1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kusitisha mapigano wafikiwa Yemen

22 Septemba 2014

Maafisa wa serikali ya Yemen na waasi wa madhehebu ya Shia wamesaini mkataba wa amani kufuatia siku kadhaa za machafuko ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 140 na maelfu wengine kukimbia makwao.

https://p.dw.com/p/1DGia
Jemen Unterzeichnung Friedensvertrag
Picha: Reuters/M. al-Sayaghi

Muafaka huo unatoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano, na kuundwa serikali ya watalaamu katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya kufanya mashauriano na vyama vyote vya kisiasa. Akizungumza katika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari na Rais Abed Rabbo Mansour Hadi katika mji mkuu Sanaa, mjumbe wa Umoja wa Mataifa Jamal Benomer alisema kiongozi wa serikali siyo lazima atoke katika chama chochote cha kisiasa. Aliongeza kuwa vikosi vya usalama vinastahili kufanyiwa marekebisho baada ya mashauriano na vyama vya kisiasa. "Muda umetimia sasa wa kuweka kando maslahi ya kibinafsi na kuyaweka mbele maslahi ya taifa. Ipo haja ya kuwajibika katika utekelezaji wa makubaliano ya mkutano huu na kujenga taifa jipya lililokubaliwa na Wayemen".

Rais Abed Rabbo Mansour Hadi alisema mkataba huo unaanza kutekelezwa maramoja. "Mpango wa kusitisha mapigano unaanza maramoja mjini Yemen. Tumesaini mkataba huu ili kusitisha umwagaji damu wa wayemen ambao unafanyika katika kila mtaa. Tunawajibika kwa ajili ya watu wetu na kwa kuweka chini silaha na tutashirikiana kuyatekeleza masharti ya muafaka huu".

Jemen Gefechte zwischen Schiiten und Sunniten
Waasi wa Houthi wamekuwa wakipambana kwa siku kadhaa na vikosi vya serikali katika mji mkuu SanaaPicha: Reuters

Lakini saa kadhaa kabla ya muafaka huo kutangazwa, waziri mkuu Mohammed Salem Bassindwa alitangaza kujiuzulu kwake kutoka serikalini. Hii ni baada ya waasi wa kishia wanaofahamika kama waHouthi kuyakamata majengo kadhaa muhimu ya serikali katika mji mkuu Sanaa, ikiwa ni pamoja na wizara ya Ulinzi, Benki Kuu, kambi muhimu ya Kijeshi na Chuo Kikuu cha Iman. Wizara ya ulinzi kisha baadaye ilikanusha ikisema hali ni tulivu na kuwa jengo lake halikuvamiwa.

Katika miezi ya karibuni, WaHouthi waliwang'oa maadui wao wenye itikadi kali za kiislamu katika msururu wa mapambano kaskazini mwa Sanaa, na katika siku za karibuni wameimarisha na kupanua udhibiti wao wa maeneo ya upande wa kaskazini mwa mji mkuu. Wapinzani wao toka zamani wanayajumuisha makundi ya wapiganaji wa Kisunni yenye itikadi kali za kiislamu ambayo yana mafungamano na serikali au chama cha siasa kali cha Islah. Waasi wa Houthi wamekuwa wakishinikiza mabadiliko ya serikali na kile wanachokiona kama usawa wa kugawana madaraka.

Wahouthi walifanya uasi wa miaka sita ambao ulikamilika rasmi katika mwaka wa 2010. Mwaka uliofuata, wimbi la megeuzi katika ulimwengu wa Kiarabu likaitikisa nchi hiyo, na mwishowe kumlazimu Rais Abdullah Saleh kuondoka madarakani mwaka wa 2012 kama sehemu ya mpango ulioungwa mkono na Marekani wa kumpa kinga ya kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameyakaribisha makubaliano hayo kati ya serikali na waasi, akitoa wito wa “muafaka huo kutekelezwa haraka na kwa kikamilifu”.

Mwandishi: Bruce Amani /AP
Mhariri: Iddi Ssessanga