1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mradi wa kinuklea wa Iran Magazetini

25 Novemba 2014

Kurefushwa mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran na halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya kukabiliwa na kura ya kutokua na imani ya bunge la Ulaya ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1Dsct
Mawaziri wa Mambo ya nchi za nje wa madola matano makuu yenye kura ya turufu katika baraza la usalama,na Ujerumani katika mazungumzo ya mradi wa kinuklea wa Iran mjini ViennaPicha: picture-alliance/dpa/Roland Schlager

Tuanzie lakini Vienna ambako jana mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi tano zenye kura ya turufu katika baraza la usalama la Umoja wa mataifa na Ujerumani pamoja na mwenzao wa Iran walikubaliana mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran yarefushwe hadi julai mosi ili kurahisisha kufikiwa makubaliano ya kuridhisha.Gazeti la "Badische Zeitung" linahisi kimsingi pande zote zinataka makubaliano yafikiwe.Gazeti linaendelea kuandika:"Mtu anaweza kusema bado watu wamedhamiria kufikia makubaliano.Iran inasumbuliwa na vikwazo,nchi za magharibi nazo zingependelea kushirikiana na Teheran katika mapambano dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam na Urusi ingendelea sana kubainisha ina uwezo wa kufuata siasa ya nje ya maana.Dhamiri hizo lakini zinakabiliana na misimamo mikali ambayo bado haikubadilika.Mpaka sasa Iran bado inaendelea kuhoji mradi wake wa kinuklea haukulengwa kutengeneza bomu la atomiki.Mpaka leo nchi hiyo haionyeshi kama iko tayari kusitisha angalao kwa miaka michache mipango ya kutengeneza bomu hilo.Kwamba mvutano kwa hivyo unaendelea si ajabu.Kama vile ambavyo si ajabu kuona pande hizo mbili zikirejea tena katika meza ya majadiliano hivi karibuni.

Frankfurter Allgemeine lina maoni sawa na hayo na linaandika:"Hakuna anaetaka kurejea katika enzi za malumbano.Lakini pia kila mmoja angependelea kurejea nyumbani baada ya majadiliano kama hayo akiwa na matokeo ya kuridhisha.Na hilo ladhihirika halijawezekana mjini Vienna.Mzizi wa fitina bado ni kuhusu idadi ya mitambo ya kurutubisha urani na ndio maana mazungumzo yanarefushwa mara moja tu...na uwezekano wa kufikiwa makubaliano ni mkubwa..."

Halmashauri ya Jucker yakabiliwa na kura ya kutokua na Imani

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu changamoto zinazoikabili halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inayoongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Luxemburg Jean-Claude Juncker.Alkhamisi ijayo halmashauiri hiyo itakabiliwa na kura ya kurokuwa na imani ya bunge la Ulaya.Gazeti la "Flensburger Tageblatt" linaandika:"Hajakosea mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker aliposema taasisi hiyo inasumbuliwa na hali ya ukosefu mkubwa wa imani inayowapa kichwa zaidi wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Halmashauri ya Juncker si madhubuti:Hasa kwa kuchaguliwa chanzo cha madeni ya Ufaransa Moscovici asimamie bajeti ya halmashauri hiyo,kamishna wa masuala ya nishati kutoka Hispania hakufafanua kikamilifu shughuli zake pamoja na makampuni ya mafuta,na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje kutoka Italia anaebidi kwanza ajikusanyie maarifa kutoka majukwaa ya kimataifa.Halmashauri kuu binafsi ndiyo inayobeba dhamana ya Umoja wa Ulaya kupoteza imani.Hata kama itasamilika na kura ya kutokuwa na imani kutokana na wingi wa kura wa vyama vya kuihafidhina na kijamaa ,hata hivyo itadhoofika kidogo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman