1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu Iran yaingia ''mita za mwisho''

2 Aprili 2015

Wanadiplomasia wa nchi sita zenye nguvu duniani na wenzao wa Iran wamefanya mazungumzo usiku kucha, katika juhudi za kutafuta muongozo wa makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/1F1fH
Mazungumzo yameendelea siku mbili baada ya muda wa mwisho kupita
Mazungumzo yameendelea siku mbili baada ya muda wa mwisho kupitaPicha: Tasnim

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif wamekuwa na majadiliano ya ana kwa ana hadi karibu alfajir ya leo, wakijaribu kupata muafaka katika mazungumzo magumu ya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran wenye utata. Naibu kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na sera za nje Helga Schmid alishirikia pia katika mazungumzo ya wanadiplomasia hao, ambayo yameendelea siku mbili baada ya muda wa mwisho wa tarehe 31 Machi kupita bila kufikia makubaliano.

Akizungumzia hatua iliyofikiwa, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema wamebakiza ''mita chache'' kufika kwenye msitari wa mwisho wa mbio za mazungumzo, na kuongeza kuwa kama inavyojulikana, mita hizo chache za mwisho ndizo ngumu zaidi. Fabius amesema wanazungumzia masuala nyeti ya kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia, na kuisaidia nchi hiyo kurejea katika jumuiya ya kimataifa.

Haja sio kupata makubaliano kwa pupa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ambaye asubuhi ya leo ameahirisha ziara yake ya nchi za Baltiki ili kubakia katika mazungumzo hayo, amealinganisha mazungumzo hayo na ''mapambano magumu'' na kuongeza kuwa wanataka kupata makubaliano yenye uhakika.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: Getty Images/Afp/Fabrice Coffrini

''Kwa vyovyote vile, makubaliano yatakayofikiwa kati yetu na Iran yatakuwa na athari kubwa kwa kila upande, hususan majiran wa Iran. Ndio sababu tunataka kuhakikisha kwamba hatutii saini makubaliano yasio na uhakika, tunataka makubaliano ambayo hayaipi Iran nafasi yoyote ya kuyakiuka.'' Amesema Steinmeier.

Miezi 18 tangu kuanza kwa mazungumzo hayo magumu, bado haijulikani kama Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani, hatimaye zitapata makubaliano yatakayoondoa uwezekano kwa Iran kupata silaha za nyuklia. Mataifa hayo sita ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Ujerumani.

Hakuna anayetaka kuambulia patupu

Lengo ni kupata muongozo wa makubaliano ambao utakuwa msingi wa makubaliano kamili yanayotarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Juni ambayo yatajengwa juu ya vipengele mahsusi vya kiufundi kuhusu mpango huo wa Iran.

Mazungumzo yamekuwa marefu na magumu.Waandishi wakisubiri usiku kucha kupata taarifa
Mazungumzo yamekuwa marefu na magumu. Waandishi wakisubiri usiku kucha kupata taarifaPicha: Isna

Wadau wote katika mazungumzo hayo wanakabiliwa na shinikizo la kupata muafaka ili wasirudi nyumbani mikono mitupu, lakini jana Marekani ilieleza bayana kwamba iko tayari kuyapa kisogo mazungumzo hayo, ikiwa msingi wa makubaliano hautapatikana.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington, kwamba umewadia muda kwa Iran kufanya uamuzi. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ambaye alionekana kuwa mwenye matumaini, alisema wanapiga hatua kusonga mbele.

Hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo ndio nfursa ya kwanza ya kukaribiana kati ya Iran na Marekani, tangu mapinduzi ya mwaka 1979 nchini Iran. Hata hivyo, hali hiyo inakabiliwa na upinzani wa makundi yenye misimamo mikali katika kila upande.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga