1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni wakati wa kuzungumza amani

9 Mei 2014

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi wa nchi hiyo Riek Machar wanakutana Ijumaa hii mjini Addis Ababa, katika mazunguzo ya kwanza ya ana kwa ana tangu kuanza kwa mgogoro wa nchi hiyo ambao umeuwa maelfu.

https://p.dw.com/p/1BwpS
Südsudan Juba Riek Machar Salva Kiir 09.07.2013
Picha: Reuters

Mkutano kati ya mafahari hao wawili wa Sudan Kusini unakuja wakati ambapo Umoja wa Mataifa umesema kuwa huenda pande zote katika mgogoro wa nchi hiyo uliyodumu kwa karibu miezi mitano sasa zimetenda uhalifu wa kivita.

Ukionya juu ya ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ulisema kuna sababu za msingi kuamini kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu umetendeka wakati wa mgogoro huo na serikali pamoja na wapinzani wake.

Mwanajeshi wa Sudan Kusini akiwa kandoni mwa bunduki ya rasharasha iliyofungiwa kwenye gari mjini Malakal.
Mwanajeshi wa Sudan Kusini akiwa kandoni mwa bunduki ya rasharasha iliyofungiwa kwenye gari mjini Malakal.Picha: Reuters

Ripoti ya Umoja wa Mtaifa iliyotolewa siku ya Alhamis, wakati wa maandalizi ya mazungumzo kati ya Kiir na Machar, imetokana na mahojiano zaidi ya 900 na waathirika na mashuhuda wa machafuko.

"Kilichotokea mjini Juba, ni sawa na kilichotokea kwa Wadinka mjini Bor, Malakal, na pia katika mji wa visima vya mafuta wa Bentiu, hivyo wote wametenda unyama bila kujali kwa kiwango gani. Kila upande unapaswa kuwajibishwa," alisema Admund Yakin, mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini Sudan Kusini.

Matumaini ya suluhu

Jamii ya kimataifa sasa imeweka matumaini yake katika mkutano huo wa kwanza kati ya mahasimu hao wawili,ambao wanatarajiwa kuafikiana juu ya namna ya kuukomesha mgogoro huo, kuruhu ufikishwaji wa misaada ya kiutu kwa wanaouhitaji, na kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mgogoro huo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry, alisema baada ya ziara fupi nchini Sudan Kusini, kuwa rais Salva Kiir yuko tayari kujadiliana juu ya kuundwa kwa serikali ya mpito. Na inavyoonekana Kiir anataka aendelee kuiongoza serikali hii ya mpito, hadi uchanguzi utakapofanyika mwakani. Swali ni iwapo kiongozi wa waasi Riek Machar, ambaye mara zote amemtaka Kiir kujiuzulu, atalikubali hilo.

Mkutano wa leo mjini Addis Ababa ndiyo jaribio la pili kukomesha mapigano baada ya makubaliano ya Januari 23, ambayo hata hivyo yalikiukwa na pande zote, kukiwa na matumaini madogo kwamba raia watapata ahueni kutokana na vurugu hizo.

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa katika kambi ya Umoja wa Mataifa mjini Juba.
Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa katika kambi ya Umoja wa Mataifa mjini Juba.Picha: Reuters

Hofu ya njaa na mauaji ya halaiki

Mpatanishi wa mgogoro huo kutoka jumuiya ya IGAD Lazaro Sumbeiywo kutoka nchini Kenya katika mahojiano na DW alisifu uamuzi wa wawili hao kukutana, na kusema kuwa viongozi hao wawili pekee ndiyo wanaweza kumaliza mgogoro huo.

Pia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema ana matumaini ya kurejea haraka kwa amani kufuatia mkutano wenye ufanisi kati ya rais Kiir na Machar. Ban aliwashinikiza wawili hao wakati wa ziara yake mjini Juba siku ya Jumanne kukubali kushiriki mkutano wa leo.

Wakati huo huo, raia wanazidi kukabiliwa na hali ya mateso kutokana na kuchacha kwa mapigano, na mashirika ya misaada yanaonya kuwa Sudan Kusini iko katika kingo za kukumbwa na baa kali zaidi la njaa tangu miaka 1980, wakati waziri John Kerry na mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay wakielezea hofu kwamba nchi hiyo inaweza kutumbukia katika mauaji ya halaiki.

Mwandishi: Katrin Mattaei/Iddi Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo