1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazozana Jamhuri ya Afrika ya Kati zakubaliana

9 Aprili 2015

Pande mbili zinazozozana katika Jamhuri ya Afrika ya Kati zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Nairobi nchini Kenya

https://p.dw.com/p/1F5CU
Picha: AFP/Getty Images/M. Medina

Makubaliano hayo muhimu yalitiwa saini hapo jana kati ya muwakilishi wa kundi la waasi wa Anti Balaka Joachim Kokate na muwakilishi wa kundi la waasi wa Seleka aliyekuwa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati michel Djotodia mjini Nairobi.

Taarifa kutoka kwa ofisi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta imemnukuu rais huyo akiwaambia waliotia saini makubaliano hayo, kwamba ''kutakuwa na watu wengi watakaojaribu kusababisha migawanyiko miongoni mwa pande zinazozozana kwa maslahi yao ya kibinafsi'' lakini akawasifu viongozi wa makundi hayo kwa kuonyesha undugu

Rais Samba Panza hajashirikishwa

Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Januari mwaka huu, yalitaka serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati inaoyoongozwa na Rais Catherine Samba Panza kubadilishwa lakini matakwa hayo hayakutambulika na serikali ya Bangui.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa/ZUMA Press

Rais Samba Panza hajakuwa sehemu ya mchakato huo wa kutafuta amani ulioanzishwa na Rais wa Congo Brazaville Denis Sassou Nguesso. Makubaliano hayo ya Januari pia yalikataliwa na jumuiya ya kiuchumi ya nchi kumi za Ukanda wa Afrika ya Kati CEEAC na tangu wakati huo pande hizo mbili hasimu zimekubaliana kuitambua serikali ya mpito iliyoko madarakani.

Mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo Keneth Marende, spika wa zamani wa bunge la Kenya amesema utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na kutafuta amani ni kigezo muhimu katika kuelekea kuamua hatma ya taifa hilo la Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na msukosuko tangu mwaka 2013 baada ya mapinduzi ya serikali yaliyomng'oa madarakani Rais Francois Bozize na kulitumbukiza taifa hilo katika machafuko yenye msingi katika tofauti za kidini kati ya wakristo na waislamu.

Vita vimekuwa CAR tangu 2013

Waasi wa Seleka walinyakua mamlaka mwezi Machi mwaka 2013 na kumuidhinisha Michel Djotodia kuwa rais na kumfanya kiongozi wa kwanza wa kiislamu kuwa Rais nchini humo.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel Djotodia
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel DjotodiaPicha: Getty Images/Afp/Eric Feferberg

Djotodia alilazimika kujiuzulu mwaka 2014 kufuatia shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kuwadhibiti waasi waliokuwa wakifanya maovu kote nchini yakiwemo mauaji, ubakaji na uporaji wa mali.

Ni wakati huo kundi la waasi la kikiristo la Anti Balaka lilipoundwa na kuanza mashambulizi makali ya kulipiza kisasi na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu na mamilioni wengine kuachwa bila ya makaazi katika taifa hilo maskini.

Wachambuzi wanatilia shaka mazungumzo hayo ya kutafuta amani ya Nairobi na hawana imani juu ya uwezo wa makundi hayo ya waasi kuyatekeleza yaliyofikiwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwenyewe.

Mwandishi: Caro Robi/Afp

Mhariri: Daniel Gakuba