1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Kobani waendelea kushambuliwa

19 Oktoba 2014

Ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani zimeshambulia maeneo ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kwa karibu mara sita katika mji wenye mapigano nchini Syria wa kobane jana Jumamosi(18.10.2014).

https://p.dw.com/p/1DYIJ
Kämpfe um Kobane 16.10.2014
Mji wa Kobani ukishambuliwaPicha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Wanamgambo wa Dola la Kiislamu walifanya mashambulio makubwa ya makombora , kwa siku kadhaa na kutikisa eneo la kati la mji wa Kobani na kupiga pia maeneo ya mpakani ndani ya Uturuki.

Mashambulio ya makombora yaliendelea baada ya mashambulio ya anga katika eneo la kati la Kobane. Makombora kadhaa yaliangukia ndani ya Uturuki karibu na kivuko cha mpakani , kinachojulikana kama Mursitpinar, kwa mujibu wa walioshuhudia.

Kämpfe um Kobane 15.10.2014
Mji wa KobaniPicha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Wanamgambo wa Dola la Kiislamu wamekuwa wakipambana na wapiganaji wa Kikurdi kwa muda wa mwezi sasa kuwania udhibiti wa mji wa Kobane na kumiliki eneo la kilometa 95 la ardhi wanayoidhibiti katika mpaka na Uturuki , lakini mashambulizi ya anga yaliyoimarishwa katika siku ya hivi karibuni yamesaidia kuzuwia kusonga mbele wanamgambo hao.

Kampeni dhidi ya Dola la Kiislamu yashika kasi

Majeshi ya muungano yamekuwa yakishambulia maeneo ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Iraq tangu Agosti na kuendeleza kampeni hiyo hadi Syria mwezi wa Septemba baada ya kundi hilo la wanamgambo ambao hapo kabla walikuwa wanalenga kupambana na majeshi ya utawala wa rais Bashar al-Assad wa Syria , kupata mafanikio makubwa ya kukamata maeneo.

Kämpfe um Kobane 13.10.2014
Mapambano ya kuudhibiti mji wa KobaniPicha: Reuters/Umit Bektas

Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO kwa kiasi fulani inasita kujiunga na muungano huo, ikisisitiza kwamba jumuiya hiyo ya kujihami inapaswa pia kupambana na Assad kufikisha mwisho vita ya uovu ambayo imesababisha kiasi ya raia 200,000 kuuwawa tangu Machi mwaka 2011.

Raia wauwawa katika mashambulizi

Jana Jumamosi(18.10.2014),shirika lenye makao yake makuu nchini Uingereza linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema majeshi yanayoongozwa na Marekani yanayoshambulia kwa mabomu maeneo ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Syria yameuwa raia 10 katika mashambulio mawili tofauti ya anga.

Flüchtlinge aus Kobane 16.10.2014
Wakimbizi kutoka mji wa KobaniPicha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Lakini uongozi wa jeshi la Marekani umesema hakuna ushahidi wa kuthibitisha ripoti hiyo. Majeshi yake yanatumia hatua maalum kupunguza uwezekano wa vifo vya raia, msemaji amesema.

Shirika la habari la Reuters haliwezi kuthibitisha kwa njia huru ripoti hiyo kutokana na vizuwizi vya kiusalama.

Mjini Kobane , kamanda wa wanamgambo wa Kikurdi wanaoulinda mji wa kobani , ambae ametoa jina lake la siri Dicle, amesema mashambulizi mapya ya kundi hilo la Dola la Kiislamu yalikuwa na nia ya kuutenga mji huo wa mwisho ambao ni kiunganisha na Uturuki.

Kämpfe um Kobane 16.10.2014
Ndege za kijeshi za muungano unaoongozwa na MarekaniPicha: Reuters/Kai Pfaffenbach

Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema wanamgambo wa Dola la Kiislamu wamefanya mashambulizi karibu 21 ya makombora siku ya Jumamosi karibu na mpaka na Uturuki.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Amina Abubakar