1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 65 ya Jamhuri ya Umma wa China

Mohamed Abdulrahman30 Septemba 2014

Chama cha kikoministi nchini China leo kinaadhimisha miaka 65 tangu kilipotwaa madaraka na kutangaza Jamhuri ya Umma wa China Oktoba 1 mwaka 1949, chini ya Uongozi wa Mwenyekiti Mao Tse Tung.

https://p.dw.com/p/1DNnv
Mao Zedong Mao Tse-tung China 1960
Mwenyekiti wa kwanza wa chama cha Kikoministi cha China Mao Tse-tungPicha: Getty Images

Sherehe hiyo ya taifa inasherehekewa huku maandamano ya kudai demokrasia zaidi yakiigubika Hong Kong iliokuwa ikitawaliwa na Uingereza kabla ya kurejeshewa China 1997.

Sherehe hiyo leo inafanyika huku waandamanaji Hong Kong wakiendelea na dai lao la kutaka waachiwe wenyewe kumchaguwa waziri wao mkuu, bila ya kuingiliwa na utawala mjini Beijing. Maandamano hayo yanafuatia hatua ya China kwamba itaruhusu uchaguzi 2017 , lakini itabakia na mamlaka ya kuyapitia majina ya wagombea na kuwa na haki ya kuyachuja.

Uingereza iliitawala Hong Kong kwa zaidi ya miaka 150.China kwenyewe, chama tawala cha Kikoministi kina tafsiri yake ya demokrasia , kile kinachoitwa " Demokrasia ya Kijamaa," kukifanyika mageuzi machache tu kama uhuru wa kugombea nyadhifa chamani kwa ushindani na uwajibika mkubwa zaidi serikalini.

Kwa mujibu wa muongozo wake, Chama cha Kikoministi hakiwezi kupingwa na lazima kiendelee kutawala .

Hata hivyo chama hicho kinataka kuendelea kusheshimu maendeleo na uhuru wa kidemokrasia katika Hong Kong chini ya msingi wa kiwango kikubwa cha kujitawala wenyewe kwa miaka 50, baada ya mkoloni wa zamani Uingereza kuikabidhi China. Vyombo vya habari vya taifa , vilimnukuu Kiongozi wa chama cha Kikoministi Xi Jinping aliyeshika hatamu miaka miwili iliopita,akiwaambia wafanyabiashara kutoka Hong Kong mjini Beijing wiki iliopita kwamba chama kitaendelea kuunga mkono mkondo wa maendeleo ya demokrasia katika Hong Kong, chini ya muundo wa sheria.

Maandamano ya Hong Kong ambamo wengi ni wanafunzi, yanakumbusha vuguvugu la kudai demokrasia nchini China juni 4 , mwaka 1989 na ukandamizaji uliofanywa na jeshi katika uwanja wa Tiannanmen mjini Beijing. Na Hong Kong ndiko mahala pekee nchini China ambako watu wanaweza kukumbuka hadharani matukio hayo ya 1989, ambapo wanafunzi huyaita " mauaji ya Tiannanmen.

China Studentenprotest in Hongkong Occupy Central Regenschirme und Polizei
Maandamano ya kudai demokrasia zaidi Hong KongPicha: Reuters/B. Yip

Wakosoaji wanasema kutokana na msimamo wa China wa kushawishi nani awe waziri mkuu mtendaji wa Hong Kong, muundo wa taifa moja , mifumo miweili ya kisiasa umo hatarini.

Wako wanaohofia maandamano ya upinzani ya muda mrefu Hobng Kong , yanaweza kuisababisha serikali mjini Beijing kuchukuwa hatua sawa na ile ya Tiannanmen.

Wapinzani wawili maarufu nchini China Teng Biao na Hu jia, walitoa wito wiki iliopita wakiitaka Marekani kuipa China onyo kali kwamba ukandamizaji wowote kwa matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji wanaokusanyika kwa amani, utapingwa vikali na kukabiliwa kwa hatua madhubuti.

Chama cha Kikoministi nchini China kina wasiwasi kuenmdelea kwa maandamano ya upinzani Hong Kong kunaweza kukawachochea wanaharakati nchini China nao kuingia mitaani .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpae
Mhariri : Josephat Charo