1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya Wahouthi yaendelezwa

27 Machi 2015

Ndege za kivita za nchi washirika wa Kiarabu zimeendelea kushambulia kambi za waasi wa Kishia nchini Yemen Ijumaa (27.03.2015) ikiwa ni siku ya pili mfululizo wakiongozwa na Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/1EyeW
Rais Abedraboo Mansour Hadi wa Yemen(kushoto) alipowasili Riyadh (26.03.2015)
Rais Abedraboo Mansour Hadi wa Yemen(kushoto) alipowasili Riyadh (26.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa

Mod

Ndege za kivita za nchi washirika wa Kiarabu zimeendelea kushambulia kambi za waasi wa Kishia nchini Yemen Ijumaa (27.03.2015) ikiwa ni siku ya pili mfululizo wakiongozwa na Saudi Arabia ambayo inaishutumu Iran kwa kufanya uvamizi katika eneo zima la Mashariki ya kati. Mohamed Dahman na mzozo wa Yemen ambao uko hatarini kugeuka kuwa vita vya mawakala.

___________________________

Uasi uliodumu kwa mwezi mmoja wa wapiganaji wa Kishia nchini Yemen umepamba moto na kuja kuwa mzozo wa eneo zima la Mashariki ya Kati ambao unatishia kuivuruga nchi hiyo ilioko ncha ya kusini mwa Rasi ya Arabuni.

Saudi Arabia ambayo inatawaliwa na Waislamu wa madhehebu ya Sunni imeapa kufanya kila iwezalo kuzuwiya kuanguka kwa mshirika wake Rais Abedrabbo Mansour Hadi wa Yemen na kuishutumu Iran nchi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa kuunga mkono unyakuaji wa madaraka wa kundi la Washia wa jamii ya Wahouthi nchini Yemen.

Hadi anayeungwa mkono na mataifa ya magharibi na mataifa ya Kiarabu ya Ghuba amewasili Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia hapo jana wakati maafisa wa serikali wakisema kwamba yuko njiani kuelekea Misri kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa siku mbili wa Umoja wa Waarabu unaofanyika nchini humo mwishoni mwa juma.

Huo ulikuwa ni uthibitisho wa kwanza kuhusu mahala alipo kiongozi huyo tokea waasi walipoanza kuusogelea mji mkubwa wa Yemen kusini wa Aden wiki hii ambapo rais huyo alikuwa amejihifadhi tokea akimbie kifungo cha nyumbani katika mji mkuu wa Sanaa mwezi uliopita.

Ushirika dhidi ya Wahouthi

Saudi Arabia inasema zaidi ya nchi 10 zimejiunga katika ushirika huo wa kupambana na Wahouthi zikiwemo nchi nne za kifalme za ghuba ya Kiarabu.

Mwanajeshi wa Saudi Arabia.
Mwanajeshi wa Saudi Arabia.Picha: imago/Xinhua

Inaripotiwa kwamba Saudi Arabia imewaweka wanajeshi wake 150,000 mpakani na Yemen. Ahmad bin Hassan Asiri ni msemaji wa jeshi na mshauri wa waziri wa ulinzi wa Saudi Arabia.

(O-Ton Asiri)

``Katika hatua hii tuliyonayo hivi sasa hakuna mipango ya kufanya operesheni ya ardhini lakini kutakapokuwa na haja hiyo wanajeshi wa nchi kavu wa Saudia na vikosi vya washirika viko tayari kupambana na aina yoyote ile ya uvamizi.“

Iran yaiingiza katika masuala ya ndani

Ikulu ya Marekani imeelezea wasi wasi wake juu ya repoti kwamba Iran inapeleka silaha nchini Yemen wakati Saudi Arabia imeishutumu Iran kwa kusema inaingilia kati masuala ya ndani ya nchi za KIiarabu iwe Lebanone,Syria, Iraq na nchini Yemen.

Waasi wa Houthi mjini Sanaa.(26.03.2015)
Waasi wa Houthi mjini Sanaa.(26.03.2015)Picha: picture-alliance/dpa/Yahya Arhab

Balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani Adel al-Jubeir ameliambia shirika la habari la Fox News nchini Marekani kwamba inabidi waushughulikie uvamizi wa Iran katika eneo hilo kwa kuwaunga mkono Wahouthi na jaribio lao la kuidhibiti Yemen.

Iran imejibu vikali shutuma hizo kwa kuyaita mashambulizi hayo ya Saudi Arabia kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa taifa la Yemen.

Takriban watu 39 wameuwawa katika mashambulizi hayo ya anga nchini Yemen yaliopewa jina Kimbunga cha Maamuzi dhidi ya Wahouthi.Imeelezwa kwamba mashambulizi hayo yatachukuwa siku chache na sio wiki kadhaa kabla ya kumalizika.

Mwandishi : Mohamed Dahman AFP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu