1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Iran kuzungumzia nyuklia

9 Juni 2014

Marekani na Iran zinakutana kwa mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja mjini Geneva juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, huku Rais Hassan Rouhani akiwa nchini Uturuki katika ziara inayolenga kuimarisha mahusiano.

https://p.dw.com/p/1CEx3
Ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya Geneva na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya Geneva na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.Picha: Dieter Nagl/AFP/Getty Images

Mazungumzo hayo ya ndani yalitarajiwa kuanza jioni ya leo (9 Juni) yataendelea kwa siku mbili, huku kila upande ukiwa na muelekeo wake.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuyatumia mazungumzo hayo kufikia lengo lake la kujenga ushawishi wa kukomesha vikwazo vya kimataifa ambavyo vimeuumiza vibaya uchumi wake.

Lakini kwa Marekani na washirika wake, lengo ni kuwa na uhakika kwamba kile Iran ikiitacho kuwa ni programu ya amani ya atomiki, si mpango wa siri wa kuunda bomu la nyuklia.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, alisema hapo jana kwamba mazungumzo ya uso kwa uso kati ya nchi yake na Marekani ni muhimu kwani kwa sasa majadiliano yapo kwenye hatua tete.

Ujumbe wa Marekani kwenye mazungumzo hayo unaongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Bill Burns, na mshauri wa ngazi za juu wa Ikulu ya Marekani, Jake Sullivan.

Viongozi hawa wawili walikuwa sehemu ya ujumbe uliokuwa kwenye mazungumzo ya miezi kadhaa ya siri nchini Oman, ambayo yalifanikiwa hatimaye kuifanya Iran na mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kukaa meza moja.

Rouhani ziarani Uturuki

Hii ni mara ya kwanza tangu miaka ya 1980 kwa Marekani na Iran kufanya mazungumzo ya moja kwa moja ya ngazi za juu kuhusiana na masuala ya nyuklia, kando ya mchakato wa mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani.

Rais Hassan Rouhani wa Iran aliye sasa ziarani Uturuki.
Rais Hassan Rouhani wa Iran aliye sasa ziarani Uturuki.Picha: Irna

Kwa muda mrefu mataifa hayo yamekuwa yakisaka mapatano juu ya mpango huo wa nyuklia ya Iran, lakini duru ya mwisho ya mazungumzo mwezi uliopita haikuwa na mafanikio sana, na sasa kumekuwa na wasiwasi kwamba mchakato mzima unaweza kusimama.

Mazungumzo ya Geneva yanafanyika, huku Rais Hassan Rouhani wa Iran akikutana na maafisa wa ngazi za juu wa Uturukik, akiwamo Waziri Mkuu Tayyip Erdogan, katika ziara ya kwanza ya rais wa Iran nchini Uturuki tangu mwaka 1986.

Iran ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa Uturuki, lakini pia ni hasimu mkubwa linapokuja suala la kuwania ushawishi kwenye eneo hilo.

Mchana wa leo, Rouhani alikuwa na mazungumzo na Rais Abdullah Gul, na baadaye kwenye mkutano na waandishi wa habari, viongozi hao waliahidi ushirikiano wa mataifa yao kwenye masuala kadhaa ya kibiashara na siasa za kimataifa.

Rouhani atasaini mikataba kadhaa kati ya mataifa hayo inayokusudiwa kupunguza hali ya kutokuaminiana baina yao, hasa juu ya suala la Syria, ambalo nchi hizo mbili zinazunga mkono pande tafauti. Uturuki inawaunga mkono wapinzani, huku Iran ikimuunga mkono Rais Bashar al-Assad.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman