1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Peshmerga wawajeresha nyuma IS

Mohammed Khelef19 Desemba 2014

Operesheni ya siku mbili ya kijeshi ya wapiganaji wa Peshmerga katika jimbo la Kurdistan imefanikiwa kufungua njia kuelekea Mlima Sinjar, uliokuwa umezingirwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1E7JH
Wapiganaji wa peshmerga baada ya ushindi kwenye mji wa Zumar dhidi ya Dola la Kiislamu.
Wapiganaji wa peshmerga baada ya ushindi kwenye mji wa Zumar dhidi ya Dola la Kiislamu.Picha: picture alliance/Emrah Yorulmaz/Anadolu Agency

Mafanikio haya ni muhimu sana katika mapambano ya kuuchukuwa mji wa Sinjar, ulio chini ya mlima wenye jina hilo hilo, ambao ulichukuliwa na IS tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu. Mkuu wa Baraza la Usalama la Mkoa wa Kurdistan, Masrur Barzani, amesema vikosi vya Kikurdi vilisonga mbele jioni ya jana kuelekea kwenye mlima huo.

"Leo tumekamilisha operesheni ambayo tuliianza jana, na ambayo inasimamiwa na mwenyewe Rais Masoud Barzani, ikihusisha eneo zima kutoka Zumar hadi Mlima Sinjar, kulikomboa eneo kubwa la Kurdistan, na pia kuwaokoa watu wa jamii ya Yazidi waliokwama mlimani. Ilikuwa operesheni kubwa na tunashukuru imefanikiwa," amesema kiongozi huyo.

Maelfu ya Wayazidi walikuwa wamekwama kwenye mlima huo mwanzoni mwa mwezi Agosti, wakati wapiganaji wa IS walipoichukua miji hiyo ya Sinjar na Zumar, na hivyo kuchochea wimbi kubwa la uhamaji.

Licha ya kwamba wengi wao waliondoshwa kwa njia ya anga au kusindikizwa na vikosi vya usalama kupitia Syria na kisha kurudi Iraq kujihifadhi kwenye jimbo la Kurdistan, lenye mamlaka yake ya ndani, lakini wengine wengi walikuja baadaye na kubakia wamekwama mlimani.

Marekani yauwa viongozi wa IS

Vijiji ambavyo vimechukuliwa hivi karibuni na vikosi vya Peshmerga vinaonesha ishara za mapigano makubwa, huku majengo mengi yakiwa yameharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya anga ya Marekani. Mkuu wa operesheni ya Marekani, Luteni Jenerali James Terry, amesema eneo lililochukuliwa na peshmerga lina ukubwa wa kilomita za mraba 100.

Wapiganaji wa peshmerga wakifurahia baada ya ushindi kwenye mji wa Zumar dhidi ya Dola la Kiislamu.
Wapiganaji wa peshmerga wakifurahia baada ya ushindi kwenye mji wa Zumar dhidi ya Dola la Kiislamu.Picha: Safin Hamed/AFP/Getty Images

Katika hatua nyengine, Marekani inasema operesheni yake ya kijeshi nchini Iraq na Syria imewauwa viongozi kadhaa wa IS, katika siku za hivi karibuni. Msemaji wa jeshi, Admirali John Kirby, amesema wanaamini kuwa IS imepoteza viongozi wake muhimu wa ngazi za juu na kati, miongoni mwao ni Haji Mutazz, naibu wa kiongozi mkuu wa IS, Abu Bakr al-Baghdadi.

Wengine ni Abdulbasit, ambaye alikuwa akishughulikia wapiganaji wa kigeni, na Radhwin Talib, ambaye alikuwa msimamizi wa IS kwenye mji wa Mosul. Jarida la Wall Street liliripoti hapo awali kwamba vikosi vya Marekani vilikuwa vimewalenga viongozi kadhaa muhimu wa IS, likimnukuu Mkuu wa Majeshi, Jenerali Martin Dempsey.

Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya IS mwezi Agosti mwaka huu, ambayo sasa yanazijumuisha nchi kadhaa washirika, ndani na nje ya Ghuba na Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba