1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza mpango wa kupambana na Ebola

17 Septemba 2014

Rais Barack Obama wa Marekani, ametangaza mpango wa kupeleka wanajeshi 3,000 Afrika Magharibi, katika juhudi za kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola, uliolikumba eneo hilo.

https://p.dw.com/p/1DDm4
Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Reuters

Akizungumza katika Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa-CDC, huko Atlanta, Georgia, Rais Obama amesema wanajeshi hao watatoa msaada wa kitabibu pamoja na vifaa katika nchi ziliozoathiriwa na Ebola na kwamba makao makuu ya kikosi hicho, yatakuwepo kwenye mji mkuu wa Liberia, Monrovia.

Wanajeshi hao watasimamia ujenzi wa zahanati mpya na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kitakuwa chini ya Meja Jenerali Darryl Williams, ambaye ni mkuu wa jeshi la Marekani barani Afrika.

Rais Obama, amesema ugonjwa wa Ebola unatishia usalama wa dunia na ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuzuia maambukizi ya virusi hivyo, ambavyo vinaenea kwa kasi sana.

Wahudumu wa afya wa Liberia wakiuondoa mwili wa mtu aliyekufa kwa Ebola.
Wahudumu wa afya wa Liberia wakiuondoa mwili wa mtu aliyekufa kwa Ebola.Picha: Reuters/James Giahyue

Amesema ugonjwa wa Ebola ni janga katika eneo la Afrika Magaribi, unaenea kwa kasi na kwa sasa maelfu ya watu wa Afrika Magharibi wameathirika na idadi hiyo inaweza ikaongezeka na mamia ya maelfu ya watu wanaweza kuambukizwa. Rais Obama amezitaka nchi mbalimbali duniani kutoa haraka msaada wa kifedha, vifaa pamoja na wataalamu wa afya.

Australia yatangaza msaada zaidi

Australia leo imetangaza kuwa itatoa mara moja Dola milioni saba zaidi za Australia ili kusaidia juhudi za kimataifa za kupambana na virusi vya Ebola. Awali nchi hiyo ilitangaza kutoa Dola milioni moja za Australia katika kusaidia kupambana na ugonjwa huo. Tayari Cuba na China zimesema zitapeleka wataalamu wake wa afya nchini Sierra Leonne.

Ama kwa upande mwingine, Shirika la Afya Duniani-WHO, limeonya kuwa maambukizi ya Ebola huenda yakaongezeka mara mbili zaidi, kila baada ya wiki tatu. Shirika hilo linakadiria kuwa ugonjwa huo huenda ukagharimu kiasi cha Dola bilioni moja kuweza kuudhibiti.

Balozi wa Liberia nchini Ujerumani, Ethel Davis
Balozi wa Liberia nchini Ujerumani, Ethel DavisPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Zaidi ya watu 2,400 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola katika nchi za Guinea, Liberia, Nigeria na Sierra Leone, huku Liberia ikiwa ni nchi iliyoathirika zaidi. Akihojiwa na DW, Balozi wa Liberia nchini Ujerumani, Ethel Davis amesema inajulikana wazi kuwa ugonjwa wa Ebola hauna tiba na maambukizi yake yanaenea kwa kasi, hivyo jumuiya ya kimataifa inapaswa kuungana pamoja na kusaidia kuutukomeza kabisa ugonjwa huo.

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amesema jana kuwa umoja huo unaongoza juhudi za kimataifa kupambana na Ebola na utauzungumzia ugonjwa huo kwenye mikutano yake ya wiki ijayo, mjini Geneva.

Nalo Shirika la Misaada la Madktari wasio na Mipaka-MSF limeonya kuwa mwitikio wa kupambana na Ebola umepungua vibaya na hatua za mara moja zinahitajika ili kudhibiti mripuko huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman