1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa UKIMWI wawaenzi wahanga wa MH17

Klaus Jansen21 Julai 2014

Zaidi ya wataalamu na wanaharakati 100 wa UKIMWI walifariki baada ya kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia, lakini mkutano wa kimataifa unaendelea mjini Melbourne. DW inamulika baadhi ya mambo yanayojadiliwa.

https://p.dw.com/p/1Cfz6
AIDS Konferenz Melbourne
Picha: picture-alliance/dpa

Licha ya mshtuko na simanzi vilivyofuatia habari za ajali ya ndege hiyo na kufariki kwa wataalamu hao, mkutano huo wa kimataifa uliyopangwa kufanyika kuanzia Julai 20 hadi 25 ulifunguliwa rasmi Jumatatu chini ya kaulimbiu ya "Hatua kuelekea ulimwengu usiyo na ukimwi."

Kwa mujibu wa wenyeji wake - shirika la kimataifa la kupambana na ukimwi, nembo ya mkutano huo - ambayo ni miguu minne iliyochorwa katika muundo wa utepe, inawakilisha kuongezeka kwa uelewa wa kisayansi, kitabibu na kijamii kwa ugonjwa wa ukimwi.

Ukubwa tofauti wa miguu iliyomo kwenye nembo hiyo unalenga kuashiria namna watu wa umri na jinsia tofauti wanavyoathiriwa na ukimwi - huku wote wakiwa katika njia moja.

Nembo ya mkutano wa mwaka huu inaashiria jinsi watu wa umri na jinsia tofauti wanavyoathiriwa na ukimwi.
Nembo ya mkutano wa mwaka huu inaashiria jinsi watu wa umri na jinsia tofauti wanavyoathiriwa na ukimwi.Picha: aids2014

Uzuwiaji mpana

Waathirika wa ukimwi hawapaswi kubaguliwa au kunyanyapaliwa - na takwa hili ndiyo msingi mkuu wa mkutano wa mwaka huu. Karibu washiriki 12,000 walijiandikisha kushiriki mjadala juu ya hali na maendeleo ya utafiti wa ukimwi. Ugonjwa huo unaendelea kukosa tiba na hivyo uzuwiaji unazidi kuwa sehemu muhimu ya utafiti.

Dawa zinazouzuwia ugonjwa huo kusambaa katika mwili ni moja ya mada za mkutano huo. Katika ajenda upo pia mjadala juu ya kile kinachojulikana kama tiba ya kuzuwia kwa watu wasio na virusi vya ukimwi, alisema mtaalamu wa Ukimwi, Profesa Norbert Brockmeyer, na kuongeza kuwa tiba hii inaweza kuzuwia sehemu kubwa ya mambukizi ya virusi vya ukimwi.

Profesa Brockmeyer anasema baadhi ya masuali yatakayojadiliwa ni namna ya kuzuwia maambukizi kwa watoto, na hasa katika mataifa yanayoendelea, na njia bora za kuwahudumia kina mama - maswali ambayo wanasayansi watahitaji kuyapatia majibu.

Mafanikio na changamoto

Siku chache kabla ya mkutano huo, Umoja wa Mataifa ulichapisha takwimu mpya zinazoonyesha kuwa watu milioni 2.1 waliambukizwa na virusi vya ukimwi katika kipindi cha mwaka uliyopita. Lakini katika hatua ya kutia moyo, profesa Brockmeyer alisema idadi ya watu waliofariki ilipungua kwa laki mbili na kuwa milioni 1.5.

Siasa na serikali moja moja zinatoa mchango mkubwa katika mjadala juu ya ukimwi - mchango huu unahusisha miongoni mwa mambo mengine, kutoa muongozo juu ya kuyashughulikia makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya ukimwi, ambayo Umoja wa Mataifa uliyachapisha mwezi wa Julai.

Mada muhimu ni kuhusu unyanyapaji dhidi ya mashoga, machangudoa na watumiaji wa madawa ya kulevya. Katika baadhi ya mataifa, sheria zinayabagua makundi hayo, na hii inatoa mwanya kwa virusi kuenea, alisema Profesa Brockmeyer.

Tamko la Melbourne linasisitiza juu ya kutendewa sawa kwa makundi yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa ukimwi.
Tamko la Melbourne linasisitiza juu ya kutendewa sawa kwa makundi yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa ukimwi.Picha: michaeljung - Fotolia

Tamko la Melbourne

"Hakuna alieachwa nyuma," ndiyo kichwa cha tamko la mkutano wa Melbourne, lililoandaliwa kabla ya kuanza kwa mkutano huo. Moja ya matakwa ya tamko hilo ni ukomeshwaji wa ubaguzi na unyanyapaa. Tamko hilo linazitaka serikali zote kuweka utaratibu wa kisheria wa kuyashughulikia kwa usawa, makundi yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa ukimwi na kumhakikishia kila mmoja upatikanaji wa tiba na taarifa.

Mashirika kadhaa ya kimataifa tayari yamesaini tamko hilo, yakiwemo Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, shirika la Kifaransa la Sidaction and Aids, na Mtandao wa kupambana na Ukimwi barani Ulaya.

Itachukuwa muda hadi kupatikana kwa chanjo au dawa ya kutibu ukimwi, lakini Profesa Brockmeyer anaamini wako katika njia sahihi. Brockmeyer anaamini ajali mbaya ya ndege iliyogharimu maisha ya wenzao, itaongeza msukumo wa utafiti zaidi katika ukimwi, katika kuwaenzi wahanga wa ajali hiyo.

Mwandishi: Heise Gudrun/DW
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Josephat Charo