1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya kura ya maoni Scotland

Abdu Said Mtullya18 Septemba 2014

Wahariri karibu wote wanatoa maoni juu ya kura ya maoni nchini Scotland. Pia wanauzungumzia mkakati wa Rais Obama dhidi ya magaidi wa Dola laKiislamu.

https://p.dw.com/p/1DF7y
Watu wa Scotland wanapiga kura kuamua juu ya mustakabal wao
Watu wa Scotland wanapiga kura kuamua juu ya mustakabal wa nchi yaoPicha: Reuters/Paul Hackett

Mhariri wa gazeti la "Thüringische Landeszeitung" anasema bila ya kujali kile ambacho watu wa Scotland watakiamua kura hiyo ya maoni ni muhimu kwa sababu inawapa wananchi fursa ya kuamua kwa amani juu ya mustakabali wa nchi yao. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linasema zoezi hilo halikuja kama zawadi.

Naye mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten" anasema watu wanaoiunga mkono hoja ya kujitoa kwenye muungano wanatumai kupata mamlaka makubwa ya kujitawala. Lakini mhariri huyo anatahadharisha kwamba biashara na Uingereza itakuwa ngumu .

Mafuta hayatatiririka daima

Mhairi anasema wanaotarajia neema kubwa zaidi baada ya kujitenga wanapaswa kutambua kwamba kwa sasa hakuna anaeweza kutoa uhakika juu ya neema hiyo. Mafuta ya Scotland yaliyopo kwenye bahari ya kaskazini hayataendelea kumiminika daima. Na kwa hivyo mengi yanaweza kuwamo mashakani ikiwa wanaotaka kujitenga watashinda katika kura ya maoni.

Mhariri wa gazeti la "Mindener Tageblatt" anaitathmini kura ya maoni nchini Scotland, katika muktadha wa uhusiano wa nchi hiyo na jumuiya ya kimataifa. Anaeleza kwamba iwapo Scotland itatangamanishwa katika Umoja wa Ulaya na katika Nato, ni jambo la kuotea. Tayari mashaka yanasikika kutoka kwa nchi fulani za Umoja wa Ulaya. Mbali na hayo Umoja wa Ulaya wenyewe unahofia kuyapigia debe maeneo mengine ya Ulaya yanayoweza kuifuata njia ya Scotland. Watu wa Scotland wanacheza patapotea juu ya mustakabal wa bara la Ulaya.

Mkakati wa Obama dhidi ya Dola la Kiislamu
Gazeti la"Die Welt" linauzungumzia mkakati wa Marekani dhidi ya magaidi wa dola la Kiislamu,na anatilia maanani kuwa Rais Obama ameahidi mambo mawili. Kwanza amesema atawashinda wapiganaji wa dola la kiislamu. Na pili amesema hatawarudisha wanajeshi wa Marakeni kule ambako alishawaondoa mnamo mwaka wa 2011 baada ya kupelekwa na Rais wa hapo awali George W Bush.

Ahadi ya Rais Obama ya kuwashinda wapiganaji wa dola la Kiislamu bila ya kuwapeleka askari wake nchini Syria na Iraq itakuwa ngumu kutimizwa. Mkuu wake wa majeshi Jenerali Martin Dempsey, amewasilisha hoja inayotofatiana na ya Rais huyo. Mhariri wa gazeti la "Die Welt" anasema hoja ya Jenerali Dempsey inaashiria kwamba tayari Kamanda huyo ameshaufungua mlango wa kuingilia Syria na Iraq na vijana wake.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman