1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Uhamiaji mkubwa

27 Aprili 2015

Kila siku mamia ya wakimbizi huelekea barani Ulaya. Matumaini yao ya kuwa na maisha mapya ni makubwa zaidi kuliko hofu yao ya kuvuka bahari ya Mediterrania, anasema Mhariri mkuu wa DW Alexander Kudascheff.

https://p.dw.com/p/1FFOQ
Libyen Auffanglager Kararim bei Misrata
Picha: DW/M. Dumas

Ni majira ya machipuko, kwa mara nyingine wakimbizi wanaitafuta njia kwenda barani Ulaya. Sababu za wao kufanya hivyo ni nyingi - umaskini, na mara nyingi umasikini uliyokithiri, ukosefu wa elimu na fursa za ajira. Kuna udikteta, utawala wa mkono wa chuma, mateso, ukandamizaji, vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita vya mara kwa mara na mara nyingine serikali zilizoshindwa, ambako makundi ya uhalifu ndiyo yanatawala.

Ugumu wa maisha na hisia za kukosa matumaini ndiyo vinavyowasukuma watu kuzikimbia nchi zao, kujaribu maisha mapya katika nchi ya kigeni, wakitumaini kupata walau bahati kidogo. Wanakuja kutokea mataifa tofauti, yakiwemo Eritrea, Somalia, Libya, Syria, Iraq na Afghanistan - bila hata kutaja uhamiaji wa ndani katika maeneo yenye migogoro.

Wakimbizi wanaokadiriwa kufikia milioni 50 wako njiani. Safari yao ni hatari na mara nyingi huishia katika kifo kwa sababu hawafanyi wenyewe safari hiyo, bali wanawategemea wasafirishaji wa magendo kuwafikisha katika mataifa ya ndoto zao.

Mhariri mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.
Mhariri mkuu wa DW, Alexander Kudascheff.Picha: DW/R.Mestdagh

Njia zinazotumiwa huwa haziko wazi, mfano kutoka Syria wanapitia Uturuki hadi Algeria, wanavuka jangwa hadi Libya na kisha wanapanda boti kwenda bara la matumaini: Ulaya, hiyo ni iwapo hawakutelekezwa na wasafirishaji wao na kuzama . Biashara hii ya utumwa mamboleo imegeuka kitegauchumi kikubwa cha mabilioni ya dola - ya kikatili na ubeuzi.

Wakimbizi wanaofanikiwa kuingia Ulaya wanarundikwa katika makaazi ya dharura, wakati mwingine hupatiwa huduma za matibabu, na mara nyingi hukabiliwa na kurudishwa kwao katika kipindi cha muda mfupi, au wanazamia na kujaribu kuishi na pia kuzihudumia familia zao, kwa kufanya kazi zisizoruhusiwa, zisizo za heshima na zisizo za ujuzi.

Baadhi hupokea msaada kutoka kwa familia zao, wengine wanasaidiwa na wasamaria wema wanaojitolea kuwasaidia wageni. Huku wengine wanategemea hisani ya mataifa yanayowapa hifadhi, na wengine wengi zaidi hurudishwa kwenye umaskini na ukosefu wa matumaini walioukimbia.

Kwa kuyazingatia hayo yote, DW itakuletea kwa wiki hii nzima mfululizo wa taarifa za undani wa mienendo ya wakimbizi - kuanzia wanapoondoka katika mataifa yao na kuwasili kwao. Tutakuletea mataifa ambayo wakimbizi wanataka kuyaacha nyuma. Tutakueleza juu ya safari ndefu, hatari na wakati mwingine ya mauti. Na tutaeleza nini wakimbizi wanaotafuta hifadhi wanaweza kutarajia nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa ujumla.

Ripoti hizo zitaonyesha hali halisi, matumaini, kuvunjika moyo, mafanikio machache na vizuwizi vikubwa, kushindwa kwa watu na wanasiasa kusaidia. Kupokea wakimbizi, kuwaokoa wawapo baharini - haya ni majukumu ya kibinaadamu. Lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba siyo kila anayetaka kuja Ulaya anaweza kufanya hivyo. Haki ya hifadhi ya ukimbizi ni haki takatifu. Lakini katika hali halisi, haki hiyo kwa sasa imevutwa kupita kikomo.

Kwa maelfu ya wakimbizi walioko kwenye fukwe za Afrika Kaskazini, jambo pekee lililomuhimu, ni boti inayoelekea kwenda Ulaya. Kwao la muhimu ni kuwasili na kunusurika njiani.

Mwandishi: Alexander Kudacheff
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Saumu Yusuf