1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msumbiji wachagua serikali mpya

Admin.WagnerD15 Oktoba 2014

Raia wa Msumbiji wamepiga kura Jumatano katika uchaguzi mkuu unaotizamiwa kukirejesha madarakani chama tawala cha Frelimo, kilichoiongoza nchi hiyo kw akaribu miongo minne.

https://p.dw.com/p/1DW1s
Wahlen Mosambik 15.10.2014 Filipe Nyusi
Picha: Reuters/Grant Lee Neuenburg

Vituo vya kupiga kura vilifunguliwa saa moja za asubuhi kote nchini, humo. Zaidi ya raia milioni 10 wameandikishwa kupiga kura katika uchaguzi huo wa rais, bunge na mabaraza ya mikoa.

Wawekezaji wa kigeni na wafadhili wana matumaini kwamba uchaguzi huo utazika uhasama ambao bado ungalipo tokea vita vya wenyewe kwa wenyewe 1975 hadi 1992, pale serikali ya Frelimo na waasi wa Renamo ambacho sasa ni chama halali cha kisiasa waliposaini mkataba wa amani mjini Roma.

Raia akipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Msumbiji uliyafanyika Jumatano.
Raia akipiga kura katika uchaguzi mkuu wa Msumbiji uliyafanyika Jumatano.Picha: Getty Images/AFP/Gianluigi Guercia

Matumaini ya raia

Kwa raia wa Msumbiji wenyewe, matumaini yao ni kuwa yeyote atakayeshinda uchaguzi atazitumia mali asili, makaa na gesi kumaliza umasikini, kuleta hali ya usawa na kuunda nafasi za ajira.

Mwanafunzi mmoja wa uhandisi Elder Mesquita mwenye umri wa miaka 24 alisema wakati umefika sasa kwa viongozi kuufikiria zaidi umma.

Dereva mmoja wa taxi katika mji mkuu Maputo Antonio Fernando mwenye umri wa miaka 35 anahisi wakati wa mabadiliko umefika, akionyesha kutofurahishwa na viongozi kutokana na tabia ya kujilimbikizia mali.

"Wamekuwa wakijitajirisha tu. Kwa miaka 40 sasa ahadi ni zile zile. Tumechoka . Sio wajinga tena kukandamizwa ndani ya mfumo wa chama kimoja. Hatuko tena miaka ya 80 bali karne ya 21. Tunamtazamo tafauti kabisa," alisema dereva huyo.

Kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama baada ya kupiga kura.
Kiongozi wa Renamo Afonso Dhlakama baada ya kupiga kura.Picha: AFP/Getty Images/Gianluigi Guercia

Upinzani wa Renamo

Frelimo kilicho madarakani tangu uhuru 1975, kimemsimamisha waziri wa zamani wa Ulinzi Filipe Nyusi mwenye umri wa miaka 55, katika uchaguzi wa rais. Hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa kiongozi wa chama cha Renamo Afonso Dhlakama mwenye umri wa miaka 61.

Dhlakama ameshindwa uchaguzi wa rais mara nne, na katika uchaguzi wa 2009 alikishutumu chama cha Frelimo kwa mizengwe akidai kulikuwa na wizi wa kura. Mgombea mwengine ni Daviz Simango wa chama cha Demokrasia MDM, ambacho kimetokeza kuwa nguvu ya tatu ya kisiasa nchini humo.

Chama hicho kiliundwa na Simango alipo jitoa kutoka Renamo 1997. Simango ana umri wa miaka 50 na mtoto wa makamu wa zamani wa Rais wa Frelimo Urio Simango. Rais mpya atachukuwa nafasi inayoachwa na Armando Guebuza baada ya kumaliza mihula miwili, kwa mujibu wa katiba.

Mwandishi. Mohammed Abdul-Rahman.
Mhariri: Iddi Ssessanga