1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Masaibu ya Messi katika Kombe la Dunia

14 Julai 2014

Kitu cha mwisho alichofanya Lionel Messi katika Kombe la Dunia 2014 ni kuipiga "freekick" iliyopaa juu kabisa ya lango na kupoteza nafasi ya mwisho ya Argentina kusawazisha goli katika fainali dhidi ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/1CcKE
Fußball WM Finale Argentinien Deutschland
Picha: Reuters

Hivi sivyo namna ambavyo mshindi huyo mara nne wa tuzo ya mchezaji bora wa ulimwengu alitaka kumaliza dimba hilo. Ilistahili kuwa Kombe la Dunia la Messi, kama tu dimba la mwaka wa 1986 lilivyokuwa la nguli mwingine wa Argentina, Diego Maradona.

Lakini baada ya kuibeba timu yake katika hatua ya makundi nchini Brazil kwa kufunga magoli manne, Messi alionekana kuishiwa pumzi. Alitengeneza nafasi katika fainali ya jana, lakini wenzake katika timu walikosa ustadi wa kumalizia na kuipa ushindi Argentina. “Nimeumia kwa kushindwa katika njia hiyo. Tulikuwa karibu kuamua kupitia penalti”. Alisema Messi na kuongeza: "Nadhani tulistahili matokeo mazuri kuliko hayo, tulikuwa na nafasi za kufunga.”

Alionekana mwenye kukata tamaa wakati akipokea tuzo ya kuwa mchezaji bora wa kinyang'anyiro hicho, na kisha akasimama kimya mlangoni wanakoingilia wachezaji uwanjani, akiangalia Wajerumani wakipokea kombe.

“Kwa wakati huu, sishughulishwi hata kidogo na kupewa tuzo hiyo. Kitu pekee cha maana kilikuwa ni kulibeba kombe,”. Alisema Messi.

Kocha wa Argentina, Alejandro Sabella, alisema Messi alistahili kupewa tuzo ya mchezaji bora wa dimba “kwa sababu alitekeleza jukumu kubwa sana. Alikuwa nguzo muhimu katika timu yake”.

Messi ameshinda kila kitu kinachostahili kushindaniwa akiwa na timu yake ya Barcelona, lakini wakosoaji wengi wanasema anahitaji kutwaa Kombe la Dunia ili kuwa kwenye kitabu kimoja cha wachezaji mahiri katika historia ya kandanda ulimwenguni.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mwandishi: Iddi Sessanga