1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu atetea hotuba yake Marekani

4 Machi 2015

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameitetea hotuba yake aliyotoa katika bunge la Marekani – Congress dhidi ya shutuma za Rais wa Marekani Barack Obama.

https://p.dw.com/p/1EkzE
USA Benjamin Netanjahu Rede vor dem Congress
Picha: Getty Images/W. McNamee

Netanyahu anahoji kuwa aliwasilisha “pendekezo mbadala” kuhusiana na makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kati ya Marekani na Iran ya mpango wa nyuklia.

Vita vya maneno kati ya Obama na Netanyahu vinaonekana vitachukuwa muda mrefu kutulia, baada ya hotuba ya hapo jana ya Netanyahu mbele ya bunge la Marekani, ambayo alitumia muda mwingi kukosoa mpango wowote wa mataifa ya Magharibi, ikiwemo Marekani, kufikia makubaliano juu ya programu ya nyuklia ya Iran. Obama alisema hotuba hiyo ya Netanyahu haikutoa mpango mwingine mbadala wa kuizuia Iran dhidi ya kutengeneza silaha za nyuklia.

Lakini baada ya kutua nchini Israel, Netanyahu alipuuzilia mbali kauli ya Obama akisema alitiwa moyo na jibu alilopata kutoka kwa Warepublican na Wademocrat. Katika hotuba yake katika bunge la Marekani, waziri mkuu huyo wa Israel alisema makubaliano yaanayotarajiwa kufikiwa kati ya Marekani na Iran kabla ya mwisho wa mwezi huu, yanaifungulia njia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Nchini Israel, kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour Isaac Herzog alielezea wasiwasi kuwa uharibifu umefanyika katika mahusiano ya Israel na Marekani ambayo ni mshirika wake mkuu. Wakosoaji wa serikali wamesema kuwa hotuba yake ilikuja ikiwa imesalia wiki mbili tu kabla ya Israel kuandaa uchaguzi wa bunge, wakati Netanyahu akionekana kuyumba katika uchunguzi wa maoni.

Isaac Herzog
Kiongozi wa upinzani wa chama cha Labour nchini Israel Isaac HerzogPicha: picture-alliance/EPA/JIM HOLLANDER

Iran pia imeipuuzilia mbali hotuba hiyo ya Netanyahu huku msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Marzieh Afkham akiishtumu Israel kwa kueneza uwongo

Na wakati Obama na Netanyahu wakiendelea kutoa mitazamo tofauti, Marekani na Iran zilikamilisha leo mazungumzo yao ya siku tatu nchini Uswisi. Lakini maafisa wa Marekani wamesema “changamoto kali” bado zipo, wakati muda wa mwisho wa Machi 31 wa kufikia makubaliano hayo ukikaribia.

Huku wakipuuza ombi la waziri mkuu wa Israel kusitisha mazungumzo hayo, mjumbe mkuu wa Marekani John Kerry na Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif waliendelea na mazungumzo yao mjini Montreux.

Lakini afisa mmoja wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani amekiri kuwa “ukweli wa mambo ni kuwa hakuna muafaka wowote utakaotangazwa na yeyote hii leo”. Kerry sasa atasafiri kuelekea Riyadh ili kuwapa taarifa washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba kuhusu muafaka unaokaribia kufikiwa pamoja na mipango ya kukutana mjini Paris siku ya Jumamosi pamoja na wenzake wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef