1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yamuapisha rais mpya

Mjahida29 Mei 2015

Rais mpya wa Nigeria aliyeapishwa rasmi hii leo Muhammadu Buhari amesema, Ufisadi, ugaidi, ukosefu wa ajira na matatizo ya umeme ni mambo ambayo yanapewa kipaumbele katika masuala ya kisiasa ya Nigeria.

https://p.dw.com/p/1FZDo
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: Getty Images/AFP/P. Utomi Ekpei

Buhari, mwenye umri wa miaka 72 aliapishwa rasmi mjini Abuja Nigeria, mbele ya takriban wageni 20,000 walioalikwa wakiwemo marais zaidi ya 50 na wawakilishi wa serikali kuu ulimwenguni. Buhari alijipatia ushindi wa asilimia 54 ya kura katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 mwezi Machi, dhidi ya rais wa zamani Goodluck Jonathan aliyeiongoza Nigeria kwa miaka mitano.

"Tunakabiliana na changamoto chungu nzima, ukosefu wa usalama, ufisadi, pamoja na ukosefu wa umeme na mafuta, haya ndio mambo tunayopaswa kuyashughulikia mara moja," alisema rais Buhari katika hotuba yake.

Rais Buhari pia ameahidi kupambana na kundi la wanamgambo wa Boko Haram waliosababisha mauaji ya watu 14,000 tangu ilipoanza uasi wake miaka yapata sita iliyopita, Kiongozi huyo mpya wa Nigeria vile vile ameahidi kuimarisha kikikosi cha wanajeshi wa majini.

Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari akiapishwa mjini Abuja
Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari akiapishwa mjini AbujaPicha: Reuters/A. Sotunde

Aidha aliwapongeza wote waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia kura akisema kwamba wao pia wamechangia katika mchakato mzima wa kuwa na uvhaguzi huru sawa na haki. Wakati huo huo Buhari amesema atahakikisha kuna uwajibikaji katika vitengo vyote vya serikali vilivyochini yake.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alikuwepo katika sherehe ya leo ya kuapishwa rasmi Muhammadu Buhari kama Rais mpya wa Nigeria. Wengine waliokuwepo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na mjumbe maalum wa China Han Changfu.

Baadhi ya Viongozi wa Afrika pia walioalikwa katika sherehe hizo ni rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, rais Alpha Conde wa Guinea rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pamoja na rais wa Ghana John Dramani Mahama anayeongoza Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS.

Rais Muhammadu Buhari aapa kupambana na Boko Haram

Nigeria Hata hivyo imekuwa na historia ndefu ya mvutano wa maeneo yake ya mipaka na kidini. Rais Buhari ambaye ni Muislamu kutoka eneo la Kaskazini ameapa kuwawakilisha raia wote kwa kuzingatia haki na usawa.

Umati wa watu ulimshangilia Buhari mara baada ya kuapishwa kuliongoza taifa hilo kwenye mji mkuu wa Abuja, huku wakipiga kelele wakisema ''Sai Baba'', wakimaanisha ''Ni Baba yetu'' kwa lugha ya Hausa.

Kuapishwa kwa Buhari kumeweka historia nchini Nigeria kwa mara ya kwanza kabisa kwa chama tawala kwenye nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Afrika, kukabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa upande wa upinzani.

Rais wa Zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais mpya wa nchi hiyo
Rais wa Zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan na rais mpya wa nchi hiyoPicha: Reuters/Afolabi Sotunde

Baada ya kuapishwa Buhari alimshukuru rais anayeondoka madarakani, Goodluck Jonathan kwa kuonyesha uzalendo katika kuweka historia kwa ajili yao, hali iliyowafanya Wanigeria kujivunia kuwa raia wa nchi hiyo na kuona fahari popote pale walipo.

Katika kuashiria ukurasa mpya wa kisiasa nchini Nigeria, Rais Buhari aliyekuwa amevalia joho/kanzu nyeupe alirusha hewani njiwa weupe pamoja na maputo ya rangi mbalimbali kwenye uwanja wa Eagle Square, tukio lililofuatiwa na kufyetuliwa mizinga kama ishara ya heshima.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri yusuf Saumu