1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani vitani dhidi ya IS

13 Septemba 2014

Ikulu ya Marekani imetangaza rasmi Ijumaa(12.09.2014) Marekani iko vitani dhidi ya kundi la Kiislamu lenye imani kali la Dola la Kiislamu, ikitaka kuondoa hali ya mkanganyiko mwingine kuhusiana na sera zake kuhusu Syria.

https://p.dw.com/p/1DBfI
F-35 Kampfflugzeug
Ndege za kijeshi za Marekani zinashambulia maeneo ya wanamgambo nchini IraqPicha: picture-alliance/ap

Katika mahojiano kadhaa ya televisheni waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry ameonekana kusita kutamka kuhusu operesheni zilizopanuliwa za Marekani dhidi ya kundi la IS nchini Iraq na Syria kuwa ni "vita".

Lakini alipotakiwa kuondoa shaka juu ya vipi rais Barack Obama anavyouangalia mzozo huu , ikulu ya Marekani na wizara ya ulinzi hazikuweka shaka yoyote.

John Kerry in der Türkei 12.09.2014
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John KerryPicha: Reuters/B. Smialowski

Marekani vitani na ISIL

"Marekani iko vitani na kundi la ISIL katika hali sawa tulivyo vitani na kundi la al-Qaeda na washirika wengine wa al-Qaeda duniani kote," amesema msemaji wa ikulu ya Marekani Josh Earnest.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani admirali John Kirby amesema kwamba Marekani haipigani katika vita vya mwisho vya Iraq na kutumia lugha kama aliyotumia Earnest.

Rais Obama anatarajiwa kuwa mjini Tampa, jimboni Florida siku ya Jumatano kupata maelezo kutoka kwa makamanda wa juu , katika kituo kikuu cha uongozi wa jeshi la Marekani , ambacho kinashughulikia majeshi ya marekani katika mashariki ya kati.

Irak Ministerpräsident Haider al-Abadi in Bagdad
Waziri mkuu wa Iraq Haider al-AbadiPicha: Reuters

Katika mahojiano siku ya Alhamis, wakati Kerry akifanya ziara katika mashariki ya kati akijenga muungano dhidi ya kundi la IS, alisita kutumia neno "vita" akimaanisha kampeni ya Marekani, akiwaambia watu kutojiingiza katika "homa ya vita".

Kerry amesema , "nafikiri "vita" si neno sahihi lakini ukweli ni kwamba tumo katika juhudi kubwa za kimataifa kuzuwia shughuli za kigaidi."

Mafunzo kwa wapiganaji wapinzani

Wizara ya ulinzi ya Marekani inadhani kuwa inaweza kuwapa mafunzo wapiganaji 5000 wapinzani wenye msimamo wa wastani nchini Syria katika muda wa mwaka mmoja, lakini changamoto ni kubwa.

Wakati rais Barack Obama akitangaza wiki hii kuhusu juhudi kubwa zaidi za kupambana na wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq zilikuja taarifa kwamba Saudi Arabia iko tayari kutoa nafasi ya eneo la mafunzo kwa wapiganaji wa upinzani wa Syria.

Obama - Rede an die Nation
Rais barack Obama wa marekaniPicha: Reuters

Obama amelitaka bunge la Marekani kutoa idhini, na pia kuidhinisha dola milioni 500, kuimarisha mafunzo na msaada mwingine kwa makundi ambayo yanamsimamo wa kati nchini Syria , ambayo yanajikuta yakipambana na wapiganaji wa Dola la Kiislamu pamoja na utawala wa rais Bashar al-Assad wa Syria.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande nae anajiunga na kampeni hiyo inayoongozwa na Marekani ya mashambulizi ya anga yanayolenga kundi la Taifa la Kiislamu, amesema waziri mkuu wa Iraq Haider al-Abadi jana Ijumaa baada ya kukutana na rais wa Ufaransa.

"Rais wa Ufaransa ameniahidi kwamba nchi yake itashiriki katika mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo wa Taifa la Kiislamu," amesema Al-Abadi katika mkutano na waandishi habari akiwa pamoja na Hollande mjini Baghdad.

Francois Hollande und Arnaud Montebourg
Rais wa Ufaransa Francois HollandePicha: Alain Jocard/AFP/Getty Images

"Jumuiya ya kimataifa inapaswa kubeba jukumu la kuzuwia ugaidi kuingia nchini Iraq kutokea Syria," al-Abadi alinukuliwa akisema na gazeti la binafsi nchini Iraq la Alsumaria.

Hollande , ambaye pia alikutana na rais wa Iraq Fouad Massoum, amesema amejadili msaada wa kijeshi na kiutu kutoka Ufaransa kwa ajili ya nchi hiyo ambayo inahangaika kuwaondoa wanamgambo wenye itikadi kali kutoka katika eneo lake la kaskazini na magharibi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Amina Abubakar