1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yasubiri mapendekezo ya Athens

23 Februari 2015

Hatima ya makubaliano ya kuweka chini silaha Ukraine,mbio za sakafuni za waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na mjadala kama watoto wachanjwe kwa lazima dhidi ya surua ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi

https://p.dw.com/p/1EfzP
Serikali ya Ukraine na waasi waanza kubadilishana wafungwaPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Vadim Ghirda

Tunaanzia Ukraine ambako matumaini yameanza kuchomoza pengine makubaliano ya pili ya Minsk yataheshimiwa.Gazeti la "Eisenacher Presse" linaandika:"Katika yale maeneo yanayohusika na mpango wa kuweka chini silaha nchini Ukraine,kuna ishara ya kupatikana utulivu baada ya waasi wanopigania kujitenga,kuuteka mji wa Debalzewo na kusema wataheshimu makubaliano ya pili ya Minsk ikiwa yanaambatana na mkakati wao.Kilichosalia lakini ni kusubiri na kuona kwa umbali gani silaha nzito nzito zitaondolewa,tena na pande zote mbili."

Gazeti la Kieler Nachrichten linatathmini umuhimu kwa pande zote mbili kuheshimu makubaliano ya kuweka chini silaha na kuandika:"Kwasababu ukweli unauma:Nchi za magharibi haziko tayari kuipatia silaha serikali ya mjini Kiev ili iweze kuwashinda nguvu waasi-kwasababu vita vikizidi makali madhara yake hakuna anaeweza kuyakadiria.Putin anaitambua vilivyo hali hiyo na anaitumia kila kukicha.Lakini ukweli pia ni kwamba hata waasi wataweza kujivunia ufanisi wa muda mrefu ikiwa watahakikisha nidhamu na utulivu katika jamii vinaimarika.Bila ya ushirikiano pamoja na serikali ya mjini Kiev,kwa mtazamo wa muda mrefu,hilo halitawezekana.

Mbio za sakafuni

Mada nyengine iliyogonga vichwa cha habari magazetini ni Ugiriki baada ya "makubaliano ya ajabu ajabu" yaliyofikiwa ijumaa iliyopita.Gazeti la "Hannoversche Allgemeine " linajiuliza kama pirika pirika za waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras hazikuwa mbio za sakafuni.Gazeti linaenelea kuandika:"Tsipras amejibwaga uwanjani kama mwanasiasa aliyepania kuiokoa nchi yake.Mjini Brussels lakini alilazimika kujifunza jinsi maamuzi yalivyo magumu .Amejifunza pia jinsi mtu anvyoweza kukabwa na madaraka.Hatimae wagiriki wanajikuta wakibakiwa na matakwa yao tu ya kuachana na mageuzi.Brussels imefanikiwa kuibadilisha hali ya mambo.Kutoka mwanasiasa aliyekuwa akitoa masharti,amesalia yule anaebidi kuwasilisha mkakati.Ulaya inasubiri kwa hamu mapendekezo yatakayotolewa na viongozi wa mjini Athens.Ikiwa matokeo yake yatakuwa kurekebisha sera za malipo ya kodi za mapato kwa Ugiriki,hapo pande zote zitafaidika.

Chanjo ya lazima dhidi ya Surua

Mada yetu ya mwisho magazetini hii leo inahusu mjadala uliozuka humu nchini kama zoezi la kuchanjwa watoto dhidi ya maradhi ya surua liwe la lazima.Gazeti la "Saarbrücker Zeitung" linaandika:"Fikra hiyo haingiii akilini.Nani atahakikisha sheria ya watoto kuchanjwa kwa lazima inaheshimiwa?Na wale watakaopinga watoto wao kuchanjwa watafanywa nini?Hasha,la maana ni kushadidia umuhimu wa chanjo,ili kuitanabahisha jamii.Na hilo linawezekana tu kupitia maelezo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga