1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Ghuba za Kiarabu zagoma kupunguza uzalishaji wa mafuta

22 Desemba 2014

Nchi za Ghuba za Kiarabu zenye utajiri wa mafuta zimesimama kidete dhidi ya nchi zenye kuzalisha mafuta ghafi ambazo sio wanachama wa Shirika la OPEC na kuapa kutopunguza kiwango cha uzalishaji.

https://p.dw.com/p/1E8VM
Viongozi wa nchi za Ghuba za Kiarabu.
Viongozi wa nchi za Ghuba za Kiarabu.Picha: picture-alliance/dpa/A. Haider

Nchi za Ghuba za Kiarabu zenye utajiri wa mafuta zimesimama kidete dhidi ya nchi zenye kuzalisha mafuta ghafi ambazo sio wanachama wa Shirika Linalosafirisha Mafuta kwa Wingi Duniani OPEC na kuapa kwamba hazitopunguza kiwango cha uzalishaji na wala kuitisha mkutano wa dharura wa shirika hilo kusaidia kuimarisha bei ya mafuta.

Wazalishaji wakuu wa mafuta katika shirika la OPEC Saudi Arabia na Kuwait zimesema hazitopunguza kiwango cha uzalishaji hata kama nchi ambazo sio wanachama wa OPEC zitapunguza uzalishaji wao wakati Umoja wa Falme za Kiarabu na Iraq zikipuuza wito wa kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa shirika hilo.

Saudi Arabia imezilaumu nchi ambazo sio wanachama wa OPEC kwa koporomoka huko kwa bei ya mafuta.Imesema haitopunguza kiwango chake cha uzalishaji iwapo nchi nyengine hazitoanza kuchukuwa hatua hiyo.

Ali al-Naimi waziri wa mafuta wa Saudi Arabia amewaambia waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa nishati hapo Jumapili mjini Abu Dhabi Umoja wa Falme za Kiarabu kwamba nchi zisizo wanachama wa OPEC zinataka kupunguza uzalishaji zinakaribishwa lakini sio Saudi Arabia haitofanya hivyo.

Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia Ali al-Naimi.
Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia Ali al-Naimi.Picha: dapd

Amekaririwa akisema "Hatujuwi nini kitakachotokea kipindi cha usoni.Kile tunachokijuwa kwa uhakika ni kwamba nchi zenye uzalishaji mkubwa na ulio bora ndizo zitakazodhibiti soko."

Zashupalia msimamo wao

Waziri wa mafuta wa Kuwait Ali al-Omair akiunga mkono kauli ya Saudi Arabia amesema hafikiri kwamba kuna haja ya kupunguza uzalishaji na kwamba licha ya kutowa fursa kwa nchi nyengine kufanya hivyo nchi hizo haziko tayari kuchukuwa hatua hiyo.

Ameongeza kusema kwamba OPEC haitopunguza uzalishaji na kwamba hakuna kitakachotokea hadi mwezi wa Juni na pia hakutokuwa na mkutano wa dharura.

Soko la mafuta duniani limezidi kuwa na ushindani katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya mwamba tope kutoka nchi ambazo sio wanachama wa shirika la OPEC lilioundwa miongo mingi iliopita.

Sababu za kushuka kwa bei

Bei za mafuta zimeshuka kwa takriban asilimia 50 tokea mwezi wa Juni kwa kiasi kikubwa kutokana na kushehena kwa usambazaji, uchumi dhaifu wa dunia na dola ya Marekani kuwa na nguvu.Wachambuzi wengine wanasema sababu nyengine ya kuyumba kwa bei ya mafuta ni ongezeko la uzalishaji wa gesi mwambatope.

Mtambo wa kusafisha mafuta Iran nchi mwanachama wa OPEC.
Mtambo wa kusafisha mafuta Iran nchi mwanachama wa OPEC.Picha: AP

Waziri wa mafuta wa Iraq Adel Abdulmahdi akifuta uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa dharura amesema inabidi wasubiri kuona jinsi masoko na nchi yatakvyokabiliana na hali hiyo.Anaamini kwamba bei ya mafuta itatulia na kuja kuwa dola sitini kwa pipa.

Saudi Arabia,Kuwait,Umoja wa Falme za Kiarabu,Qatar na Iraq huzalisha mapipa milioni 20 kwa siku au theluthi mbili ya mafuta ya yanayozalishwa na OPEC.

Shirika hilo mwezi uliopita liliamuwa kuendelea na kiwango cha uzalishaji wake wa mapipa milioni 30 kwa siku jambo ambalo limepelekea kuanguka kwa bei za mafuta.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mwandishi : Gakuba Daniel