1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na viongozi wa Balkan

Elizabeth Shoo28 Agosti 2014

Mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya unalenga kuimarisha uhusiano wa kibiahsra kati ya umoja huo na nchi za Balkan. Viongozi wa nchi nane watahudhuria kikao hicho Berlin.

https://p.dw.com/p/1D31r
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani
Picha: Reuters

Mkutano huu unajumuisha viongozi wa nchi nane za Balkan zikiwemo Albania, Kosovo, Macedonia, Serbia and Montenegro, Slovenia na Croatia. Hii ni mara ya pili kwa Merkel kukutana na viongozi hao katika kipindi cha muda mchache. Mwezi Julai mwaka huu, Kansela wa Ujerumani alifanya ziara mjini Dubrovnik, Croatia na kuhudhuria mkutano kama huu. Nia ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya ni kuyahimiza mataifa ya Balkan yaweke mikakati ya kubadili sera za kisiasa na kiuchumi. Pamoja na hayo, mataifa hayo yametakiwa kumaliza uhasama miongoni mwao ambao umekuwepo kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso pia atauhudhuria mkutano wa Berlin. Anasindikizwa na kamishna wa nishati Günther Oettinger na kamishna wa upanuzi Stefan Fule.

Umoja wa Ulaya umesema unataka kuonyesha kwamba bado inaziunga mkono nchi za Balkan. Hii ni baada ya mataifa hayo kutokupewa kipaumbele na Umoja wa Ulaya kwa sababu ya migogoro inayoendelea Ukraine na Mashariki ya Kati.

Safari ndefu kufikia Umoja wa Ulaya

Nchi nyingi zinazohudhuria mkutano wa leo zimeazimia kujiunga na Umoja wa Ulaya. Ndio maana Umoja huo unataka kukaza ushirikiano wa kibiashara kati yake na nchi za Balkan ili nchi hizo zipige hatua moja zaidi kuukaribia Umoja wa Ulaya. Mpaka sasa ni Croatia na Slovenia tu zilizofanikiwa kupata uanachama.

Eneo la Balkan limepitia migogoro mingi kama vita vya Croatia mwaka 1991
Eneo la Balkan limepitia migogoro mingi kama vita vya Croatia mwaka 1991Picha: picture alliance/dpa

Nchi zilizobalkia bado zina safari ndefu hadi ziweze kuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya. Ni nchi ambazo bado zinapambana na matatizo sugu kama vile rushwa. Mbali na hayo, utawala wa sheria haufuatwi na viongozi wote. Uchumi nao bado si imara. Kabla ya nchi yoyote kupewa uanachama wa Umoja wa Ulaya, lazima ianzishe muundo mpya kabisa wa uchumi.

Macedonia ndio taifa ambalo kwa sasa lina uwezekano mkubwa zaidi wa angalau kupewa nafasi ya kuomba uanachama wa Umoja wa Ulaya. Lakini hata kama mazungumzo hayo yataanza itaichukua Macedonia miaka kadhaa hadi kweli kuingia kwenye umoja huo.

Kwa upande mwingine, uhasma kati ya makabila makuu matatu ya raia wa Bosnia-Herzegovina umelifanya taifa hilo lishindwe kupiga hatua za maendeleo ili kutimiza masharti ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuomba uanachama.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef