1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watetezi wa mazingira wayataka mataifa kuunga mkono

Admin.WagnerD22 Januari 2015

Umoja wa Mataifa, utafanya jaribio lake la tatu na la mwisho kufikia makubaliano la kuanzisha majadiliano ya kuwepo mkataba wa kimataifa kuhusu viumbe anuwai, ambao utadhibiti shughuli za eneo la bahari la kimataifa.

https://p.dw.com/p/1EPBJ
SYMBOLBILD USA verstärken Marine-Präsenz vor syrischer Küste - Kriegsschiff im Pazifik
Picha: Jose Cabezas/AFP/Getty Images

Mkutano wa siku nne wa kamati maalumu ya Umoja wa Mataifa ulitarajiwa kufanya maamuzi siku ya Ijumaa, kuhusu muda wa mwisho uliyowekwa wa Septemba mwaka huu, kuanza majadiliano juu ya pendekezo la mkataba huo.

Mshauri mwandamizi wa sera wa shirika la kimataifa la mazingira la Green Peace Sofia Tsenikli, aliliambia shirika la habari la IPS, kuwa mkutano huu ndiyo nafasi ya mwisho ya kufikiwa uamuzi juu ya kuanzisha majadiliano hayo.

Eneo kubwa zaidi duniani lisilo na udhibiti

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, muungano wa mashirika ya kutetea mazingira wa High Seas Alliance, ulisema eneo la bahari la kimataifa ni kubwa sana, likichangia karibu theluthi mbili ya eneo la bahari zote na karibu asilimia 50 ya eneo zima la sayari ya dunia, lakini hadi sasa haliko chini ya udhibiti wa serikali yoyote ya kitaifa.

"Hii inamaanisha kuwa bahari hizo ndiyo eneo kubwa zaidi lisilo na ulinzi wala utawala wa kisheria duniani," ulisema muungano huo. Ukosefu wa utawala kwenye bahari za kimataifa unaelezwa kama moja ya sababu kuu zinazochangia kuchafuliwa kwa bahari kunakosababishwa hasa na shughuli za kibinaadamu.

Shirika la Green Peace limelitaka baraza la UN kuunga mkono majadiliano ya kuanzisha mkataba wa kulinda bahari.
Shirika la Green Peace limelitaka baraza la UN kuunga mkono majadiliano ya kuanzisha mkataba wa kulinda bahari.Picha: Robert Visser/Greenpeace

Masuala yatakayojadiliwa yanahusisha maeneo ya majini yaliyohifadhiwa na tathmini za athari za kimazingira katika maeneo yaliyo nje ya udhibiti wa serikali za mataifa, na vilevile ushiriki wa manufaa ya rasilimali za kijenetiki za majini, ujenzi wa uwezo na uhamishaji wa teknolojia ya majini.

Umuhimu wa kuwa na mkataba

Wakati huo huo, muungano wa High Seas unasema kitisho kinachozidi kukuwa kutokana na shughuli za binaadamu, zikiwemo uchafuzi wa mazingira, uvuvi uliyopitiliza, uchimbaji, uhandisi wa kijiolojia na mabadiliko ya tabianchi, vimefanya kuwepo kwa mkataba wa kimataifa wa kulinda bahari, kuwa muhimu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea.

Mchakato huo uliyoanzishwa wakati wa mkutano mazingira wa Rio+20 nchini Brazil mwaka 2012, umechambua kwa kina kuhusu ukubwa na uwezekano mfumo mpya wa kimataifa, chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1994, kuhusu sheria ya baharini, kwa ufipi UNCLOS.

Wakati wa mkutano wa Rio+20 mataifa wanachama yalikubali kuanzisha majadiliano kuhusu mkataba mpya kufikia mkutano mkuu wa 69 wa baraza la Umoja wa Mataifa Septemba 2015. Makundi ya kutetea mazingira yanasema kuna uungwaji mkono mkubwa kwa mkataba wa utekelezaji wa maazimio ya UNCLOS kutoka kwa mataifa na makundi ya kikanda duniani, kuanzia mataifa ya kusini-mashariki mwa Asia, hadi serikali za Afrika, mataifa ya Ulaya na Amerika Kusini na pia mataifa madogo ya visiwa yanayoendelea.

Bahari ya kimataifa ndiyo eneo kubwa zaidi ulimwenguni lisilo na sheria zinazoliongoza.
Bahari ya kimataifa ndiyo eneo kubwa zaidi ulimwenguni lisilo na sheria zinazoliongoza.Picha: picture alliance/akg-images

Ni lipi eneo la bahari ya kimataifa?

Kwa mujibu wa kundi la mazingira, bahari ya kimataifa inaelezwa kama eneo la bahari lililoko mbali na ukanda wa kiuchumi wa taifa lolote - linalofikia asilimia 64 ya bahari - na kina cha bahari kilichoko mbali na mwambao wa bara la taifa lolote lile.

Maeneo hayo yanachangia asilimia 50 ya uso wa dunia na yanahusisha baadhi ya mifumo ya ekolojia yenye umuhimu wa kipekee kwa mazingira na inayokabiliwa na kitisho kikubw azaidi ulimwenguni.

Muungano huo unasema ni mkataba wa kimataifa kuhusu bio anauwai za bahari za kimataifa, unaoweza kushughulikia mifumo dhaifu ya kisheria inayoshindwa kulinda bahari za kimataifa na hivyo bahari zote duniani - kutokana na vitisho zinavyokabiliana navyo katika karne hii ya 21.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ips
Mhariri: Saumu Yusuf