa uhuru." Amesema Pillay.

Naye Naibu Mkuu Kamisheni ya Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, Kyung-Wha Kang, amekiambia kikao hicho cha dharura kilichoitishwa mahsusi kujadili jaala ya Gaza, kwamba ndani ya siku mbili zilizopita, mtoto mmoja wa Kipalestina amekuwa akiuawa kila saa.

Waombolezaji katika hospitali ya Khan Younis kusini mwa Gaza, baada ya Mpalestina mwengine kuuawa tarehe 23 Julai 2014.
Waombolezaji katika hospitali ya Khan Younis kusini mwa Gaza, baada ya Mpalestina mwengine kuuawa tarehe 23 Julai 2014.Picha: Reuters

"Huko Gaza, watu 443 au zaidi ya asilimia 74 ya waliokwishakuuawa ni raia, na robo moja ya raia waliouwa hadi sasa ni watoto. Mtoto mmoja amekuwa akiuwa kila baada ya saa moja ndani ya kipindi cha siku mbili sasa. Kila mmoja kati ya watoto hawa alikuwa na jina na mustakabali na maisha yake ambayo yamekatwa katika hali ya kutisha." Amesema Kang.

Israel yajibu kwa hasira

Palestina iliomba kuitishwa kwa kikao hiki cha dharura, ambacho hatimaye kitalipigia kura azimio ililoliwasilisha. Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Eviatar Manor, amejibu shutuma dhidi ya nchi yake kwa lugha kali akisema kamwe Israel haitawacha kuwalinda raia wake.

"Azimio ambalo litawasilishwa kwenu leo kwa ujumla halina uwiano, la kibaguzi na linaloharibu. Linatia mafuta kwenye moto. Inalizawadia kundi la wahalifu na kuuadhibu upande unaowalinda raia wake. Baraza hili liwache kutafuta sarafu kwenye taa za barabarani. Linaweza tu kurejesha heshima yake kwa kuilaani Hamas vikali," alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, mjini Jerusalem tarehe 23 Julai 2014, ambako wawili hao wanasaka usitishwaji wa mapigano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, mjini Jerusalem tarehe 23 Julai 2014, ambako wawili hao wanasaka usitishwaji wa mapigano.Picha: Reuters

Hayo yakitokea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amewasili Tel Aviv katika jitihada za kusaka usitishwaji wa mapigano kati ya Israel na Hamas.

Msemaji wa wizara hiyo, Jen Psaki, amesema Kerry amewasili Israel asubuhi ya leo, ambako atakutana na maafisa wa serikali kabla ya kuelekea Ukingo wa Magharibi kuonana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, na baadaye kukutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo